MIMEFICHUKA kwamba, mastaa wa Yanga wapo kwenye mpango wa kugomea mechi zijazo baada ya kutopewa bonasi zao walizoahidiwa katika mechi tatu kati ya nne walizocheza msimu huu.
Yanga ambayo imeanza msimu huu kwa kasi ikishinda mechi tatu za Ligi Kuu Bara na moja ya Ngao ya Jamii, wikiendi hii itapambana na Azam FC ukiwa ni mchezo wa ligi kuu utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Kwa msimu huu, viongozi wa Yanga wamewaahidi wachezaji wao kwamba, watakuwa wakiwapa bonasi
ya shilingi milioni 20 katika kila ushindi wa mechi za Ligi Kuu Bara.
Mbali na Ligi Kuu Bara, pia walipokuwa wakijiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba uliochezwa
Septemba 25, mwaka huu, wachezaji wa Yanga waliahidiwa shilingi milioni 400 endapo wangeshinda, wakashinda 1-0 kwa bao la Fiston Mayele.
Mmoja wa watu waliopo ndani ya Kambi ya Yanga liyopo Avic Town, Kigamboni, Dar, ameliambia Spoti Xtra kwamba, wachezaji wamekuwa na malalamiko yao ya chini kwa chini juu ya kutopewa bonasi hizo ambazo ni haki yao baada ya kufanikisha kile walichoambiwa.
Mtoa taarifa huyo aliongeza kwamba, wachezaji hao wanadai bonasi zao za mechi tatu ambayo ni sawa na
shilingi milioni 440 kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii na mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Geita Gold na KMC.
“Wachezaji wana hali mbaya kwa sasa, huko kambini hawana furaha ya moja kwa moja kwa sababu zile ahadi walizopewa za bonasi bado hawajapewa zote hali inayowafanya kuwa na mpango wa kutaka kugomea mechi zijazo.
“Viongozi kama wameziba masikio hivi na tunavvyokwenda kucheza na Azam, nadhani kuna
jambo linaweza kutokea. Watu wasishangae ingawa wengi wanaona hivi sasa timu inacheza kwa morali, lakini
itafikia kipindi watachoka.
“Katika mechi nne ambazo tumeshinda kuanzia ile ya Ngao ya Jamii, bonasi iliyotoka ni moja tu ya ushindi
dhidi ya Kagera Sugar ambayo ilikuwa mechi ya kwanza ya ligi msimu huu.
“Baada ya hapo, mechi mbili zilizofuatia dhidi ya Geita Gold na KMC, hakuna bonasi iliyotoka mpaka sasa. Jumlisha na ile ya Ngao ya Jamii ambayo bonasi ilikuwa ni shilingi milioni 400, nayo haijatoka mpaka leo. Hapo jumla ni shilingi milioni 440.
“Hizo bonasi zilizowekwa msimu huu, ushindi katika ligi kuu ni shilingi milioni 20, lakini mechi kubwa zile za dabi, inakuwa tofauti,” alisema mtoa taarifa huyo.
Katika kuweka sawa mzani juu ya taarifa hiyo, Spoti Xtra limemtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa
Yanga na Mjumbe wa Kamati Tendaji klabuni hapo, Rodgers Gumbo, ambapo alisema: “Utaratibu wa kutoa bonasi
kwa wachezaji wa Yanga ni utamaduni wa kawaida na wachezaji wote wanajua ni kiwango gani wanakipata iwapo
watashinda au kutoa sare kwenye mchezo.
“Kuhusu ni muda gani mpaka malipo hayo yanaweza kukamilishwa inategemea na mchezo, kuna mechi malipo
yake huwa baada ya mechi, lakini kuna mechi ambazo malipo huchukua muda
kukamilika.
“Kuhusu taarifa kuwa kuna mchezaji anadai posho hazina ukweli wowote, ndiyo maana hata mchezo uliopita
dhidi ya KMC wachezaji wetu walionekana kuwa na ari kubwa, hili pia mtaliona kwenye mchezo wetu wa Jumamosi dhidi ya Azam.”