Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashabiki Simba: Ruvu lazima afe Kirumba

44256 Mashabiki+pic Mashabiki Simba: Ruvu lazima afe Kirumba

Wed, 17 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

BAADHI ya mashabiki wa Simba jijini Mwanza wametamba kuwa kikosi chao lazima kishinde mbele ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa keshokutwa Novemba 19 katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Wakizungumza na Mwanaspoti mashabiki hao kutoka tawi la Isamilo jijini Mwanza kwa kujiamini wamesema Simba atashinda mabao 3-0 kama alivyofanya mara ya mwisho timu hizo zilipokutana uwanjani hapo msimu uliopita.

Salum Mtimbuka amesema timu yao haitishwi na maneno mengi huku akiwataka wanachama wenzake na mashabiki kujitokeza kwa wingi siku ya mechi kuiunga mkono na kumshuhudia kocha mpya Pablo Franco.

"Hatuna wasiwasi Simba ni timu kubwa haijawahi kutuangusha popote iendapo tuna uhakika wa pointi tatu muhimu, ushindi hapa ni muhimu liwake jua ama inyeshe mvua hatupotezi pointi kirahisi," amesema Mtimbuka.

Mwenyekiti wa tawi hilo, Amani Rashid amesema mtanange huo utakuwa na mvuto lakini timu yao ina nafasi kubwa ya kushinda kulingana na ukubwa wa kikosi walichonacho na kurejea kwa baadhi ya nyota wao waliokuwa majeruhi.

Mratibu wa Simba mkoa wa Mwanza, Nasaibu Naimocha amesema timu yao haijapotea kama ambavyo baadhi ya mashabiki wamekuwa wakisema bali yalitokea makosa madogo ambayo yamerekebishwa huku akiwahimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi kumpa sapoti kocha mpya.

"Wana Simba tuwe na subira katika kipindi hiki ambacho tunaendelea kuirekebisha timu yetu, timu iko vizuri na haijapotea kwa ushirikiano wetu tutafika pale tunapopataka na kutetea taji kwa awamu ya tano," amesema Naimocha.

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kutua jijini Mwanza saa moja jioni kwa ajili ya mchezo huo wa ligi dhidi ya wenyeji wao Ruvu Shooting utakaopigwa Ijumaa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz