Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa Ligi Kuu wanavyotesa FDL

32034 Pic+mastaa TanzaniaWeb

Mon, 17 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dirisha dogo la usajili Tanzania Bara limefungwa juzi Jumamosi ambapo nyota mbalimbali wamehama kutoka timu moja kwenda nyingine.

Zipo sababu kadhaa ambazo husababisha mchezaji akahama kutoka timu moja kwenda nyingine ambapo kuna wanaohama kwa ajili ya kusaka masilahi, nafasi za kucheza lakini wengine wanakwenda kupata changamoto mpya.

Hata hivyo, upo usajili ambao umeonekana kushangaza watu hasa ule wa wachezaji kutoka timu zilizopo Ligi Kuu ambao wametua kwenye klabu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Wapo waliosajiliwa na timu hizo kwa mkataba wa mkopo, lakini pia wapo waliotua moja kwa moja ikiwa ni sehemu ya mkakati wa klabu hizo za Ligi Daraja la Kwanza kujiimarisha ili kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Mbali na hao wapo nyota ambao waliwahi kutamba kwenye Ligi Kuu hapo zamani ambao kwa sasa wanachezea timu mbalimbali za Ligi Daraja la Kwanza.

Spoti Mikiki inakuletea orodha ya nyota waliowahi kutamba kwenye Ligi Kuu ambao kwa sasa wamejazana kwenye Ligi Daraja la Kwanza na mchango wao katika timu hizo.

Arusha United

Katika harakati za kupanda Ligi Kuu msimu ujao, ‘Wana Utalii’ wa Arusha United wamefanya usajili wa kiungo Abdulhalim Humoud aliyewahi kutamba katika timu za Coastal Union, KMC, Simba, Mtibwa Sugar, Azam na Majimaji ya Songea.

Humud anakutana na mshambuliaji mkongwe aliyesajiliwa na timu hiyo akitokea Boma FC ya Mbeya ambayo aliifungia mabao matano kabla hajaihama, Gaudence Mwaikimba aliyewahi kuwika Yanga na Taifa Stars pia.

Ukiondoa wawili hao, pia kuna Zahoro Pazi ambaye hadi sasa ameifungia mabao matatu Arusha United ambayo inashika nafasi ya pili kwenye Kundi B ikiwa na pointi 14.

Ndani ya Arusha United, wachezaji wengine waliocheza Ligi Kuu ni Yusuph Mgwao, Hamad Kibopile, Julius Mrope, Jeremiah Katula, Ishala Juma na Sino Agustino.

Namungo FC

Moja ya timu znazotajwa kuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi kwenye Ligi Daraja la Kwanza msimu huu ni Namungo FC na imekuwa ikipewa nafasi kubwa ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Katika dirisha dogo la usajili imewasajili Mbaraka Yusuph na Oscar Masai kutoka Azam FC, pia imemnasa Charles Edward kutoka JKT Tanzania. Kabla ya kuwanasa hao, tayari Namungo FC inayoshika nafasi ya tatu kwenye Kundi A ilikuwa tayari inao baadhi ya wachezaji Ligi Kuu akina Reliant Lusajo, Jukumu Kibanda na Stefano Mwasika.

Mawenzi Market

Inashika nafasi ya tano kwenye Kundi A ikiwa na pointi 11 ambazo imezipata baada ya kuibuka na ushindi katika mechi tatu, kutoka sare mbili na kupoteza miwili.

Abdi Kassim aliyewahi kung’ara Yanga, Mtibwa Sugar na Taifa Stars, ndiye nyota aliyecheza Ligi Kuu ambaye yupo ndani ya kikosi hicho.

Rhino Rangers

Maafande hao wa Tabora ni miongoni mwa timu zinazopigania kupanda Ligi Kuu katika Kundi B la Ligi Daraja la Kwanza msimu huu.

Kwenye kikosi chao wana Salum Machaku aliyewahi kucheza Simba na Lipuli ya Iringa.

Reha FC

Nyota waliowahi kutamba kwenye Ligi Kuu ambao wamo katika kikosi cha Reha FC ni Ramadhani Madebe, Abbas Kapombe, Zuberi Ubwa na Ugochukwu Uzoka.

Polisi Tanzania

Maafande hao waliopo Kundi B huku wakitumia Uwanja wa Ushirika kwa ajili ya mechi zao za nyumbani, nyota waliowahi kucheza Ligi Kuu ambao wamo kwenye kikosi chao ni Bantu Admin, Nahoda Bakari na James Ambrose.

Njombe Mji

Imewabakiza baadhi ya wachezaji wake waliokuwa na timu hiyo kwenye Ligi Kuu msimu uliopita ingawa mwanzoni mwa msimu iliongeza baadhi ya nyota ili waisaidie kupanda daraja.

Baadhi ya nyota waliowahi kuonja Ligi Kuu ambao ni Emmanuel Momba, Claude Wigenge, Juma Mpakala na Laban Kambole.

Friends Rangers

‘Watoto wa Magomeni’ nao wanajivunia baadhi ya nyota waliowahi kucheza Ligi Kuu ambao wapo katika kikosi chao ambao ni Jabir Aziz, Alphonce Matogo, Fred Cosmas na Hassani Khatibu.

Geita Gold

Ni moja ya timu tishio kwenye kundi B la Ligi Daraja la Kwanza msimu huu ambako inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 13 lakini katika mafanikio hayo huwezi kubeza mchango wa nyota kadhaa waliowahi kutamba Ligi Kuu ambao ni John Mwenda na Anthony Matogolo.

Dodoma FC

Ni moja ya timu ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao ikibebwa na uongozi bora na imara ambao inayo lakini pia ina nguvu za kiuchumi za kuwawezesha kuwapa huduma sahihi wachezaji.

Ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa kundi B na pasipo shaka yoyote, mchango wa nyota kadhaa waliocheza Ligi Kuu miaka ya nyuma huwezi kuweka kando.

Wachezaji hao ni pamoja na Samuel Ngassa, James Mendy, Nassoro Masoud ‘Chollo’ na Peter Mutabuzi.

Green Warriors

Maafande hawa wamekuwa hawafanyi vizuri kwenye Ligi Daraja la Kwanza msimu huu kutokana na kuwakosa idadi kubwa ya wachezaji wenye uzoefu ambao wapo kwenye programu za mafunzo jeshini.

Mastaa waliowahi kutamba Ligi Kuu ni Hussein Bunu, George Osei, Juma Mdindi, Jafari Kissoky, Saad Kipanga, Cecil Efrem na Juma Mdindi.



Chanzo: mwananchi.co.tz