Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maskini Mwakinyo! yamemkuta mapya

25011 Mwakinyo+pic TanzaniaWeb

Thu, 1 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Bondia anayechipukia vyema katika masumbwi nchini, Hassani Mwakinyo amesema ameshitushwa na taarifa za kuporomoka katika ubora wa viwango vya ngumi duniani.

Mwakinyo aliyepanda hadi namba ya 16 kwa ubora duniani katika uzito wa super welter, baada ya kumchapa Sam Eggington wa Uingereza kwa TKO raundi ya pili, ameporomoka hadi nafasi ya 17 huku Mmarekani, Jarett Hurd akiendelea kuongoza.

Katika viwango vipya vya mtandao wa ngumi wa Dunia (boxrec), Mwakinyo ameshuka kwa nafasi moja licha ya hivi karibuni kumchapa Said Yazidu kwa KO raundi ya kwanza na Joseph Sinkala kwa TKO raundi ya pili.

Nafasi ya 16 aliyokuwepo Mwakinyo inashikwa na Magomed Kurbanov raia wa Russia ambaye ana rekodi ya kushinda mapambano 16 (11 kwa KO), hajawahi kupigwa na pambano lake la mwisho alizichapa Oktoba 13 siku saba kabla ya Mwakinyo kupigana na Yazidu.

“Nimeshtushwa kuporomoka kwa nafasi moja, lakini nitajipanga upya,” alisema Mwakinyo jana alipozungumza na gazeti hili.

Alisema kushuka huko kutamsukuma kuongeza umakini ulingoni huku akijipanga kwa mapambano ya kimataifa, akiamini ataanza kufanya hivyo kuanzia Januari, mwakani.

Mwakinyo ana pointi 115, Kurbanov pointi 116 na Mtanzania huyo amezidiwa pointi 202 na Hurd ambaye ni bondia namba moja kwa ubora duniani katika uzito huo akiwa na pointi 318.

“Kinachotokea kwenye uzito wake waliokuwa chini ya Mwakinyo mmoja akicheza akashinda anapanda, lakini inategemea amecheza na bondia wa aina gani,” alisema promota wa ngumi nchini, Juma Ndambile.

Promota huyo ambaye kampuni yake ya Don Chief Promotions ndiyo iliyompeleka Mwakinyo kuzicahapa Uingereza alisema, mapambano aliyocheza mteja wake hayakuwa ya kumuongezea pointi.

“Mwakinyo ana nyota nne na nusu, amecheza na bondia wa nyota moja haimsaidii katika kupanda kwenye viwango vya ubora, isipokuwa itamuongezea rekodi ya mapambano aliyocheza na kushinda, lakini kama ingetokea Yazidu au Sinkala wangeshinda, basi wangechukua nyota zote za Mwakinyo,” alisema Ndambile.

Promota huyo alisema bondia wa kiwango kikubwa anaweza kuwania nafasi ya kuwa namba moja wa dunia, hivyo anapaswa kuwa na usimamizi mzuri katika kuandaliwa mapambano atakayocheza ambayo yanatakiwa kuwa ya kumjenga na kumpandisha kwenye viwango bora.

Chanzo: mwananchi.co.tz