SADDAM SADICK
Mwanza. Klabu ya Mbao imethibisha kuacha rasmi na kocha wake Amri Said 'Stam’ kutokana na kuendelea na msimamo wake wa kutofanya kazi na Msaidizi wake Ally Bushiri ‘Benitez’.
Kocha Stam ameiongoza Mbao katika michezo 17 ambapo ameiwezesha kuvuna pointi 24 na kukaa nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, huku akiweka rekodi ya kipekee kwa kuifunga Simba hadi sasa.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Solly Njashi aliliambia tovuti ya www.Mwanaspoti.co.tz leo kuwa katika mazungumzo yao na kocha huyo wameafikiana kuachana kutokana na yeye kutokubali kufanya kazi na msaidizi wake.
Alisema kikubwa walichofanikiwa ni kuachana kwa amani kwani hapakutokea msuguano hivyo wataendelea kutambua kazi na mafanikio yake aliyoyaacha ndani ya timu.
“Ni kweli leo tumemalizana na Kocha Said baada ya kubaki na msimamo wake wa kutokufanya kazi na Msaidizi wake Bushiri, kwahiyo tumezungumza tukafikia makubaliano na bahati nzuri hapajatokea mgogoro, tumeachana naye kwa uzuri na kiroho safi,”alisema Njashi.
Mwenyekiti huyo aliongeza kwa sasa timu itakuwa chini ya Bushiri ambaye hata hivyo atabaki kuwa Kocha Msaidizi kama mkataba wake unavyoelekeza na kwamba wanaamini atafanya vizuri.
Alisema kuwa kikubwa ni mashabiki na wadau wa soka Jijini Mwanza kumpa ushirikiano kocha huyo mpya kwa malengo ya kuifanya Mbao kuzidi kufanya vizuri katika mashindano yake.
“Bushiri anabaki kuwa Kocha Msaidizi kutokana na mkataba wake unavyosema,tunaamini atafanya vizuri kikubwa ni kumpa ushirikiano ili tuweze kusonga mbele,”alisema Kiongozi huyo.