Dar es Salaam. Wakati mwaka 2018 ukionekana kuwa wa nuksi kwa baadhi ya nyota wa Ligi Kuu wengine waliouanza vizuri wameumaliza vibaya tofauti na matarajio ya wengi.
Wachezaji hao wamejikuta wakishindwa kutamba na wengine kuporomoka viwango vyao jambo lililopelekea wengine kusotea benchi, kutokuwa na msaada kwenye timu zao ama kujikuta wakipewa mkono wa kwaheri kwenye timu zao.
Kiungo Mnyarwanda wa Simba, Haruna Niyonzima anaweza kuuelezea mwaka 2018 wa nuksi zaidi kwake kutokana na changamoto alizokutana nazo zilizomfanya apoteze nafasi ndani ya kikosi cha Simba.
Niyonzima ambaye alisajiliwa na Simba kabla ya kuanza msimu wa 2017/2018, alikosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Simba kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara ingawa nyakati nyingine alikuwa na matatizo binafsi yaliyosababisha akosekane uwanjani.
Na katika kudhihirisha jinsi mwaka huu ulivyomuendea vibaya licha ya kuonekana ameanza kurejea kwenye kiwango chake, ameshindwa kulishawishi benchi la ufundi la timu hiyo kumpa nafasi na katika Ligi Kuu msimu huu amecheza mechi zisizozidi mbili.
Staa mwingine ambaye anamaliza mwaka vibaya ni beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul ambaye naye amejikuta akishindwa kuhimili ushindani wa namba na kusotea benchi katika idadi kubwa ya mechi za timu hiyo mwaka huu.
Abdul ambaye alikuwa beki tegemeo wa Yanga miaka kadhaa iliyopita, alijikuta akishindwa kutamba mbele ya mabeki wenzake Hassan Kessy na Paul Godfrey.
Katika mechi za Ligi Kuu msimu uliopita zilizochezwa mwaka huu, beki Hassan Kessy ambaye kwa sasa anachezea Nkana Red Devils ndiye aliyekuwa anapewa nafasi kubwa ya kucheza kwenye kikosi cha Yanga huku Juma Abdul akiwekwa nje.
Wakati wengi wakiamini kuondoka kwa Kessy kungempa unafuu Abdul, msimu huu beki huyo amejikuta akishindwa kupata nafasi mbele ya beki chipukizi, Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye amekuwa akipewa nafasi ya kucheza mara kwa mara na benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha Mwinyi Zahera.
Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Juma Liuzio naye ni miongoni mwa nyota ambao wamejikuta wakishindwa kuchanua katika mwaka 2018 tofauti na ilivyotarajiwa.
Nyota huyo ambaye Simba walimsajili akitokea Zesco United ya Zambia, alishindwa kufunga bao kwenye kikosi cha Wekundu wa Msimbazi katika mwaka huu jambo lililopelekea asiongezwe mkataba mpya na kuamua kutimkia Mtibwa Sugar.
Hata hivyo, ameendelea kuwa kwenye wakati mgumu katika kikosi cha Mtibwa Sugar ambako licha ya kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, amefunga mabao mawili tu kwenye Ligi Kuu msimu huu.
Mfano wa mchezaji mwingine aliyechemka mwaka 2018 ni aliyekuwa mfungaji Bora wa Ligi Kuu msimu wa 2016/2017, Abdulrahman Musa ambaye licha ya kuaminiwa kuwa angeendeleza kasi yake ya kufumania nyavu, alijikuta akipata majeraha ya mara kwa mara lakini hata alipokuwa akipata nafasi ya kucheza, alishindwa kufanya kile kilichotarajiwa.
Mshambuliaji huyo ndani ya mwaka 2018, amefunga mabao yasiyozidi manne kwenye Ligi Kuu akiwa ndani ya jezi za timu ya Ruvu Shooting na JKT Tanzania anayochezea hivi sasa.
Katika kundi hilo pia yupo kipa Said Mohammed ‘Nduda’ ambaye alisajiliwa na Simba mwaka 2017 baada ya kukoshwa na kiwango chake bora alichoonyesha ndani ya jezi za Mtibwa Sugar.
Kipa huyo ndani ya mwaka huu amedaka mechi mbili tu za Ligi Kuu tena ni zile mbili za mwishoni mwa msimu uliopita dhidi ya Kagera Sugar na Majimaji ambazo zilichezwa wakati Simba ikiwa imeshatwaa ubingwa.
Msimu huu, hali ilizidi kuwa ngumu baada ya kusajiliwa kwa kipa Deogratias Munishi jambo lililopelekea apelekwe kwa mkopo kwenye timu ya Ndanda FC.