Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastraika waiangusha Stars nyumbani

68668 Pic+matokeo

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

UBUTU wa safu ya ushambuliaji ta timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa chini ya nahodha, John Bocco, umeinyima timu hiyo kupata ushindi nyumbani, licha ya kutawala sehemu kubwa ya pambano lao la kwanza kuwania tiketi ya Fainali za (Chan) za 2020.

Kocha Etienne Ndayiragije aliwaanzisha Bocco, Ayoub  Lyanga na Idd Seleman 'Nado' huku akiwaweka benchi Salim Aiyee, Ibrahim Ajibu na Kelvin John aliowaingia kipindi cha pili katika pambano hilo la raundi ya kwanza lililopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Stars ilitawala mpira kwa asilimia 60 za kipindi cha kwanza hasa eneo la kiungo lililokuwa chini ya Jonas Mkude, Abubakar Salum 'Sure Boy' na Hassan Dilunga waliokuwa wakigawa mipira kiufundi wakisaidiwa na krosi za mabeki wa pembeni, Paul Godfrey na Gadiel Michael, lakini washambuliaji walikosa utulivu na kujikuta wakimaliza dakika 90 bila kufunga na Harambee ambao walionekana kuyahitaji matokeo hayo mapema tu.

Matokeo ya jana yanaiweka Stars katika mazingira magumu ya kusonga mbele katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Agosti 4 mjini Nairobi.

Stars itajutia nafasi ambazo ilipata kipindi cha kwanza na kushindwa kuzitumia huku katika kipindi hicho ikifika langoni mwa Kenya mara nne huku Kenya ikifika mara mbili

Harambee Stars ilisubiri hadi dakika ya 13 kufanya shambulizi la kwanza lakini mabeki wa Stars wakiongozwa na Kelvin Yondani na Erasto Nyoni walikuwa makini na kumfanya kipa Juma Kaseja kutosukwasukwa langoni.

Pia Soma

Katika kipindi cha kwanza, Kaseja aliokoa hatari mbili langoni kwake huku kipa wa Harambee akifanya kazi ya ziada kuokoa mashuti ya Stars.

Dakika ya tatu, Stars ilinyimwa penati baada ya beki wa Harambee kuunawa mpira kwenye eneo la hatari uliopigwa na John Bocco ambaye aliuwahi mpira uliopigwa na beki wa Kenya katika harakati za kuokoa ukambabatiza Hassan Dilunga na kumkuta Bocco.

Dakika ya 16, Bocco tena alipiga shuti kali ambalo lilipaa juu ya goli na kutoka nje, Paul Godfrey alishindwa kumalizia mpira wa krosi dakika ya 11 baada ya kuzidiwa nguvu na beki wa Kenya ikawa goli kiki.

Kiungo Jona Mkude nusura awanyanyue mashabiki dakika ya 38 kwa shuti la umbali wa kama mita 30 ambalo kipa wa Kenya alitoka kuucheza bila mafanikio lakini shuti hilo likapita pembezoni mwa mligoti wa kushoto wa goli na kutka nje.

Kama Stars wangekuwa makini wangeenda mapumziko wakiwa mbele, lakini shuti la Hassan Dilunga dakika ya 43 likaokolewa na mabeki na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda kwa Stars.

Kipindi cha kwanza Stars ilipata kona tatu, Harambee Stars haikupata kona yoyote

Kipindi cha pili timu zote zilianza kwa kushambuliana kwa zamu kabla ya Iddi Seleman kuandika bao dakika ya 58 lakini likakataliwa kwa kuwa mfungaji alikuwa ameotea.

Dakika ya 64, mpira wa adhabu ndogo nje kidogo ya 18 uliopigwa na Ibrahim Ajibu aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ayubu Lyanga dakika ya 54 unaokolewa na mabeki wa Kenya, faulo ilitengenezwa na Iddi Seleman ambaye alifanyiwa na mabeki wa Kenya akiwa kwenye muvu.

Kama sio uzoefu wa Kaseja, Harambee wangepachika bao dakika ya 74 baada ya mabeki wa Stars kujichanganya na wachezaji wa Harambee kugongeana pasi safi lakini Kaseja alitumia uzoefu wake kuupanchi mpira uliokokuwa unaelekea golini.

Dakika ya 76 Iddi Seleman nusura afunge baada ya kupokea pasi ya Kelvin John (Mbape) aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Hassan Dilunga  lakini kipa wa kenya na mabeki wake walikuwa makini kuokoa.

Dakika ya 90, Salim Ayee aliyeingia dakika ya 85 kuchukua nafasi ya John Bocco alipiga shuti kali nje ya 18 likapanguliwa na kipa wa Harambee Stars.

Kwa matojkeo hayo Stars inahitaji sare ya aina yoyote ya mabao katika mechi ya marudiano itakayopigwa wikiendi hii nchini Kenya, kama inataka kusonga raundi ya pili ikutane na Sudan, japo rekodi zinaonyesha kwa misimu minne mfululizo ya michuano hiyo tangu 2011-2018 Tanzania haijawahi kupata ushindi kwenye michezo ya ugenini zaidi ya kuambulia sare ambazo hata huzitibulia kwani huwa wameshaharibu nyumbani.

Mwaka 2011, baada ya kupata mchekea kwa Somalia waliocheza mechi moja tu nyumbani na kushinda 6-0, walienda kulala 1-0 katika raundi ya pili dhidi ya Rwanda waliokuwa wametoka nao sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam.

msimu uliofuata yaani 2014, ilipigwa nje ndani na Uganda kwa kufunga 1-0 nyumbani na kulala 3-1 mjini Kampala na katika mbio za kwenda Rwanda kwenye fainali za 2016, ililala 3-0 nyumbani na kutoka sare ya 1-1 ugenini na msimu uliopita walilazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na kutoka suhulu ugenini dhidi ya Rwanda.

Chanzo: mwananchi.co.tz