Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa 20 walioanza kuichezea Taifa Stars na umri mdogo

Mon, 3 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati wa Fainali za Kombe la Dunia nchini Russia, mshambuliaji wa Ufaransa, Kylian Mbappe (19) aliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa rekodi ya kuwa kinda aliyefunga bao kwenye mchezo wa fainali.

Mbappe aliweka rekodi hiyo, Julai 15 kwenye nyasi za uwanja wa Luzhniki kwa kuwa mchezaji wa pili mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao kwenye mchezo wa fainali dhidi Croatia ambapo Ufaransa ilishinda kwa mabao 4-2.

Pele ndiye amesalia kama mchezaji kinda zaidi aliyefunga bao akiwa na miaka 17 kwenye mchezo wa fainali ya 1958 wakati Brazil ilipoilaza Sweden kwa mabao 5-2.

Spoti Mikiki linakuletea rekodi za wachezaji ambao wameitumikia Taifa Stars kwa vipindi tofauti wakiwa na umri mdogo zaidi kuanzia mwaka 2000.

Victor Costa ‘Nyumba’ v Sudan

Beki wa kati wa zamani wa Simba, Victor Costa ‘Nyumba’ aliweka rekodi hiyo Oktoba 12, 2002 kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza pale ambapo Taifa Stars ilifungwa na Sudan mabao 2-1 katika mchezo wa kuwania mataifa ya Afrika

Costa alicheza mchezo huo ambao bao pekee la Taifa Stars lilifungwa na Mohamed Abdallah Rajab, wakati huo Costa akiwa na miaka 15 na siku 35.

Juma Liuzio v Gambia

Mshambuliaji Juma Luzio akiwa na umri wa miaka 16 na siku 287 aliingia dakika ya 61 kuchukua nafasi ya Khamis Mcha, Septemba 7, 2013 katika mchezo ambao Taifa Stars ilifungwa na Gambia kwa mabao 2-0.

Mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa BANJUL nchini Gambia ulikuwa wa kuwania nafasi ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2014 zilizofanyika Brazil.

Said Maulid v Ghana

Said Maulid ‘SMG’ akiwa na umri wa miaka 16 na siku 55, Oktoba 28, 2000 aliichezea Taifa Stars kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya tatu ya kwenye kombe la COSAFA Castle ambapo Stars iliifunga Ghana kwa mabao 3-2.

Taifa Stars ilijikuta ikimaliza pungufu kwenye mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Kasarani, Nairobi kutokana na Juma Khamis kuonyeshwa kadi nyekundu huku kwa upande wa Ghana Bilson Abeiku na Armando Adamu Baba walionyeshwa kadi nyekundu.

Juma Kaseja v Kenya

Kipa wa KMC kwa sasa, Juma Kaseja aliichezea Taifa Stars mchezo wake wa kwanza akiwa na miaka 17 na siku 223 kwenye mchezo michuano ya Cecafa dhidi ya Kenya, Novemba 30 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Taifa Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo huo lililofungwa dakika ya tisa na Henry Morris.

Ulimboka Mwakingwe v Sudan

Ulimboka Mwakingwe ambaye alikuwa akisifika kwa vyenga enzi zake alianza kuichezea Taifa Stars akiwa na miaka 18 na siku 27, Desemba 2, 2002 kwenye Kombe la Chalenji la Cecafa.

Katika mchezo huo, Taifa Stars ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Sudan na bao la Stars lilifungwa na Salvatory Edward.

Uhuru Selemani v Zambia

Winga wa Biashara United, Uhuru Selemani aliivaa jezi ya Taifa Stars kwa mara ya kwanza Novemba 21, 2007 akiwa na miaka 18 na siku 69 kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Zambia, uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Aliyeibuka shujaa kwenye mchezo huo, alikuwa Mika Chuma aliyeifungia Taifa Stars bao pekee lililoifanya timu hiyo ya taifa ya Tanzania kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Emmanuel Gabriel v Uganda

Mshambuliaji wazamani wa Simba, Emmanuel Gabriel aliichezea Taifa kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 18 na siku 154, Oktoba 23, 2002 kwenye mchezo wa nusu fainali ya kombe la Castle Lager dhidi ya Uganda.

Taifa Stars iliyosheheni nyota wengine kama Salvatory Edward, Abdallah Juma, Edibilly Lunyamila, Steven Mapunda, Selemani Matola, Meck Maxime (nahodha), Suleiman Mbaruku na Gabriel akiwemo iliambilia kipigo cha mabao 2-0.

Farid Mussa v Kenya

Winga wa CD Tenerife ya Hispania, Farid Mussa aliichezea mchezo wake wa kwanza Taifa Stars dhidi ya Kenya, Disemba 10, 2013 kwenye uwanja wa wa taifa wa Nyayo, Nairobi nchini Kenya akiwa na umri wa miaka 18 na siku 203.

Katika mchezo huo wa nusu fainali ya CECAFA, Taifa Stars ilipoteza kwa bao 1-0 alilofungwa Ivo Mapunda dakika ya tano na Clifton Miheso.

Shadrack Nsajigwa v Zanzibar

Beki kisiki wa zamani wa Yanga, Shadrack Nsajigwa aliichezea Taifa Stars kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 18 na siku 204, Septemba 2, 2002 dhidi ya Zanzibar kwenye mchezo wa kirafiki uliomalizika kwa sare bao 1-1.

Bao la Taifa Stars kwenye mchezo huo uliochezwa uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam, lilikuwa la kusawazisha dakika ya 78 kupitia kwa Athumani Machupa baada ya kutanguliwa dakika 60 kwa bao la Ame Khamis wa Zanzibar.

Amir Maftah v Zambia

Maftah alivaa jezi ya Taifa Stars kwa mara ya kwanza kwenye michezo ya kimataifa dhidi ya Zambia akiwa na miaka 18 na siku 328, Novemba 21, 2007 ambapo Stars ilishinda kwa bao la Mika Chuma.

Adam Kingwande v Mauritius

Kingwande naye aliichezea Taifa Stars kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 19 na siku tano, Septemba 6, 2008 kwenye mchezo wa kunawania kufuzu kwa kombe la Dunia dhidi ya Mauritius.

Taifa Stars iliibuka na ushindi kwenye mchezo huo kwa mabao 4-1, mabao hayo yalifungwa na Kigi Makasi, Jerson Tegete alifunga mara mbili na Nizar Khalfan.

John Kanakamfumu v Zambia

Kanakamfumu aliichezea Taifa Stars kwa mara yake ya kwanza akiwa na miaka 19 na siku 26, Novemba 21, 2007 kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Zambia.

Mrisho Ngassa v Cameroon

Winga wa Yanga, Mrisho Ngassa alianza kuichezea Taifa Stars akiwa na miaka 19 na siku 40, Juni 14, 2008 pindi ambapo Tanzania ilikuwa ikiwania nafasi ya kucheza Kombe la Dunia mbele ya Cameroon ambao ilikuwa nayo Kundi I.

Ngassa alicheza kwa mara yake ya kwanza na kushindwa kuisaidia Taifa Stars kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo uliomalizka suluhu Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mudathir Abbas v Malawi

Abbas aliichezea kwa mara ya kwanza Taifa Stars akiwa na miaka 19 na siku 157, Oktoba 2015 dhidi ya Malawi.

Mchezaji huyo kwa sasa anaitumikia Azam.

Shaaban Nditi v Zanzibar

Mkongwe Nditi aliuvaa uzi wa Taifa Stars kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 19 na siku 171, Septemba 2, 2002 kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Zanzibar.

Erasto Nyoni v Zambia

Beki wa Simba mwenye umri wa miaka 30, alianza kuichezea Taifa Stars akiwa na miaka 19 na siku 197, Novemba 21, 2007 kwenye mchezo dhidi ya Zambia.

Shiza Kichuya v Kenya

Kichuya aliichezea Taifa Stars kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 19 na siku 198, Mei 29, 2016 kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Kenya, iliyochezwa kwenye uwanja wa Kasarani.

Said Ndemla v Malawi

Kiungo wa Simba, Said Ndemla akiwa na umri wa miaka 19 na siku 213 ndipo alipoanza kuichezea Taifa Stars kwenye mchezo kuwania kufuzu kwa kombe la Dunia dhidi ya Malawi, Octoba 11, 2015 kwenye uwanja wa Kamuzu.

Jerson Tegete v Mauritius

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Jerson Tegete aliichezea Taifa Stars akiwa na miaka 19 na siku 236, Mei 31, 2008 katika mchezo dhidi ya Mauritius.

Alikuwa kipenzi cha kocha Marcio Maximo kwani alimtengeneza baada ya kuona kipaji chake.

John Bocco v New Zealand

Mshambuliaji wa zamani wa Azam, John Bocco alivaa jezi ya timu ya taifa akiwa na miaka 19 na siku 302, Januari 3, 2009 kwenye mchezo wa kirafiki ambao ulichezeshwa na mwamuzi Odan Mbaga na kumalizika kwa ushindi wa Taifa Stars kwa mabao 2-1, yaliyofungwa na Jerson Tegete dakika ya 55 na Mwinyi Kazimoto dakika ya 89.

Saimon Msuva v Gambia

Mshambuliaji wa Difaa El Jadida ya Morocco, Saimon Msuva alivaa uzi wa Taifa Stars kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 19 na siku 340, Septemba 7, 2013 dhidi ya Gambia.

Thomas Ulimwengu v Morocco

Ulimwengu naye aliichezea Taifa Stars kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 19 siku 359, Juni 8, 2013 kwenye mechi ya kuwania nafasi ya Kombe la Dunia, iliyochezwa kwenye uwanja wa Marrakech mjini Marrakech.

Ulimwendgu bado anachezea Stars na yuko Sudan kwa sasa.

Chanzo: mwananchi.co.tz