Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manyika, Pawasa wapigilia msumari Ninja kufungiwa

46254 Pic+ninja Manyika, Pawasa wapigilia msumari Ninja kufungiwa

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya wachezaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Bennedict Tinocco na Juma Nyangi kufungiwa, baadhi ya wadau wa soka wametoa maoni tofauti kuhusu adhabu hizo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wakili Kiomoni Kibamba alisema wachezaji hao wamefungiwa kwa utovu wa nidhamu.

Shaibu anayecheza (Yanga), Tinoco (Mtibwa Sugar) na Nyangi wamefungiwa mechi tatu kila mmoja baada ya kupatikana na hatia. Pia kamati hiyo imezipiga faini Simba, Yanga na Azam kwa makosa tofauti.

Mwananchi lilimtafuta kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Manyika Peter ambaye alisema TFF inapaswa kutoa adhabu kali kwa wachezaji watovu wa nidhamu.

“TFF itoe adhabu kali zaidi zitakazomfanya mchezaji mwingine aogope na iwe hata kwa timu ndogo na uzuri siku hizi mechi zinaonyeshwa.

Mechi zinaonyeshwa na televisheni mchezaji anapoonyesha utovu wa nidhamu ni hatari kwa maendeleo ya soka,” alisema Manyika.

Kocha wa timu ya Taifa ya Ufukweni, Boniface Pawasa alisema adhabu walizopewa wachezaji hao ni ndogo kulingana na makosa waliyotenda.

Pawasa, mmoja wa mabeki hodari wa zamani wa Simba na Taifa Stars, alisema itungwe kanuni ambayo itagusa adhabu ya mchezaji kukatwa mshahahara na fedha kupelekwa TFF endapo ataonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu.

Shaibu anadaiwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Coastal Union Andrew Shenchimba katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Februari 3.

Tinoco aliingia matatani kwa madai ya kumkanya makusudi mchezaji wa Biashara United katika mchezo uliochezwa Februari 14.

Kwa upande wake Nyangi alionekana katika picha za mkanda wa video akimdhalilishaji beki wa Yanga, Gadiel Michael katika mechi ya Machi 2.

Wakati huo huo, Yanga imetozwa faini Sh8 milioni, Simba Sh3 milioni na Azam FC Sh3 milioni kwa makosa mbalimbali waliyofanya kwenye Ligi Kuu Bara.



Chanzo: mwananchi.co.tz