Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo matatu yaibeba KMC Ligi Kuu Bara

58284 Pic+kmc

Mon, 20 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati timu tano kati ya sita zilizopanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu zikiwa katika hali mbaya huku African Lyon ikishuka daraja, mambo yanaonekana kuinyookea KMC licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo.

Huku ikiwa haina uzoefu na Ligi Kuu, KMC ambayo ilipanda baada ya kuongoza Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza msimu 2017/2018, imetimiza malengo kwa kujihakikishia kubaki Ligi Kuu na inaweza kumaliza katika nafasi nne za juu endapo itazifunga Mbao FC na African Lyon.

Hata isipopata ushindi katika mechi hizo, inaweza kumaliza kwenye nafasi hiyo ikiwa Mtibwa Sugar, Lipuli, Ndanda na Mbeya City zitateleza kwenye mechi zao zinazofuata.

Mafanikio ya KMC yanaonekana kuchangiwa na mambo makubwa matatu usajili, benchi la ufundi na uongozi bora.

KMC ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 49 sawa na Mtibwa iliyopo nafasi ya tano, lakini inanufaika na faida ya mabao ya kufunga na kufungwa, nafasi ya saba ni Lipuli (48), Ndanda (47) na Mbeya City (46).

KMC ilitinga nusu fainali ya Kombe la Azam Sports Federation, mashindano ambayo bingwa anashiriki Kombe la Shirikisho Afrika ingawa iliondolewa na Azam kwa kipigo cha bao 1-0.

Pia Soma

Pamoja na ugeni kwenye ligi, KMC ndio timu iliyopoteza mechi chache ukiondoa Simba, Yanga na Azam kwa kuwa imefungwa mechi tisa, sare mara 16 na imeshinda michezo 11.

Mafanikio ya KMC yanakuja kipindi ambacho JKT Tanzania, Coastal Union, Alliance na Biashara United hazijajua hatima zao kama zitabaki Ligi Kuu au zitashindwa wakati African Lyon imeshateremka rasmi.

Biashara United inashika nafasi ya 18 ikiwa na pointi 40, JKT Tanzania ipo nafasi ya 17 na pointi 41, Coastal Union nafasi ya 12 ikiwa na pointi 44 wakati Alliance ni ya 11 na pointi ilizokusanya ni 44.

Akizungumza jana, Kaimu Katibu Mkuu wa KMC, Walter Harrison alitaja mambo matatu yamechangia KMC itikise kwenye Ligi Kuu licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza.

“Kwanza ni uwepo wa kocha mzuri wa daraja la juu Etienne Ndairagije, ana uwezo mkubwa wa kuwaandaa, kuwajenga na kuwaunganisha wachezaji hasa vijana, pili tulifanya usajili mzuri wa wachezaji ambao kundi kubwa walikuwa ni vijana wenye kiu, njaa ya mafanikio na vipaji.

“Jambo jingine ni uongozi sikivu. Mnapokuwa na viongozi wanaosikilizana, inakuwa ni rahisi kuwa na malengo yanayofanana na kuendesha vyema timu pasipo migogoro. Ndiyo maana unaona timu inapata huduma zote kwa wakati,” alisema Harrison.

Kocha Ndairagije alisema kiufundi timu yake inabebwa na uwepo wa wachezaji bora ambao wanafanyia kazi kile wanachoelekezwa na benchi la ufundi.

“Unaweza kuwa na wachezaji wenye vipaji lakini wasiwe na msaada kwenye timu ikiwa hawafuati kile ambacho wanatakiwa wakifanye.

“Binafsi nafurahi kuona vijana wangu wana nidhamu ya kufuata kile wanachotakiwa wakifanye na ndiyo maana tumeweza kumudu ushindani wa ligi,” alisema Ndairagije.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aaron Kagurumjuli alisema KMC inaendeshwa kwa mfumo wa taasisi hata ikitokea hatakuwepo katika nafasi hiyo timu itaendelea kuhudumiwa na manispaa.

“Kuna Bodi ya timu na Katibu wa Bodi ni mimi (Mkurugenzi), tumeweka mazingira ya timu yetu kuendeshwa kitaasisi, haiendeshwi na mtu, hivyo ikitokea sipo bado timu itaendelea kuhudumiwa,” alisema Kagurumjuli.

Mkurugenzi huyo alisema timu ina bajeti ya halmashauri na inaandaliwa ipasavyo ndiyo sababu imeweza kupambana licha ya uchanga ilionao kwenye Ligi Kuu.

Chanzo: mwananchi.co.tz