Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manula aacha rekodi AFCON

65552 Manula+poic

Fri, 5 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kipa wa Taifa Stars, Aishi Manula ni miongoni mwa makipa watatu waliofanya vizuri kwenye hatua ya makundi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoendelea Misri, baada ya kushika nafasi ya pili kwa kuokoa idadi kubwa ya mashambulizi kutoka kwa timu pinzani.

Manula (23) ameokoa mashambulizi 14 katika mechi mbili dhidi ya Senegal ambayo timu hiyo ilifungwa mabao 2-0 na Kenya iliyolala kwa kuchapwa mabao 3-2.

Katika orodha hiyo, kipa wa Namibia, Llyod Kazapua ndiye kinara baada ya kuokoa mashambulizi 15 katika mechi tatu alizocheza dhidi ya Tunisia, Afrika Kusini na Ivory Coast.

Kwa tathmini ya kawaida, Manula ndio kama kinara kwani ana wastani wa kuokoa mashambulizi saba (7) kwa kila mchezo wakati Kazapua yeye ana wastani wa kuokoa mashambulizi matano (5).

Pengine Manula angeweza kumaliza kama kipa kinara wa kuokoa idadi kubwa ya mashambulizi laiti angecheza mechi ya mwisho dhidi ya Algeria ambayo Taifa Stars ilicharazwa mabao 3-0, lakini aliwekwa benchi na nafasi yake kuchukuliwa na Metacha Mnata ambaye naye aliweka rekodi ya kuidakia timu hiyo kwa mara ya kwanza.

Kipa Patrick Matasi wa Kenya amemaliza akiwa nafasi ya tatu kwa kuokoa idadi kubwa ya mashambulizi katika fainali hizo akiwa amefanya hivyo mara 12 na nafasi ya nne inashikwa na Mohamed El-Shenawy wa Misri ambaye ameokoa michomo 10.

Pia Soma

Katika nafasi ya tano yupo Daniel Akpeyi wa Nigeria ambaye ameokoa mashambulizi tisa sawa na Jonas Mendes wa Guinea Bissau huku Edmore Sibanda (Zimbabwe), Brahim Souleymane (Mauritania) na Ley Matampi (DR Congo) ambao kila mmoja ameokoa michomo minane.

Nyuma ya makipa hao yupo kipa wa KMC ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Jonathan Nahimana aliyedakia Burundi ambaye ameokoa mashambulizi saba akisimama imara katika milingoti mitatu. Fainali hizo zimeingia hatua ya 16 bora.

Chanzo: mwananchi.co.tz