KOMBE la Dunia la 2022 haliko mbali kwa sasa, na msisimko unaongezeka kadiri muda unavyokaribia licha ya kwamba si timu zote zina uhakika wa kufuzu katika michuano hiyo itakayofanyika nchini Qatar.
Hadi sasa timu za taifa 13 zimefuzu kwa Kombe la Dunia kati ya 32 zitakazoshiriki kwa ujumla. Bado haijafahamika ni mataifa gani yatachukua nafasi zilizobaki.
Ingawa mechi za mchujo bado hazijachezwa, tayari kuna baadhi ya vigogo ambao wamejihakikishia kukosa kucheza Kombe la Dunia. Hakika ni pigo kubwa kwa wachezaji na mashabiki wao.
Makala hii inaangalia wachezaji 10 wa thamani zaidi ambao tayari kuna uwezekano mkubwa wa kukosekana kwenye Kombe la Dunia Qatar, twende sasa...
#10. Sebastien Haller (Ivory Coast) – Euro Mil. 27
Mshambuliaji huyo mrefu alizaliwa na baba Mfaransa na mama raia wa Ivory Coast. Sebastien Haller aliiwakilisha Ufaransa katika maisha yake ya ujana, lakini aliamua kuichezea Ivory Coast katika ngazi ya juu.
Akiwa ameanza maisha ya soka nchini Ufaransa, alipata mafanikio yake ya kwanza aliposajiliwa na Eintracht Frankfurt ya Ujerumani. Halafu akasajiliwa West Ham United kwenye Ligi Kuu England na kujiunga na Ajax msimu uliopita wa majira ya joto. Haller amekuwa na wakati mzuri nchini Uholanzi, tayari amefunga mabao saba katika mechi 12 za ligi.
Akiwa na thamani ya Euro milioni 27, mshambuliaji huyo hataonekana kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Mabao yake yalikuwa ya kufurahisha kuyatazama kwenye hatua za kufuzu kwa Ivory Coast, lakini hayakuwa msaada kwa timu hiyo.
#9. Naby Keita (Guinea) – Euro Mil. 32
Kiungo huyo wa kati wa Liverpool hatimaye anaimarika na kuonyesha thamani yake akiwa na klabu hiyo ya Merseyside msimu huu.
Naby Keita ambaye ni raia wa Guinea tayari ana mabao mawili kwa jina lake kwenye Ligi Kuu England na anaonyesha dalili za kuimarika zaidi kuliko msimu uliopita.
Keita ana thamani ya Euro milioni 32, na ni mmoja wa wachezaji nyota wa Kiafrika ambao watakaokosa michuano ya Kombe la Dunia 2022. Guinea ilikuwa na matokeo mabaya katika raundi ya pili ya kufuzu, kwani haikushinda mchezo hata mmoja katika mechi zake sita ilizocheza.
#8. Nicolas Pepe (Ivory Coast) – Euro Mil. 35
Mengi yalitarajiwa kutoka kwa Nicolas Pepe aliposajiliwa na Arsenal. Mshambuliaji huyo alifanya vema akiwa Lille kwenye Ligi Kuu Ufaransa, Ligue 1, ambayo ilimsaidia kuhamia Ligi Kuu England.
Katika misimu yake miwili ya kwanza akiwa na 'Washikabunduki' hao, Pepe amejitahidi kudumisha kiwango.
Huku Ivory Coast ikiwa imeshindwa kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia 2022, mshambuliaji huyo mwenye thamani ya Euro milioni 35, hatacheza nchini Qatar. Pepe sasa atajikita katika kufufua kiwango chake na kuisaidia Arsenal katika mashindano yote msimu huu.
#7. Martin Odegaard (Norway) – Euro Mil. 40
Mchezaji mwingine wa Arsenal atakayekosa kushiriki Kombe la Dunia la FIFA ni kijana Martin Odegaard. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, aliutumia msimu uliopita kwa mkopo kwa 'Washikabunduki' hao kabla ya kusajiliwa moja kwa moja msimu huu.
Kiungo huyo wa zamani wa Real Madrid, anaweza kuwa mchezaji nyota katika siku zijazo.
Huku Norway ikimaliza nafasi ya tatu katika Kundi G kuwania kufuzu kutoka Mataifa ya Ulaya kuelekea Qatar, Odegaard atakosa kucheza michuano hiyo. Akiwa na thamani ya Euro milioni 40, kiungo huyo wa kati wa Arsenal anaweza kucheza Kombe la Dunia lijalo mwaka 2026.
#6. Edmond Tapsoba (Burkina Faso) – Euro Mil. 40
Si wengi wanaweza kuwa wamesikia jina la Edmond Tapsoba. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, ni beki mahiri na mkali, kwa sasa anaichezea Bayer Leverkusen kwenye Ligi Kuu Ujerumani, Bundesliga.
Kwa kasi yake, utulivu na uwezo wa kupiga pasi, mara nyingi analinganishwa na Jerome Boateng. Beki huyo mrefu wa kati amekuwa akitajwa kuwa na mafanikio makubwa na hivi karibuni anaweza kutarajiwa kuchezea klabu kubwa zaidi.
Burkina Faso walipambana vikali, lakini waliweza kumaliza nafasi ya pili katika Kundi A la raundi ya pili ya mchujo.
Akiwa na thamani ya Euro milioni 40, Tapsoba anaweza kuonekana akicheza Ligi Kuu ya England kwa siku zijazo.
#5. Wilfried Zaha (Ivory Coast) – Euro Mil. 45
Baada ya karibu kila msimu kuonekana kama Wilfried Zaha angeondoka Crystal Palace, cha kushangaza ni kwamba hakuna uhamisho wowote uliofanyika kwa nyota huyo wa Ivory Coast na amebaki kuwa nguzo muhimu kwa Eagles hao.
Kwa uwezo wake wa ajabu wa kuchezea mpira na kufunga mabao, Zaha amekuwa kama ‘masiha’ wa Crystal Palace. Alifunga mabao 11 ya Ligi Kuu England katika mechi 30 msimu uliopita na tayari amefunga mara nne katika mechi 10 za Ligi Kuu msimu huu.
Kwa bahati mbaya, Zaha hakuweza kuisaidia nchi yake kufuzu na atakosa kucheza Kombe la Dunia mwaka 2022. Akiwa na thamani ya Euro milioni 45, winga huyo sasa atakuwa na kazi moja tu ya kuisaidia Crystal Palace kwenye Ligi Kuu.
#4. Franck Kessie (Ivory Coast) – Euro Mil. 55
Franck Kessie alianza maisha yake nchini Italia pale Atalanta. Baada ya kukaa kwa mkopo kwa miaka miwili na AC Milan, kiungo huyo wa kati alisajiliwa kwa mkataba wa kudumu mwaka 2019.
Tangu wakati huo, Kessie amekuwa mchezaji muhimu kwa wababe hao wa Serie A. Kiungo huyo wa kati wa Ivory Coast anamaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu na inaonekana kama ataondoka klabuni hapo.
Kwa kuwa Ivory Coast wametupwa nje ya nafasi yao ya kucheza Kombe la Dunia la 2022, Kessie sasa anaweza kuzingatia maisha yake kwenye klabu. Akiwa na thamani ya Euro milioni 55, anatarajiwa kuchezea klabu kubwa msimu ujao.
#3. Milan Skriniar (Slovakia) – Euro Mil. 60
Kombe la Dunia la FIFA la 2022 litakosa baadhi ya walinzi bora kabisa na Milan Skriniar ni mmoja wao. Amekuwa mmoja wa mabeki bora wa kati kwenye Ligi Kuu Italia, Serie A, kwa miaka michache iliyopita.
Hapo awali aliichezea Sampdoria, ambayo ilimsaidia kuhamia Inter Milan. Skriniar ni mkabaji hodari pia ana uwezo wa kucheza kama kiungo mkabaji.
Slovakia ilishindwa kufuzu Kombe la Dunia 2022 na akiwa na thamani ya Euro milioni 60, Skriniar atakosekana katika michuano hiyo.
#2. Jan Oblak (Slovenia)
Mslovenia huyo amekuwa mmoja wa magolikipa thabiti katika ulimwengu wa soka kwa muda mrefu. Jan Oblak amekuwa nguzo muhimu zaidi kwa Atletico Madrid.
Kipa huyo wa zamani wa Benfica alitajwa kwenye orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo ya Ballon d'Or ya 2017 na 2018.
Akiwa na thamani ya Euro milioni 70, kipa huyo wa Atletico Madrid hatakuwapo kwenye Kombe la Dunia la 2022, kwani Slovenia ilishindwa kufuzu kwa hatua ya mtoano. Mchezaji wa hadhi ya Oblak anastahili kucheza katika mashindano ya kiwango cha juu kama Kombe la Dunia.
#1. Erling Haaland (Norway)
Kizazi cha vijana cha sasa cha wanasoka wenye uwezo mkubwa na Erling Haaland ni mmoja wa wachezaji kama hao, ambaye amekuwa akitawala kikatili mbele ya lango.
Kwa jina la utani 'The Terminator', Mnorway huyo ana sifa zote za kuwa mshambuliaji wa kiwango cha kimataifa. Kwa kutumia umbo lake refu na dhabiti, Haaland ni mchezaji mgumu sana kumzuia.
Haaland alikuwa na kiwango cha juu zaidi wakati akiichezea RB Salzburg akifunga mabao 17 katika mechi 16 pekee za ligi na alisajiliwa Borussia Dortmund mwaka 2019. Hadi sasa amefunga mabao 49 katika mechi 49 za Ligi Kuu Ujerumani, Bundesliga, akiwa na umri wa miaka 21.
Dalili zote zinaonyesha mustakabali mzuri sana kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Molde. Kwa bahati mbaya, Haaland atakosa kucheza Kombe la Dunia la mwakani, kwani Norway ilishindwa kufuzu, ikipungukiwa na pointi tatu tu.