Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa 10 wenye hali ngumu Ligi Kuu

82993 Mastaa+pic Mastaa 10 wenye hali ngumu Ligi Kuu

Fri, 8 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ligi Kuu Tanzania Bara inazidi kupamba moto huku msimu ukielekea kufikia theluthi moja na ushindani wa aina yake ukionekana kuongezeka siku hadi siku kabla mashindano hayo hayajafikisha nusu ya mechi zote tofauti na misimu iliyopita.

Wapo wachezaji ambao wamekuwa wakifanya vizuri na kugeuka lulu katika timu zao kutokana na jinsi ambavyo wamekuwa wakitoa mchango mkubwa lakini wapo ambao wanaonekana kutokuwa msaada kwa klabu zilizowasajili.

Katika orodha hiyo ya mastaa ambao hawajaonyesha makeke, wapo ambao kabla ya msimu kuanza, walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kutamba na usajili wao ulitikisa lakini hadi sasa wakati ligi ikizidi kuchanja mbuga, bado hawajaonyesha makali tofauti na kile kilichotarajiwa.

Jicho la Spoti Mikiki limekuwa likifuatilia ligi kwa ukaribu na linakuletea orodha ya wachezaji 10 ambao hadi sasa hawajafanya kile ambacho wengi walitegemea wafanye kwenye klabu zao.

Francis Kahata-Simba

Kiwango bora alichokionyesha katika kikosi cha Gor Mahia ambacho kilifanya vizuri kwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Kenya na kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2018, kiliishawishi Simba kumnyakua mwanzoni mwa msimu huu ikitegemea awe chachu ya kuzalisha mabao katika kikosi chao. Hata hivyo, kiungo huyo mshambuliaji ameshindwa kuwa na mchango kwani hajajihakikishia nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza na hajafunga bao katika Ligi Kuu huku akitoa pasi moja tu iliyozaa bao.

Issa Bigirimana-Yanga

Usajili wake ulipokewa kwa shangwe na mashabiki na wanachama wa Yanga wakiamini atakuwa mkombozi wao katika kuzalisha mabao kutokea pembeni lakini mwisho wa siku matarajio yao yamekuwa kinyume.

Winga huyo aliyenaswa kutokea APR ya Rwanda, amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara lakini pia hata pale anapopata nafasi, amekuwa haonyeshi kiwango kizuri na hadi sasa hajapangwa hata katika mchezo mmoja wa Ligi Kuu.

Selemani Ndikumana-Azam FC

Aliingia kwa mguu mbaya ndani ya kikosi cha Azam FC baada ya kupata majeraha kabla hata hajaanza kuitumikia lakini licha ya sasa kuwa tayari ameshapona, nyota huyo wa Burundi ameshindwa kujihakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha klabu hiyo na kujikuta akisotea benchi akishindwa kuwapiku Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Richard Djodi na Shabani Chilunda.

Wilker Da Silva-Simba

Changamoto ya majeruhi ilimnyima nafasi ya kuonyesha makali yake katika kikosi cha Simba lakini hata baada ya kupona, kiwango alichoonyesha katika mechi chache ambazo amepata nafasi ya kucheza kimeanza kuwapa wasiwasi mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kama ataweza kuwa msaada kwao katika kufumania nyavu.

Vitalis Mayanga-KMC

Alimaliza msimu uliopita akiwa amepachika mabao 10 kwenye kikosi cha Ndanda FC huku akiwa ameonyesha kiwango bora ambacho kilishawishi idadi kubwa ya timu kuwania saini yake.

Hata hivyo mambo yanaonekana hayajamuendea vizuri ndani ya kikosi cha KMC kwani hadi sasa hajapachika hata bao moja na amejikuta hana namba ya kudumu.

Deo Kanda-Simba

Uzoefu wa kuchezea klabu kubwa ya TP Mazembe uliwapa imani Simba kuwa winga huyo atakuwa chachu kwa kikosi chao kufanya vizuri msimu huu sio tu kwenye mashindano ya ndani bali pia hata ya kimataifa.

Lakini mambo yamekuwa kinyume na mchezaji huyo wa kimataifa wa DR Congo ameonekana kuchemsha na kufunikwa na wachezaji wazawa ambao ni Hassan Dilunga na Miraji Athumani.

Maybin Kalengo-Yanga

Wakati anasajiliwa kutokea Zesco United, kundi kubwa la mashabiki wa Yanga lilikuwa na matumaini kwamba limepata mrithi sahihi wa nafasi iliyoachwa wazi na Amissi Tambwe ambaye timu hiyo ilimtema mara baada ya msimu uliopita kumalizika.

Mambo yamekuwa kinyume kwani Kalengo ameonekana kushindwa kulishawishi benchi la ufundi la Yanga kumpa nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosini na mbaya zaidi amepata majeraha ya mguu ambayo yatamuweka nje kwa muda mrefu na kubwa zaidi hadi anaumia, bado hajaifungia bao lolote Yanga katika mechi za mashindano.

Aron Kalambo-Mbeya City

Alionyesha kiwango bora msimu uliopita wakati alipokuwa akiitumikia Prisons jambo lililopelekea aingie katika rada za timu mbalimbali zikiwemo Yanga na KMC lakini mwisho wa siku akaangukia kwa Wagonga Nyundo wa jiji la Mbeya, Mbeya City.

Katika hali ya kushangaza, ,mambo yamegeuka kwa Kalambo kwani ameonyesha kiwango duni katika mechi tatu alizoichezea timu hiyo katika Ligi Kuu, ameruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.

Ibrahim Ajibu-Simba

Msimu uliopita alikuwa ni miongoni mwa wachezaji tishio katika Ligi Kuu akifunga jumla ya mabao sita na kupiga pasi 16 zilizozaa mabao akiwa katika kikosi cha Yanga ingawa baada ya hapo aliamua kurejea Simba.

Hali imekuwa kinyume ndani ya kikosi cha Simba kwani amekuwa hana nafasi katika kikosi cha kwanza na amecheza katika mechi chache akiwa anatokea benchi huku akiwa hajapachika bao na amepiga pasi moja tu iliyozaa bao.

Abalkassim Suleiman-Azam FC

Kiwango bora alichokionyesha akiwa na kikosi cha Kagera Sugar msimu uliopita ambapo alipachika mabao saba kiliishawishi Azam imsajili kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake msimu huu lakini mambo yanaonekana kuwa tofauti.

Kiungo huyo mshambuliaji ameshindwa kufurukuta na kujikuta akisotea benchi.

Chanzo: mwananchi.co.tz