Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Matano mazito 2019 yanayoikabili Tanzania

34377 Pic+matano Tanzania Web Photo

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Leo ni mwaka mwingine, ni mwaka mpya wa 2019 baada ya kumalizika kwa mwaka 2018 jana saa 6:00 usiku na ilipoingia dakika moja, mwaka 2019 ulikuwa umeanza.

Kumalizika kwa mwaka mmoja na kuanza mwaka mwingine, pia masuala mbalimbali ya michezo yanatoka hatua moja na kuingia hatua nyingne.

Wakati mwaka huu unaanza, Tanzania itakuwa kwenye mambo mazito katika medani ya michezo ambayo kimsingi yanaihusu Serikali moja kwa moja wakati mambo mengine ni vyama ay mashirikisho ya michezo husika.

Ligi ya Mabingwa Afrika

Simba ndiye mwakilishi pekee wa Tanzania, Ligi ya Mabingwa Afrika na tayari imeingia hatua ya makundi. Simba itaanza kampeni yake Januari 11 kucheza na JS Saoura ya Algeria katika mchezo wa kwanza.

Simba itacheza mechi tatu nyumbani na tatu ugeninikusaka tiketi ya kuingia robo fainali.

Tayari Serikali imesisitiza kuwa bega kwa bega na timu zote zitakazoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa kwa hali na mali itakapohitaji.

“Kiu ya Watanzania 2019 ni kuvunja rekodi, Simba inatuwakilisha vizuri kimataifa, ni wakati wao kupambana na kuweka rekodi angalau hata ya kufika nusu fainali na ikiwezekana fainali. Sisi kama Serikali tutakuwa nao pamoja,” alisema Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo.

Simba imepangwa Kundi D pamoja Al Ahly ya Misri na AS Vita ya DR Congo.

Fainali za Afcon U-17

Tanzania itakuwa mwenyeji wa fainali za Afrika zitakazoanza jijini Dar es Salaam kuanzia Aprili 14 hadi 28 huku Serengeti Boys ikiwa jicho la Watanzania na itafungua dimba na Nigeria, iko Kundi A pamoja na Angola na Uganda.

Kundi B lina timu za Morocco, Cameroon, Senegal na Guinea.

Mzigo uliopo mbele ni kuyasimamia mashindano na kuhakikisha yanamalizika salama lakini pia kuhakikisha kombe linabaki Tanzania.

Mara kadhaa, Waziri wa Habari, sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amekuwa akiahidi kufanyika kwa mashindano ya mafanikio akisisitiza kuwa Serikali itasimamia kila hatua kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF).

Naye kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo alisema kuwa kilicho mbele yao ni maandalizi na itakapofika mashindano, timu yake itakuwa imeiva vya kutosha kukabiliana na yoyote.

Taifa Stars vs Uganda

Tanzania inataka kukata kiu ya miaka 39, kukata tiketi ya kucheza fainali za Afrika mwaka huu.

Taifa Stars imebakisha mchezo na Uganda siku 82 zijazo ambao utaamua nafasi ya Tanzania.

Ushindi wa Tanzania utategemea matokeo ya Cape Verde na Lesotho kwani endapo Lesotho itashinda, itakata tiketi na kuiacha Stars ikisononeka.

“Bado tunayo nafasi, mechi yetu ya mwisho na Uganda tunahitaji kupambana kufa na kupona ili kujiweka kwenye mazingira mazuri, naomba Watanzania watuamini, vijana watapambana ili kufuzu,” alisema kocha wa Stars Emmanuel Amunike.

Stars ambayo imesalia peke yake Afrika Mashariki baada ya Uganda na Kenya kufuzu, ilipotea njia baada ya kufungwa bao 1-0 na Lesotho katika mchezo ambao ilikuwa lazima kushinda kufufua matumaini ya kushiriki fainali hizo.

Michezo ya Afrika Morocco

Tanzania itatuma wawakilishi kwenye michezo ya Afrika (All African Games) itakayoanza Agosti 23 hadi Septemba 3 nchini Morocco.

Kazi kubwa itakuwa kwa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kushirikiana na vyama vitakavyofuzu kuhakikisha wanapeleka wanamichezo walioiva katika; ngumi, riadha, kuogelea, soka la wanwake, judo na kunyanyua vitu vizito.

Ubingwa wa Riadha wa Dunia

Tanzania itashiriki pia mashindano ya ubingwa wa riadha wa dunia yatakayofanyika Doha, Qatar kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 6 mwaka huu.

Tanzania ambayo haikupeleka wanamichezo wa kutosha kwenye Michezo ya Madola kule Gold Coast, Australia Aprili mwaka jana, ni wazi itatumia mashindano hayo kwa wanariadha kusaka viwango na hadi kufikia mwezi huo, watapatikana wa kutosha.

Mpaka sasa, wanariadha; Failuna Abdi, Stephano Huche, Ezekiel Ngimba na Agostino Sulle tayari wamefuzu kwa mashindano hayo.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania, (RT), Anthony Mtaka alisema mwaka 2019 wa kuweka rekodi nyingine baada ya ile ya mwaka jana ya Alphonce Simbu aliyeshinda medali ya shaba ya marathoni kwenye mashindano hayo ya dunia.

Pia kuna baadhi ya mashindano mengine ambayo ni ya kawaida kwa kanda mbalimbali kama kuwania kufuzu Michezo ya Olimpiki 2020 kule Tokyo, Japan, Michezo ya Kanda za Tano, na Sita Afrika kwa riadha , kikapu, na ngumi pamoja na Chalenji na Kombe la Kagame.



Chanzo: mwananchi.co.tz