Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo matatu yaliyoipa ubingwa Vijana RBA

Mambo matatu yaliyoipa ubingwa Vijana RBA

Sat, 14 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Vijana City Bulls haijachukua ubingwa wa Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) kwa bahati mbaya, kwani walijipanga mapema kutwaa ufalme huo.

Vijana City Bulls imetwaa ubingwa baada ya kuichapa Savio kwa pointi 53-51 katika mchezo uliokuwa na ushindani ambapo ulichezwa Jumatatu usiku kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa.

Vijana City Bulls ambayo ilianza vizuri na kumaliza ya pili kwenye hatua za awali za ligi ikiwa nyuma ya JKT, imebebwa na mambo matatu.

Ubora wa kikosi, malengo na uzoefu wa ligi hiyo ndivyo vitu ambavyo vimeibeba na kutwaa ubingwa mbele ya Savio.

Baada ya mechi 30 kwa timu zote 16 zinazoshiriki Ligi ya RBA kumalizika, Jogoo na Segerea BC zilishuka daraja huku nane zikifuzu kucheza robo fainali (playoff) kusaka bingwa wa msimu huu.

Timu hizo ni JKT, Kurasini Heat, Pazi, Oilers, Savio, ABC, Vijana City Bulls na Mgulani JKT.

Katika msimamo huo, Vijana City Bulls ilimaliza kwenye nafasi ya pili baada ya kushinda mechi 27 na kufungwa tatu ikiwa na pointi 58 nyuma ya JKT ambayo ilishinda mechi 28 na kufungwa mbili ikimaliza ligi kwa pointi 58, ingawa iliomba kujitoa ili ipate nafasi ya kujiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Savio ambayo haikuanza vizuri msimu kwa kufungwa mechi saba, ilimaliza ya nne katika msimamo ikiwa na pointi 52 baada ya kushinda mechi 23.

Vijana City Bulls ilitinga fainali baada ya kuifunga Ukonga Kings mechi mbili na licha ya kupoteza mchezo wa awali, ilirekebisha makosa michezo miwili na wa tatu wakati Savio iliifunga Kurasini Heat katika mechi mbili mfululizo.

Katika mchezo wa fainali, Vijana iliongoza robo ya kwanza na ya pili kwa kushinda pointi 18-11 na 10-09, Savio ikaongoza robo ya tatu kwa pointi 16-10 lakini ushindi huo haukuweza kuwapa ubingwa Savio baada ya kuruhusu sare ya pointi 15-15 katika robo ya nne na ya mwisho.

Kocha wa Vijana City Bulls, Ashraf Haroun alisema huo haukuwa ushindi wa bahati, lakini walijipanga tangu mechi ya kwanza ya ligi.

“Ndio sababu tulimaliza katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi, tulijipanga mapema, tukafanya usajili wa ubingwa, vijana walikuwa na morali ya ubingwa na tumefanikiwa,” alisema kocha Ashraf.

Ingawa kocha wa Savio, Mziray Wilfred alisema Vijana City Bulls ilipata bahati ya ubingwa kwa kuwa ilikuwa ni lazima bingwa apatikane.

“Mechi ilikuwa ngumu na bingwa ameamuliwa na muda tu, maana tulicheza kwa mtindo wa funga nikufunge, ndio sababu hata tofauti ya pointi imekuwa chache,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz