Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapro wapya Simba gumzo

38349 Simba+pic Mapro wapya Simba gumzo

Fri, 25 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salalam. Makocha na wachezaji wa zamani wa Tanzania wameponda viwango vya chini vilivyoonyeshwa na wachezaji wapya wa Simba, mshambuliaji Hunlede Kissimbo kutoka Togo na beki Mghana Lamine Moro katika mchezo dhidi ya AFC Leopards.

Kissimbo na Moro walitua nchini wiki hii kwa majaribio na kocha Patrick Aussems ametoa siku saba ya kupima viwango vyao.

Katika mchezo dhidi ya AFC Leopards Kissimbo aliyecheza na Okwi alionekana kushindwa kuendana na kasi.

Kissimbo alishindwa kuzitumia vizuri krosi na pasi nyingi alizopewa na Okwi wakati beki Moro aliyeanza na Pascal Wawa na baadaye Juuko Murshid, alionekana mzito na kufanya makosa kadhaa yaliyosahihishwa na wenzake.

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema kama Simba wanataka kuwasajili wachezaji hao kwa lengo la kuwasaidia katika mashindano ya kimataifa watakuwa wamekosea.

“Wachezaji wa kimataifa tunaowasajili lazima viwango vyao viwe zaidi ya wazawa. Haiwezekani ukamsajili mshambuliaji ambaye hamzidi John Bocco kwa kiwango halafu unamlipa fedha nyingi, hayo yanakuwa matumizi mabaya ya fedha,”alisema Pawasa.

Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula alisema anashangazwa kuona wachezaji wanatoka nje, lakini wanazidiwa viwango na wazawa.

“Inatakiwa Simba inayoshiriki mashindano ya kimataifa kusajili wachezaji kutoka nje kuja kucheza siyo watu wa majaribio.

“Nafikiri hao wachezaji warudi tu kwao wakapumzike na kama Simba inataka kweli kusajili mchezaji wa maana walete aina ya Jean Makusu wa AS Vita ya Congo,” alisema Mwaisabula.

Kocha wa Prisons ya Mbeya, Mohammed ‘Adolph’ Rishard, alisema Kissimbo na Moro ni wa kawaida na atashangaa kama watasajiliwa na Simba.

Rishard aliyekuwepo uwanjani katika mchezo huo, alisema wachezaji hao walionyesha kiwango cha kawaida na wala usingedhani kama wa kimataifa.

“Sijui kama wamewasajili au ndio wako katika majaribio, lakini hawana kiwango cha kucheza Simba ni wa kawaida sana.

“Hata ukipita katika timu zetu za hapa nyumbani zinazoshiriki ligi mbalimbali unaweza kupata wachezaji wenye viwango bora kuliko hao wa Simba,” alisema Rishard.

Kauli ya Aussems

Kocha Aussems alisema anahitaji muda wa kuwaangalia wachezaji hao na atawapa mechi nyingine kabla ya kufanya uamuzi. “Bado nahitaji muda zaidi wa kuwaangalia katika mechi nyingine ili kuona kama wanastahili kusajiliwa katika kikosi cha Simba,” alisema Aussems. Simba juzi ilimleta mshambuliaji mwingine raia wa Namibia, Sadney Urikhob kwa majaribio.



Chanzo: mwananchi.co.tz