Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manula aiweka Simba mtegoni

Aishi Manula aiweka Simba mtegoni

Fri, 2 Apr 2021 Chanzo: ippmedia.com

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam hivi karibuni zinasema vigogo hao wa Sudan wanadaiwa kutenga kiasi cha zaidi ya Sh. milioni 200 ili kumsajili golikipa huyo ambaye ni mlinda mlango namba moja wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars).

Inadaiwa pia Al Merreikh imemwandalia Manula mshahara mara tatu ya kile anacholipwa na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na gazeti hili jana, Manula alisema yeye bado ni mchezaji mwenye mkataba na Simba, hivyo atasikiliza na kufuata uamuzi utakaofanywa na klabu yake hiyo ambayo kwa sasa imeweka mguu mmoja ndani kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Manula alisema mpaka sasa klabu tano zinazoshiriki ligi mbalimbali zimeonyesha nia ya kuhitaji huduma yake, lakini hawezi kuziweka wazi kwa sababu yuko ndani ya mkataba na Simba.

"Kwa sasa ninawasikiliza waajiri wangu ambao ni Simba, kuhusu suala zima la ofa hiyo kwenda au kuendelea kusaidia timu katika Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika," alisema Manula ambaye alitua Simba akitokea Azam FC.

Golikipa huyo alisema masharti ya mkataba wake na Simba yanambana hivyo hawezi kusema chochote kuhusiana na ofa hizo, lakini anaamini waajiri wake watafanya uamuzi kwa kuangalia maslahi kwa pande zote mbili.

"Simba wao ndio wenye nafasi ya kufanya uamuzi wa kuniuza au kunibakiza kwa kuendelea kuitumikia klabu yao, kwangu ni bora kwa sababu nina imani ya kuwa bora zaidi, watakapochukuwa uamuzi wa kuniuza pia itakuwa jambo nzuri kutokana na kupata maslahi kwao na kwangu pia," alisema Manula.

Kuhusu kiwango bora ambacho amekionyesha katika siku za hivi karibuni alisema hizo ni juhudi zake binafsi, mafundisho kutoka kwa kocha wao mpya wa magolikipa Mbrazili Milton Nienov pamoja na ubora wa sasa kikosi hicho cha Simba.

"Simba kwa sasa ni timu bora pia ujio wa kocha Milton umechangia kwa kiasi kikubwa kuwa katika bora, pamoja na makipa wenzangu kwa sababu ukiangalia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika sisi tuna 'clean sheet nne', tatu zangu na moja ya Beno Kakolanya," Manula alisema.

Manula ambaye msimu uliopita alitangazwa kuwa Kipa Bora ameiongoza Simba kufikisha pointi 10 na kuwa kinara wa Kundi A katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo walishinda bao 1-0 ugenini dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) halafu wakapata ushindi kama huo walipowakaribisha vigogo wa Afrika, Al Ahly kutoka Misri.

Hata hivyo Manula hakusimama langoni wakati Simba ikicheza dhidi ya Al Merreikh jijini Khartoum kwa sababu ya kuwa mgonjwa na mchezo ulimalizika kwa sare ya bila kufungana lakini aliporejea tena langoni timu yake iliibuka na ushindi mnono wa magoli 3-0 dhidi ya mabingwa hao wa Sudan.

Wakati huo huo, kikosi cha AS Vita kikiwa na wachezaji 24 na viongozi tisa kiliwasili nchini jana usiku tayari kwa mchezo wa raundi ya tano utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.

Katika hatua nyingine, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu aliliambia gazeti hili wachezaji, Meddie Kagere na Luis Miquissone walitarajiwa kurejea nchini jana kuungana na wenzao kwa ajili ya mchezo huo ambao mashabiki 10,000 wameruhusiwa kushuhudia mtanange huo.

Chanzo: ippmedia.com