Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo sita yaliyoipa Simba ubingwa Ligi Kuu

61236 Simba+%255Bpic

Tue, 4 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Si jambo la ajabu Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya kufikisha pointi 93.

Tangu nusu ya msimu wa ligi Simba ilionyesha dalili zote za kutetea taji lao kama ilivyofanya msimu uliopita na hilo lilichangiwa na sababu mbalimbali za ndani na nje ya uwanja.

Kwa kutambua hilo, Spoti Mikiki inataja sababu au maeneo yaliyochangia mafanikio ya Simba msimu huu.

Nguvu ya kiuchumi

Simba ilitenga bajeti ya takribani Sh6 bilioni kujiendesha kwenye msimu wa ligi, fedha ambazo zimetumika katika usajili, maandalizi ya timu kabla ya msimu, malipo ya mishahara na posho, gharama za kambi, usafiri na matibabu na shughuli za kiutawala. Matokeo yake yalionekana kwa Simba kuwapa huduma nzuri za daraja la juu wachezaji wake na kuwafanya kuwa katika hali nzuri kisaikolojia.

Usajili makini

Pia Soma

Kiasi cha fedha kinachokadiriwa kufikia Sh1.3 bilioni kilitumiwa na Simba kuimarisha kikosi chake msimu huu kwa kusajili nyota wapya na kuongeza mikataba ya baadhi ya wachezaji wengine ambao mikataba yao ilikuwa inaelekea ukingoni.

Baadhi ya wachezaji wapya waliosajiliwa ni Meddie Kagere, Clatous Chama, Deogratias Munishi ‘Dida’, Zana Coulibaly, Paschal Wawa na Adam Salamba.

Maandalizi bora ya msimu

Wakati kundi kubwa la timu likiweka kambi ya maandalizi ya msimu hapa nchini, Simba iliweka kambi Uturuki.

Katika kambi hiyo walikutana na miundombinu na vifaa bora ambavyo viliwapa nafasi ya kujiandaa vizuri hasa katika kujenga stamina na ufiti wa wachezaji lakini pia walipata nafasi ya kucheza mechi kadhaa za kirafiki dhidi ya timu imara ambazo ziliwapa mazoezi ya kutosha.

Benchi la ufundi

Hakuna namna unayoweza kuelezea mafanikio ya Simba katika Ligi Kuu pasipo kumtaja Patrick Aussems na wasaidizi wake ambao wamefanya kazi kubwa kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo mazuri kwenye mechi zake licha ya kukabiliwa na ratiba ngumu.

Na katika benchi hilo la ufundi la Simba, kuna mtu anaitwa Adel Zrane ambaye ni mtaalamu wa viungo na kuwaweka fiti wachezaji ambaye ametoa mchango mkubwa katika kuwafanya wachezaji wa Simba kumudu ratiba ngumu ambayo ilikuwa nayo katika Ligi Kuu msimu huu ambapo kuna wakati ililazimika kucheza mechi nne mfululizo za mikoani ndani ya siku 10.

Ubora wa wachezaji

Maandalizi na huduma nzuri ambazo Simba ilipata msimu imekuwa chachu ya kuimarisha ufanisi na mchango wa wachezaji wao ndani ya uwanja ambapo wamekuwa wakicheza kwa ari na morali ya hali ya juu tofauti na wachezaji wa timu nyingine.

Pia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja katika kikosi hicho ulichangia timu hiyo kupata matokeo mazuri na mfano ni Meddie Kagere aliyeibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 23 msimu huu. Mbali na Kagere, wengine waliokuwa chachu ya mafanikio hayo ni pamoja na Clatous Chama, John Bocco, Emmanuel Okwi na beki kiraka Erasto Nyoni.

Mashindano ya kimataifa

Baada ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na kutolewa kwenye robo fainali, kiu ya mashabiki, wanachama na wapenzi wa Simba ilikuwa ni kuona timu yao inakwenda kushiriki kwa mara nyingine mashindano ya Klabu Afrika.

Lakini kwa bahati mbaya Simba ilitolewa mapema na Mashujaa FC ya Kigoma katika raundi ya kwanza ya Kombe la Azam Sports Federation ambalo bingwa wake anawakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Chanzo: mwananchi.co.tz