Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Man United ya Solskjaer mishahara namba moja, uwanjani hovyo kabisa

Sosha Pic Data Man United ya Solskjaer mishahara namba moja, uwanjani hovyo kabisa

Wed, 10 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

LONDON, ENGLAND. USHAAMBIWA, pesa hainunui mapenzi. Cheki, Chelsea ya Thomas Tuchel ipo matawi ya juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, lakini wala haitumii pesa nyingi kwenye kulipa mishahara mastaa wake.

Lakini, taji la timu inayolipa pesa nyingi mastaa wake kwa mujibu wa Spotrac - linakwenda kwa Ole Gunnar Solskjaer na kikosi chake cha Manchester United, ambayo ina mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi kwenye ligi, Cristiano Ronaldo.

Sasa njoo uwatafute kwenye msimamo wa ligi sasa, hata kwenye tano bora hawapo licha ya kulipa mishahara mikubwaaa.

Cheki hapa bili ya mishahara kwa kila timu kwenye Ligi Kuu England na huu ndio msimamo utakavyokuwa ikizingatiwa mishahara inayolipwa.

20. Brentford

Brentford ndiyo timu yenye bili ndogo zaidi ya mishahara kwenye Ligi Kuu England, ikilipa Pauni 12.8 milioni tu kwa mwaka. Karibu nusu ya bili hiyo, Pauni 6.1 milioni inatumika kwenye idara ya kiungo, yenye mastaa kama Sergi Canos na Christian Norgaard huku washambuliaji wakitumia Pauni 1.4 milioni kwenye mgawanyo huo wa mishahara.

19. Leeds

Kikosi cha Marcelo Bielsa ni moja ya timu inayocheza soka la kuburudisha kwenye EPL, lakini mishahara yao kwa mwaka ni Pauni 17.9 milioni tu. Leeds inatumia Pauni 9.8 milioni kulipa safu ya ushambuliaji mishahara, inayoundwa na Patrick Bamdford, Raphinha na Rodrigo. Viungo wanalipwa Pauni 2.4M akiwamo fundi, Kalvin Phillips.

18. Norwich City

Licha ya Norwich City imekuwa na hali mbaya kwenye ligi msimu huu, lakini inalipa mishahara mastaa wake, Pauni 24.2 milioni kwa mwaka. Pauni 10.8 milioni inatumika kwa mabeki, ambao wamekuwa waliruhusu tu mabao, huku makosa makubwa waliyofanya kulipa fowadi yao mshahara wa Pauni 1.9 milioni kwa mwaka na ndio maana hawafungi mabao ya kutosha.

17. Watford

Linapokuja suala la timu zilizopanda daraja msimu huu, yenyewe inalipa mshahara wa Pauni 30.1 milioni. Sehemu kubwa ya bili yao ya mishahara inatumika kwa wachezaji wa viungo, Pauni 11.4 milioni na beki Pauni 10.6 milioni. Safu yao ya ushambuliaji, Watford inatumia Pauni 5.5 milioni kuwalipa mastaa wake kama Joshua King, Joao Pedro na Ismaila Sarr.

16. Burnley

Chama la kocha Sean Dyche kwa sasa linatumia Pauni 33.8 milioni kwenye mishahara ya wachezaji na mgawo umekuwa vizuri, ambapo makipa wanalipwa Pauni 2.1 milioni, mabeki Pauni 13 milioni na mastraika wanalipwa Pauni 9.9 milioni. Dirisha lililopita, Clarets ilifanya usajili mkubwa wa mastaa Nathan Collins, Maxwel Cornet na Connor Roberts.

15. Brighton

Brighton wapo kwenye ubora wao msimu huu huku bili yao ya mishahara ikiwa Pauni 37.2 milioni kwa mwaka. Kocha Graham Potter amewaweka kwenye kiwango bora kabisa, huku zaidi ya Pauni 11 milioni ikitumika kwenye mastraika na mabeki, wakati uwekezaji mkubwa upo kwenye sehemu ya kiungo, ambapo eneo hilo inalipa mishahara Pauni 13.2 milioni kwa mwaka.

14. Southampton

Southampton inatumia Pauni 43.8 milioni kwa mwaka kwenye kulipa mishahara mastaa wake, huku Pauni 18.3 milioni ikitumika kulipa mastraika - akiwamo Adam Armstrong na Che Adams. Pauni 12 milioni na zaidi inatumika kulipa wachezaji wa idara ya kiungo, huku wakizidi kwa Pauni 7.3 milioni mishahara ya Brighton, Burnley, Leeds na Brentford kwa pamoja.

13. Wolves

Wolves yenyewe imewekeza Pauni 45.3 milioni kwenye malipo ya wachezaji wake kwa mwaka, huku Pauni 14.3 milioni ikitumika kuwalipa mastaa wao kwenye safu ya ushambuliaji. Viungo wa Wolves wanalipwa mshahara wa Pauni 13.6 milioni tu, licha ya kuwa na mafundi wa uhakika kwenye soka kama Wareno wawili, Ruben Neves na Joao Moutinho.

12. Newcastle United

Hali ya mambo kwenye ligi si mazuri kabisa, lakini Newcastle United ni moja ya timu yenye bili kubwa ya mishahara yake kwa mwaka, ikilipa Pauni 46.9 milioni. Wanatumia pesa nyingi kwenye beki, ambayo ni mbovu kwelikweli, Pauni 19.4 milioni. Na sasa baada ya kuwa chini ya matajiri wa Kiarabu, bili yao ya mishahara inaweza kuwa kubwa zaidi mwakani.

11. Aston Villa

Licha ya kurejea kwenye ligi kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita, Aston Villa wao bili yao ya mishahara kwa wachezaji kwa mwaka ni Pauni 51.7 milioni. Sehemu kubwa ya bili yao hiyo inakwenda kwenye safu ya ushambuliaji, ikiwalipa Ollie Watkins, Bertrand Traore, Danny Ings na Leon Bailey, huku wakifurahia kumuuza Jack Grealish Pauni 100 milioni.

10. Crystal Palace

Vijana wa London Kusini, Crystal Palace wao bili yao ya mishahara ni kubwa kuliko Aston Villa, wakilipa Pauni 51.8 milioni kwa mwaka. Makipa wa Palace wanalipwa Pauni 6.3 milioni, huku safu yao ya ushambuliaji ikitumia zaidi ya Pauni 17 milioni, kuwalipa mastaa wake kama Christian Benteke, Wilfried Zaha na wengine kwenye ushambuliaji.

9. Leicester City

The Foxes kwa sasa wanatumia Pauni 54.5 milioni kwenye kulipa mishahara na haishangazi kuona wamemaliza kwenye Top Five kwa misimu miwili mfululizo. Pauni 7.8 milioni inatumika kuwalipa makipa, wakati Pauni 16.5 milioni ni mishahara wa idara ya mabeki na kwenye viungo inatumia Pauni 17.5 milioni.

8. West Ham

West Ham United kwa sasa inapambana kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kuongeza bili yao ya mishahara na kufikia Pauni 59.6 milioni. Mabeki ndio wanakula pesa nyingi, Pauni 25 milioni, huku fowadi yao yenye wakali kama Jarrod Bowen, Michail Antonio na Andriy Yarmolenko inalipwa Pauni 15.8 milioni kwa mwaka.

7. Everton

Kocha Rafa Benitez hakuwa na pesa nyingi za kusajili, lakini Everton inatumia Pauni 70.9 milioni kwenye kulipa mishahara ya wachezaji wake kila mwaka. Sehemu kubwa ya bili ya mishahara yao inakwenda kwenye idara ya kiungo, wakilipa Pauni 27.4 milioni, wakati Brentford huo ni mshahara wa kikosi chao kizima cha wachezaji 28. Fowadi wanalipwa Pauni 11 milioni.

6. Tottenham

Tottenham inaweza kuwa na uwanja wenye thamani kubwa England, lakini inalipa mastaa wake Pauni 78.7 milioni tu kwa mwaka. Kwenye mkwanja huo, Pauni 27 milioni wanalipwa washambuliaji ikiwamo Harry Kane na Son Heung-min, huku viungo wakitumia Pauni 30.9 milioni kwenye sehemu hiyo ya bili ya mishahara ya klabu hiyo.

5. Arsenal

Arsenal inatumia pesa nyingi kwenye kulipa mishahara mastaa wake kuliko mahasimu wao Tottenham, wanalipa Pauni 99.8 milioni. Sehemu kubwa ya mshahara wa Arsenal unakwenda kwenye idara yao ya ushambuliaji, Pauni 38.3 milioni zinatumika kuwalipa Pierre Emerick Aubameyang, Nicolas Pepe na Alexandre Lacazette. Wanatumia Pauni 34.2 milioni kwa mabeki.

4. Liverpool

Mabingwa wa England 2019-20, Liverpool kwa sasa wao bili yao ya mishahara kwa mwaka ni Pauni 139.2 milioni, huku chama hilo la Jurgen Klopp likitumia Pauni 36.7 milioni kuwalipa mastraika, wakiwamo Mohamed Salah na Sadio Mane. Liverpool inazizidi Burnley, Watford, Norwich, Leeds na Brentford kwa mishahara yao ya pamoja.

3. Man City

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, wao wanatumia Pauni 143.2 milioni kwenye mishahara ya wachezaji. Na utashangaa, Pauni 22.7 milioni tu inatumika kwa mastraika, huku kwenye kiungo ndio panapotumia pesa nyingi ya mishahara ya Manchester City, ambazo ni Pauni 73.5 milioni.

2. Chelsea

Chama la Thomas Tuchel, Chelsea linashika usukani wa ligi, lakini bili yao ya mishahara kwa wachezaji ni Pauni 162.6 milioni. Chelsea, inatumia Pauni 51.5 milioni kulipa mastraika, Pauni 59.6 milioni kulipa mishahara viungo wake na Pauni 40.7 milioni inatumika kwenye mishahara ya mabeki.

1. Man United

Ndo hivyo. Linapokuja suala la mishahara ya wachezaji, Man United inatumia Pauni 226.7 milioni kwa mwaka. Katiba lugha nyepesi, Man United inalipa mishahara mikubwa kuliko hata mishahara ya Brentford, Leeds, Norwich, Watford, Burnley, Brighton na Southampton kwa pamoja.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz