Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo yanoga riadha, wanne wapenya kushiriki Olimpiki

Alphonce Simbu Mambo yanoga riadha, wanne wapenya kushiriki Olimpiki

Tue, 26 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Tanzania inaweza kuanza kutamba, licha ya kwamba ni kwa idadi ndogo ya wanamichezo waliojihakikisha kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki sasa, ambao ni wanne.

Kwa hao wanne ni uhakika, kwani wametajwa kufikia viwango vya kuiwakilisha nchi kwenye mashindano hayo yanayoanza Julai, 2024 nchini Ufaransa.

Mbali na hao, wanariadha wengine wanane mwakani watachuana kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa kusaka viwango hivyo.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Riadha la Dunia (WA), siku ya mwisho kufuzu ni Aprili 30 kwa mbio ya marathoni na Juni 30 kwenye mbio za uwanja, miruko na mitupo tayari kwa Olimpiki itakayoanza mwishoni mwa Julai.

Alphonce Simbu ndiye alikuwa mwanariadha wa kwanza nchini kufuzu, kabla ya Magdalena Shauri.

Hivi karibuni, Gabriel Geay na Jackline Sakilu wamefikia viwango baada ya kukimbia ndani ya muda wa kufuzu kwenye mbio za China na Valencia.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Jackson Ndaweka amesema Sakilu alikimbia kwa saa 2:26:50 huko China ambao ni muda uliowekwa na WA kufuzu au chini ya hapo kwa wanariadha wa marathoni wanawake.

Kwa wanaume muda ni saa 2:08:10 au chini ya muda huo ambao tangu pazia la kufuzu lifunguliwe mwaka huu, Simbu na Geay pekee ndio wamekimbia muda huo na Magdalena kwa wanawake.

Kwa mujibu wa Ndaweka, Failuna Abdi, Sarah Ramadhan, Faraja Lazaro na Emmanuel Giniki pia wanatazamiwa kushiriki mbio za kutafuta viwango hivyo mwakani kwa marathoni.

“Pia tunakwenda kutafuta viwango kwenye michezo ya uwanjani, kuna mashindano makubwa mwakani ya Afrika nchini Cameroon na Michezo ya Afrika kule Ghana. Haya yote yanatoa viwango vya Olimpiki," amesema Ndaweka.

“Wanariadha wetu wengine Transfora Musa (mita 10,000) Elizabeth Iranda (mita 5000), John Nahhai (mita 1500) na Andrew Rhobi (mita 800 na 1500) watashiriki kwa ajili ya kutafuta viwango vya Olimpiki.”

Bosi huyo wa RT amesema kuwa wanariadha wote kwa pamoja wataanza kambi mwanzoni mwa Februari kujiandaa mashindano ya kufuzu na waliofuzu kujiweka fiti kwa ajili ya Olimpiki.

Mbali na riadha, ngumi, judo, kuogelea na soka la wanawake wanashiriki mashindano ya kusaka viwango hivyo. Timu ya Twiga Stars inashiriki mashindano ya kufuzu, muogeleaji Hilal Hilal, judoka Andrew Thomas na bondia Yusuph Changalawe wanaendelea na mazoezi kutafuta viwango.

Chanzo: Mwanaspoti