Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Masau Bwire usiyemjua kwenye elimu

29013 Maswawi+pic TanzaniaWeb

Tue, 27 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mashabiki wengi wa mpira wa miguu Tanzania wanamjua kama mmoja wa watu wanaosisimua mchezo huo nje ya uwanja.

Anasifika kwa aina ya usemaji wake uliojaa misemo iliyojaa ucheshi, kebehi na kejeli. Ni mtu asiyekosa sababu na visingizo hata pale timu yake inapofanya vibaya kwa kukosa uwezo wa kiufundi uwanjani.

Huyu ni Masau Bwire, msemaji wa timu ya Ruvu Shooting inayoshirikia Ligi Kuu ya mpira wa miguu nchini.

Wengi wanaujua upande mmoja wa Bwire kama mwanamichezo na msemaji mahiri wa timu. Upande wa pili haujulikani na wengi.

Mwalimu mahiri wa Hisabati

Bwire ni mwalimu mahiri wa somo la Hisabati anayefundisha Shule ya Msingi Makumbusho iliyopo jijini Dar es Salaam.

Umahiri wake katika somo hilo umejulikana zaidi hivi karibuni baada ya kupokea barua ya pongezi kutoka ofisi za kata ya Makumbusho kufuatia matokeo mazuri ya darasa la saba yaliyotangazwa hivi karibuni.

Katika matokeo hayo, wanafunzi wake 54 walipata alama A kwenye somo la hilo, huku 52 wakipata B, 34-C na wanafunzi 11 wakipata alama D. Wanafunzi watatu walipata E, huku sifuri zikikosekana.

Anasema siri ya ufaulu huo ni tabasamu analowapa wanafunzi wake anapokuwa darasani. Kwake, upole na ukali kupita kiasi ni adui wa ufundishaji.

“Sijawahi kununa kisa nafundisha hesabu, tabasamu langu ninapowaelekeza wanafunzi wangu kuhusu somo hili ambalo linaonekana gumu kwa watu wengi limesababisha wanafunzi wangu wafaulu,” anasema.

Kiuhalisia somo la Hisabati linaogopwa na wengi kiasi hata cha kutungiwa majina kama ‘ugonjwa wa taifa’ lakini Bwire anasema wanafunzi wake hufurahia somo hilo.

Barua ya pongezi ya Bwire iliandikwa na kusainiwa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Makumbusho Simon Sylvester kama motisha ya kumtaka afanye vyema zaidi.

“Ofisi inakupongeza sana kwa ufundishaji wa bidii kubwa na mzuri wa somo la Hisabati, inakuhimiza pia uongeze juhudi ili mitihani ijayo tufanye vyema zaidi kitaifa,” inasema sehemu ya barua.

Masau Bwire wa darasani

Sifa moja ya Bwire wa kwenye michezo ni ucheshi na mazungumzo yake ya bashasha hasa anapopata nafasi ya kuzungumzia timu yake dhidi ya timu shindani. Sifa hii huibeba pia darasani kama anavyoeleza:

“Mimi ninapokuwa darasani kwanza vijana huwa wanafurahi na wanatabasamu kwa namna ambavyo naongea nao, nawashirikisha katika kufanya mifano ubaoni, kueleza kwa kina, kufafanua hatua kwa hatua, kwa mifano,” anasema.

Anasema mwanafunzi akikosea huwa anamtia moyo kwamba kukosea sio kwamba hajui.

“Huwa naelekeza kwa upendo na furaha kabisa, watoto wengi hupenda kujifunza kutokana na aina ya mwalimu,” anasema.

Kazi ya ualimu

Masau Bwire anayejiita mzalendo na mtu wa kawaida kwenye jamii alianza kufundisha mwaka 1994.

“Inawezekana hata wewe (mwandishi) ni mmoja kati ya wanafunzi wangu. Kiukweli walimu huwa hatuzeeki, tupo vilevile kwa sababu kazi yetu imebeba amani,” anasema Masau ambaye ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto 12.

Anasema tangu aanze kazi hiyo ameshafundisha shule nne tofauti ikiwamo ya Makumbusho ambayo yupo sasa.

Bwire anasema ualimu ni kazi ya maana ambayo inapaswa kupewa heshima yake, ndio maana hakuwa tayari aliposhawishiwa kuacha kazi hiyo na kujikita katika michezo.

“Nilichowaambia kwa kweli naupenda ualimu, kwa sababu nilianza nao nitaendelea kuwa mwalimu hadi pale nitakapofikia. Ukweli ni kwamba mtu akiupenda ualimu kutoka moyoni kama mimi ninavyoipenda, atakuwa na mafanikio makubwa,” anasema.

Wanafunzi na siri ya kufaulu Hisabati

Mwalimu Bwire anasema ili wanafunzi wafaulu vizuri Hisabati lazima mwalimu ajifunze namna ya kukaa na watoto.

“Unajua ukiwa mkali sana kiasi kwamba mtoto akikuona darasani anajenga hofu. Mimi wakati nipo shule ya msingi nilifundishwa na walimu tofauti, Nashukuru walinipenda pengine ni kwa sababu ya utii,” anasema na kuongeza;

“Kuna wanafunzi hawataki mwendo wa upole kwa hiyo upole na ukali vyote viwe ni kwa kiasi.’’

Anasema mtoto akijengewa msingi mbovu wa Hisabati akiwa madarasa ya awali, hatoweza kufanya vizuri kwenye somo hilo kwa sababu atalichukia.

“Hata huko mtaani jamii huwa inasema Hisabati ni somo gumu na wengi wanasema wazi hawaliwezi. Mtoto akisikia na yeye anajijenga hivyo kwamba hawezi,” anaeleza.

Ualimu na uanamichezo

Mwenyewe anasema anaweza kujigawa katika majukumu yake yote na akatekeleza wajibu wake bila kubabaika wala kuegemea upande mmoja.

“Muda wa kazi ukija shuleni utanikuta, hakuna kipindi ninachokosa kwa sababu eti mimi ni msemaji wa Ruvu Shooting. Lakini hakuna siku nimeacha kuisemea timu yangu kwa sababu mimi ni mwalimu,” anasema.

Anasema kila kitu kikipangiwa utaratibu wake hakiwezi kusumbua na kwamba, ukipenda jambo unalofanya utalifanya vizuri zaidi.

‘‘Ninapokuwa kazini wengine wanaweza kufikiri nipo mbali kumbe nyie ndio mmenifuata,” anasema.



Chanzo: mwananchi.co.tz