Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa saba Yanga kuikosa Mbeya City

89770 Yanga+pic Mastaa saba Yanga kuikosa Mbeya City

Tue, 24 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Yanga itawakosa wachezaji saba wa kikosi cha kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City.

Yanga leo itakuwa ugenini kusaka pointi tatu dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine kabla ya Ijumaa kuikabili Prisons.

Wachezaji wanne Feisal Salum ‘Fei Toto’, Abdulaziz Makame, Mohammed Issa ‘Banka’ na Ally Ally watakosa mchezo huo kwa kuwa wanatakiwa kutoa maelezo kwa kamati ya nidhamu baada ya kuchelewa kuripoti kambini.

Pia Yanga itakosa huduma ya Mrisho Ngassa ambaye ana matatizo ya kifamilia, Kelvin Yondani na Juma Abdul ambao walikuwa na timu ya Kilimanjaro Stars katika mashindano ya Kombe la Chalenji.

Fei Toto, Makame, Banka na Ally walichelewa kujiunga kambini Yanga licha ya Zanzibar Heroes kutolewa mapema tangu Desemba 15 katika Kombe Chalenji nchini Uganda.

Yanga ilicheza mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Iringa United Jumamosi iliyopita bila wachezaji hao ambao hawakuwa sehemu ya maandalizi ya mchezo wa leo.

Akizungumza jana, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli kina Makame watapelekwa kamati ya nidhamu kujadiliwa kabla ya kutolewa uamuzi.

“Wachezaji wanne hawako kambini, watapelekwa kamati ya nidhamu kujieleza kwanini mpaka sasa hawajajiunga na timu ingawa walirejea muda mrefu kutoka mashindano ya Chalenji,”alisema Bumbuli.

Wakati Yanga ikiwakosa wachezaji hao, leo ina kibarua kigumu kupata ushindi mbele ya kocha mpya wa Mbeya City Amri Said ‘Stam’ aliyejaza nafasi ya Juma Mwambusi.

Hii itakuwa mara ya pili Yanga kukutana na Stam mwaka huu akiwa na timu mbili tofauti. Mara ya kwanza ilikuwa Mei 10 Uwanja wa Karume, Mara ambapo aliingoza Biashara United kupata ushindi wa bao 1-0 kabla ya kuivaa Mbao.

Kocha huyo akiwa Mbao aliiongoza katika michezo 17, alishinda sita, sare sita na kupoteza mechi tano, timu yake ilifunga mabao 12 na kufungwa 16. Akiwa Biashara United aliingoza mechi 24, alishinda tisa, sare tisa, kupoteza tisa, ilifunga mabao 23 na kufungwa 23.

Stam atakuwa katika benchi wakati Mbeya City ikiwa kinara wa kufungwa mabao mengi 19. Timu hiyo itamtegemea mshambuliaji Peter Mapunda mwenye mabao matano kuipatia matokeo mazuri.

Tangu Mbeya City ilipopanda Ligi Kuu mwaka 2013 imekutana na Yanga mara sita Uwanja wa Sokoine. Yanga imeshinda mechi tatu, yenyewe imeshinda moja na kutoka sare michezo miwili.

Mara ya Mwisho Mbeya City kuifunga Yanga kwenye uwanja huo ilikuwa Novemba 2, 2016 iliposhinda mabao 2-1.

Wakati huo huo, Azam jana ilinusurika kupokwa Kombe la FA baada ya kushinda kwa penalti 4-1 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 dhidi ya timu ya daraja la kwanza African Lyon.

Chanzo: mwananchi.co.tz