Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manji atikisa Mkutano Mkuu wa Yanga kesho

8915 Manji+pic TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati ajenda za mkutano mkuu wa Yanga, utakaofanyika kesho Jumapili jijini zikiwa hazijawekwa hadharani, mijadala kuhusu mwenyekiti wa klabu hiyo Yusuf Manji imeanza kuonyesha dalili za wazi kuteka mkutano huo.

Manji anaonekana kugusa hisia za wanachama wa Yanga ambao huenda wakatumia sehemu kubwa ya mkutano huo kumshawishi atengue uamuzi wake wa kujiuzulu sambamba na kufanya uwekezaji ndani ya klabu hiyo kupitia mabadiliko ya uwekezaji ambayo wamepanga kuyafanya.

Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa alisema wanachama wao walishafikishiwa ajenda tangu siku 30 zilizopita hivyo hawawezi kuziweka hadharani kwa kipindi hiki.

“Wanachama waliangalia wenyewe ajenda zinazofaa na kuongeza nyingine hivyo hatuwezi kuzitaja hadharani ajenda hizo ambazo wanachama watazijadili kwenye mkutano,” alisema Mkwasa.

Tangu alipojiuzulu nafasi ya uenyekiti wa Yanga, Mei 22 mwaka jana, uongozi, wajumbe wa Bodi ya Udhamini na wadau mbalimbali wakubwa wa klabu hiyo wamekuwa wakionyesha juhudi kubwa kumshawishi Mfanyabiashara huyo kurejea kwenye nafasi yake kutokana mchango mkubwa ambao amekuwa akitoa katika kuisaidia Yanga.

Miongoni mwa juhudi na hatua ambazo Yanga wamezichukua kumshawishi Manji ni kukataa barua yake hiyo ya kujiuzulu ambayo aliiandika mwaka mmoja uliopita jambo ambalo kwa mujibu wa ufafanuzi wa kikatiba kutoka kwa Mwenyekiti wa Matawi ya Yanga jijini Dar es Salaam, Kais Edwin.

“Kikubwa cha kwanza ambacho ninaweza kukisema ni kuwa mimi na wanachama wote halali wa Yanga tunatambua bado Manji ni mwenyekiti wa klabu yetu na sio vinginevyo.

Baada ya ndugu Yusuf Manji kutangaza kujiuzulu, sisi viongozi wa matawi tulipinga barua yake na tulimpa nafasi tu ya kumpumzika jambo ambalo tunashukuru hata Kamati ya Utendaji ilituunga mkono kwa sababu Katiba ya Yanga ina kipengele ambacho kinawapa haki wanachama kupinga kujiuzulu kwake.

Hakuna mkutano wowote ambao ulifanyika kujadili kujiuzulu kwake hivyo bado kikatiba yeye ni mwenyekiti na ana haki za msingi kuhudhuria na ikibidi hata kuuongoza mkutano,” alisema Kais.

Huku ikidaiwa Bodi ya Wadhamini wa Yanga pamoja na uongozi wa timu hiyo umefanikiwa kumshawishi Manji kushiriki kwenye mkutano huo, dalili za jina huenda likazima ajenda nyingine kujadiliwa na badala yake suala la kumshawishi Manji kutengua kujiuzulu kwake pamoja na kufanya uwekezaji ndani ya klabu hiyo ndilo linaonekana kushika hatamu.

Chanzo: mwananchi.co.tz