Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manji afunguka,Yanga full mzuka

13436 Manji+pic TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

UNAAMBIWA kazi imeanza Jangwani. Yanga jioni ya leo inatarajiwa kushuka Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kuikaribisha Mtibwa Sugar katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, huku Mwenyekiti wake, Yusuf Manji akituma salamu.

Bosi huyo aliyerudisha ule mzuka Jangwani mpaka Mwarabu kupigwa katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ameanza mambo akituma salamu maalumu jeshini pamoja na kwa klabu yake kwa kazi nzuri waliyofanya wikiendi iliyopita.

Manji alianza kwa kumtumia salamu hizo Mkuu wa Majeshi nchini, Jenerali Venance Mabeyo akimshukuru kwa kufika kwake katika mchezo huo wa CAF ambao Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya USM Alger ya Algeria.

Jenerali Mabeyo ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika mchezo huo ambao vijana wa Yanga walipiga mpira mwingi tofauti na ilivyokuwa katika mechi zao nne za awali walizopoteza tatu na kutoka suluhu mchezo mmoja dhidi ya Rayon Sports.

Mwanaspoti limeshuhudia barua maalumu ya Manji akimshukuru Jenerali Mabeyo kwa maneno yake kabla ya mchezo huo kwa wachezaji wa timu hiyo akisema yalikuwa kichocheo kikubwa kwa Yanga kupata ushindi huo.

Mbali na salamu hizo za Mabeyo, Manji pia ameandika barua maalumu kwa ofisi ya Katibu Mkuu wa Yanga akimshukuru kwa kusimamia mchezo huo pamoja na kuwapongeza wachezaji wa timu hiyo na wanachama wake na mashabiki wa timu hiyo.

Alisema wanachama wa Yanga walimpokea vyema na kuishangilia kwa nguvu na kuipa heshima nchi na serikali yao kwa ushindi huo na amewataka pia kufika kwa wingi uwanjani kuipa nguvu timu yao inayoanza ligi leo.

Aliwapongeza pia viongozi wa klabu hiyo kwa kusimamia vyema usajili na kutengeneza timu nzuri ambayo anaamini sasa inaweza kupambana kurudisha mataji yaliyopotea msimu uliopita.

DUA NZITO JANGWANI

Katika hatua nyingine, jana pale Jangwani kuhakikisha Yanga inaanza safi ligi uongozi wa timu hiyo walifanya dua maalumu kwa timu yao pamoja na wanachama wao.

Dua hiyo ilifanyika makao makuu ya Yanga na kuhudhuriwa na wachezaji, viongozi, wanachama na mashabiki wao ikiwa ni utamaduni wa klabu hiyo kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

MAKAMBO AMBIPU OKWI

Straika mpya wa Yanga Heritier Makambo amesikia taarifa za kutajwa kuwania tuzo ya Mfungaji Bora ambayo msimu uliopita ilibebwa na Emmanuel Okwi wa Simba kisha akasema hilo sio tatizo kwake, lakini akatamka kila anapofunga anasahau hapohapo na kuangalia mbele zaidi.

Akizungumza na Mwanaspoti Makambo alisema anaweza kuwa mshindani mzuri kuwania kiatu cha dhahabu cha Mfungaji Bora, lakini utaratibu wake ni atakuwa anafunga kuhakikisha kwanza Yanga inakuwa bingwa.

Makambo raia wa DR Congo alisema kila atakapokuwa anamaliza mechi moja na kufunga hataki kuweka akili ya mabao hayo kichwani kwake ambapo anataka kusahau ili atafute mabao zaidi.

Alisema mbali na kuwa straika wa kwanza pia atakuwa akiwatengenezea nafasi wenzake ikitokea amebanwa na mabeki, lengo likiwa ni kuitanguliza timu yake na sio mafanikio binafsi.

“Kila mshambuliaji angependa kuwa mfungaji bora, ila sitaki kuweka sana akili ya kuwa mfungaji bora nataja kwanza timu yangu ifanikiwe. Tunacheza kama timu sio lazima nifunge, ikitokea nimekabwa sana nitawatengenezea wenzangu.”

 

Chanzo: mwananchi.co.tz