Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayay, Kipingu waibuka uchaguzi wa Yanga SC

35343 Pic+mayay Mayay, Kipingu waibuka uchaguzi wa Yanga SC

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati kampeni za uchaguzi wa Yanga zikitarajiwa kuanza leo, wapigakura wametakiwa kufanya tathimini ya kina kuhusu uwezo wa wagombea wanaowataka kabla ya kuwachagua.

Yanga itafanya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji Januari 13, mwaka huu.

Uchaguzi wa Yanga umewaibua baadhi ya vigogo na wachambuzi wa soka ambao wamewataka wapigakura kutumia vyema fursa hiyo kuchagua viongozi makini wenye dhamira ya kuleta maendeleo ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.

Akizungumza Dar es Salaam jana, nahodha wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema wapigakura wana wajibu wa kuchagua viongozi waadilifu na watendaji.

Mayay alisema wapigakura wanapaswa kuwahoji wagombea wanaotaka kuongoza Yanga na amewataka wasichague viongozi kwa kufuata mkumbo au mihemko.

“Wagombea watakapopita kwenye matawi, wanachama wajitaidi kuuliza maswali ya msingi, yale ya kuifunga Simba yametosha, wawaulize mikakati ya kuitoa Yanga kwenye mtikisiko wa kiuchumi na mengine ya maendeleo, “alisema Mayay.

Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Mstaafu, Idd Kipingu alisema wagombea wa nafasi hizo wapimwe kupitia kampeni zao kama wana uwezo wa kuongoza na kuipa Yanga maendeleo.

“Wachague wagombea watakaokuwa tayari kuitumikia klabu, wamsikilize kila mgombea ana sera gani na wampime kama anastahili kuongoza Yanga ama la, “ alisema Kipingu.

Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Samwel Lukumay alisema namna ya mchakato wa kupiga kura, ukumbi ambao uchaguzi utafanyika na mambo mengine yatawekwa bayana leo.

“Taratibu za uchaguzi zitawekwa wazi kwenye mkutano utakaofanyika kesho (leo) ukihusisha kamati yetu ya uchaguzi na ile ya TFF, “ alisema Lukumay.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ally Mchungahela alisisitiza wagombea kufanya kampeni za kistaarabu hadi Januari 12, siku moja kabla ya uchaguzi huo.

Awali, uchaguzi huo uligubikwa na utata baada ya Serikali kuitaka TFF kusimamia uchaguzi huo na nafasi zote zilizokuwa wazi ikiwemo ya mwenyekiti ijazwe.



Chanzo: mwananchi.co.tz