Arusha. Achana na ushindi wa kwanza iliyopata Yanga dhidi ya USM Alger ikiwa ni rekodi yao tangu alipoondoka Kocha George Lwandamina katika mashindano ya CAF, lakini furaha zaidi imekuja baada ya Wanayanga kumuona Yusuf Manji uwanjani.
Mwenyekiti huyo wa Yanga aliyejiuzulu Mei 20 mwaka jana kutokana na matatizo kadhaa yaliyomkabili, alihudhuria mchezo huo wa tano wa Kundi D wa Yanga katika Kombe la Shirikisho Afrika na vijana kushinda mabao 2-1.
Ushindi huo na ujio wa Manji umewafanya Wanayanga wa jijini hapa kuhamasishana kuichangia timu yao ili mambo mazuri yaendelee hata katika Ligi Kuu Bara inayoanza keshokutwa Jumatano.
Katibu wa Matawi ya Yanga Mkoa wa Arusha, Destrich Kateule alisema kuwa ujio wa Manji uwanjani umetafsiriwa na wadau wa klabu hiyo kuwa ndio iliyowapa hamasa nyota wa Yanga kucheza na timu kushinda mechi ya kwanza ya makundi.
Hata hivyo, alisema matokeo hayo kutokuwa na faida kwa timu yao kwani imeshandolewa kwenye mbio za kutinga robo fainali, ila imeongeza chachu ya kuona wana uwezo wa kulirejesha taji lao la Ligi Kuu kutoka mikononi mwa Simba.
“Ujio wa Manji tu uwanjani ni hamasa tosha kwetu hata kama hajasema chochote lakini tunaamini anacho kitu kikubwa atakachofanya kwa Yanga hivyo kwa kuanzia sisi kama wanachama tumeanza tangu jana kuhamasishana kuichangia timu yetu,” alisema Kateule.
Katibu huyo alisema timu yao iko vizuri hasa wakicheza kwa hamasa ila kikubwa kinachowakwamisha ni uchumi kuyumba, hivyo kwa sasa baada ya kumuona Mwenyekiti wao yuko pamoja nao, wanaanza nguvu mpya ya kuchangia timu huku wakiwahamasisha mashabiki ambao bado si wanachama kufanya hivyo.
“Kwa Arusha tu pekee tuna wanachama zaidi ya 200 kila mmoja tulihamasisha achangie kuanzia 5000 hadi 10,000 kupitia mitandao ya simu tunaamini zitikana fedha za kutosha za kuwati nguvu nyota wetu ili katika ligi watishe," alisema.
Alisema pia wanahamasisha mashabiki wengine kuingia uanachama na kuwa na moyo wa dhati ya kuisaidia klabu yao kwa hali na mali.
Alisema kama wanachama wanaamini zimebaki siku chache kama sio saa kabla ya Manji kurejea Yanga hivyo wanafanya juhudi za kuweka mazingira sawa akirudi aikute klabu inaendelea na uchumi ili kuepuka kumbebesha mzigo mkubwa.