Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa waliotikiswa na usajili Ligi Kuu

77020 Mastaa+pic

Tue, 24 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Msimu wa Ligi Kuu 2019/2020 unaendelea kushika kasi ambapo imefikia raundi ya tatu.

Wakati ligi hiyo ikiwa haijafika hata robo ya mechi zinazopaswa kuchezwa ili ikamilike, baadhi ya wachezaji wameanza kugeuka lulu na wengine wamejikuta katika wakati mgumu wa kupata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza.

Miongoni mwa wachezaji ambao dalili za kupoteza nafasi katika kikosi cha kwanza kwenye klabu zao zimeanza kujitokeza ni wale ambao msimu uliopita walikuwa tegemeo kwa timu zao.

Ujio wa wachezaji wapya umeonekana kugeuka mwiba kwa wachezaji hao na ikiwa watashindwa kupambana wanaweza kujikuta wakizidi kupotea na hata kuonyeshwa mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu.

Spoti Mikiki inakuletea tathmini ya wachezaji ambao ujio wa nyota wapya umefanya nafasi zao kwenye vikosi vya kwanza ndani ya timu zao kuwekwa rehani.

Pascal Wawa-Simba

Pia Soma

Advertisement
Alikuwa tegemeo kwenye kikosi cha Simba msimu uliopita akicheza na Erasto Nyoni kama mabeki wa kati mbele ya Juuko Murshid na Yusuph Mlipili ambao pia wanacheza katika nafasi hiyo.

Hata hivyo, hakuanza vizuri msimu huu kwa kufanya makosa ya mara kwa mara hasa katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ya Msumbiji ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 na kuifanya Simba itolewe kwa faida ya bao la ugenini.

Kiwango hicho kisichoridhisha cha Wawa kililifanya benchi la ufundi la Simba kuamua kumuweka kando na kuanza kumpanga beki raia wa Brazil, Tairone da Silva ambaye katika mechi mbili dhidi ya JKT Tanzania na Mtibwa Sugar alionyesha kiwango bora kilichokosha wengi. Da Silva ameonyesha kuelewana na Nyoni jambo linalomuweka katika nafasi finyu Wawa kurudi kikosi cha kwanza.

Donald Ngoma-Azam

Msimu uliopita alikuwa ndio tegemeo la Azam FC katika kufumania nyavu ambapo alimaliza akiwa amefunga mabao 11 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo alitengeneza pacha tishio na Obrey Chirwa.

Lakini mambo yamegeuka msimu huu ambapo amekuwa hana nafasi katika kikosi cha kwanza na badala yake benchi la ufundi chini ya Kocha Etienne Ndayiragije limekuwa likimtegemea zaidi mshambuliaji Richard Djodi ambaye amesajiliwa na Azam katika dakika za mwisho kabla ya kufungwa dirisha kubwa la usajili mwezi Agosti.

Kasi, uwezo wa kupiga pasi za mwisho, kufunga mabao, kuchezesha timu na uwezo wa kupiga mipira iliyokufa, vimemfanya Djodi amuweke Ngoma katika nafasi ngumu ya kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Azam.

Stamili Mbonde-Mtibwa

Alianza vyema msimu uliopita akipachika mabao manne katika mechi za mwanzoni za Ligi Kuu lakini akakumbwa na majeraha ambayo yalimfanya awe nje ya uwanja kwa muda mrefu na kujikuta akipoteza nafasi mbele ya Jaffari Kibaya na Juma Liuzio.

Kwa sasa amepona lakini amekutana na changamoto mpya mbele ya kijana Riffat Msuya ambaye ameanza kuwa chaguo la kwanza katika nafasi ya mshambuliaji wa kati wa kikosi cha Mtibwa Sugar na tayari ameshaifungia timu hiyo bao kwenye Ligi Kuu na kuendelea kuwepo kwa Kibaya na Liuzio kunazidi kuiweka rehani nafasi yake.

Juma Nyoso- Kagera Sugar

Kwa takribani misimu minne iliyopita, Nyosso aliyewahi pia kuzitumikia Simba, Mbeya City na Ashanti United alikuwa chaguo la kwanza kwenye nafasi ya mlinzi wa kati wa kikosi cha Kagera Sugar.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni benchi la ufundi la Kagera Sugar linaanza kumuondoa kwenye hesabu zake taratibu, beki huyo mbabe amejikuta akisoteshwa benchi kwenye mechi mbili mfululizo ambazo timu hiyo ilicheza katika Ligi Kuu dhidi ya Biashara United na Alliance FC.

Katika mechi zote mbili, Kocha Mecky Maxime amekuwa akiwatumia mabeki Hassan Isihaka na Erick Kyaruzi kucheza kama walinzi wa kati.

Bahati mbaya zaidi kwa Nyoso ni kwamba Kyaruzi na Isihaka wameonyesha uelewano wa hali ya juu na wameunda safu imara iliyoruhusu bao moja tu jambo linalomuweka kikaangoni mkongwe huyo na hivyo kutakiwa kufanya kazi ya ziada.

Hashim Manyanya- Namungo

Alikuwa ndiye mpishi mkuu wa mabao ya Namungo FC msimu uliopita wakiwa Ligi Daraja la Kwanza huku pia akichangia mengine kwa kufunga na alitabiriwa kuwa mmoja wa nyota watakaong’ara msimu huu wa Ligi Kuu.

Hata hivyo, msimu haukuanza vizuri kwake kwani amejikuta akisotea benchi katika mechi mbili za kwanza huku benchi la ufundi la Namungo FC likiwa na imani kwa wachezaji Bigirimana Blaise na George Makanga ambao wanacheza nafasi ya winga.

Manyanya anapaswa kupambana na kujituma zaidi ili aweze kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza cha Namungo FC kwani kuna ushindani mkubwa kutokana na uwepo wa wachezaji wenye uzoefu kumzidi.

Feisal Salum-Yanga

Msimu uliopita alikuwa akipangwa nafasi ya kiungo namba sita ikionekana wazi ni mpango na mbinu za Kocha Mwinyi Zahera kutaka timu ichezeshwe kuanzia nyuma kutokana na uwezo wa kiungo huyo kutoka Visiwani Zanzibar katika kufanya uamuzi wa haraka na kupiga pasi sahihi pindi awapo na mpira mguuni.

Kwa kiasi fulani Yanga ilionekana kufanikiwa katika hilo lakini changamoto ambayo iliikumba ni kwamba Feisal hakuwa na msaada mkubwa kwenye kuilinda timu na mara kwa mara ikajikuta ikiwa inashambuliwa.

Hilo lilipelekea timu hiyo kumsajili kiungo Abdulraziz Makame ambaye ameonyesha kufanya vizuri kwenye kutimiza jukumu la kuilinda timu na kuichezesha lakini pia yupo Mohammed Issa ‘Banka’ ambaye naye anamudu kucheza nafasi ya kiungo.

Uwepo wa Banka na Makame lakini pia nahodha Papy Tshishimbi, unaonekana wazi utamuweka Feisal katika nafasi finyu ya kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga msimu huu iwapo atashindwa kugangamala. Mabadiliko makubwa yanaweza kutokea msimu huu.

Chanzo: mwananchi.co.tz