Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo 6 yaigharimu Simba

40176 Pic+simba Mambo 6 yaigharimu Simba

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kucheza chini ya kiwango kwa Simba katika kipindi kisichozidi siku 20 ni matokeo ya mambo sita ambayo yasipofanyiwa kazi, inaweza kujikuta ikifanya vibaya zaidi licha ya uwekezaji iliyofanya.

Uvivu wa wachezaji ndani ya uwanja, mbinu zisizoendana na ubora na udhaifu wa wapinzani, nidhamu nje ya uwanja kwa wachezaji, ufiti wa mwili kwa nyota wa kikosi chake, makosa binafsi ya mchezaji mmoja mmoja na ufanisi duni wa wachezaji wa kigeni, kwa kiasi kikubwa vimeiangusha Simba katika siku za hivi karibuni.

Ndani ya siku 18, Simba imejikuta katika wakati mgumu kupata matokeo mazuri ndani ya uwanja ambapo kwa mechi tano ilizocheza kwenye mashindano mawili tofauti, imepata ushindi ndani ya dakika 90 mara moja, ikitoka sare moja na kupoteza michezo mitatu.

Katika mechi tano ilizocheza ndani ya siku hizo ambazo hazizidi 20, Simba imefunga mabao mawili huku safu yake ya ulinzi ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 13.

Simba inayosifiwa kwa safu kali ya ushambuliaji kwa timu za Afrika Mashariki na Kati, kati ya mechi tano ilizocheza ndani ya siku 18, ilimaliza mechi tatu bila kufunga bao huku ikifanya hivyo kwenye mechi mbili tu.

Majanga kwa Simba yalianzia Januari 19 ilipochapwa mabao 5-0 ugenini huko DR Congo mbele ya AS Vita katika mchezo wa raundi ya pili ya hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi D.

Baada ya mchezo huo ilirejea nchini na moja kwa moja ilishiriki Kombe la SportPesa ambapo ilianza kwa kuichapa AFC Leopards ya Kenya mabao 2-1 katika mechi ya robo fainali.

Ndoto ya Simba kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ziliyeyuka katika mechi ya nusu fainali baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Bandari FC ya Kenya.

Jinamizi la Simba ndani ya dakika 90 liliendelea baada ya kutoka sare na Mbao katika mechi ya kuwania mshindi wa tatu ingawa ilikuja kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 5-4.

Baada ya kumalizika mashindano hayo, Simba ilirejea kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambako Februari 2 ilinyukwa mabao 5-0 na Al Ahly mjini Cairo.

Moja ya mambo yanayoonekana kuiangusha Simba ni kitendo cha wachezaji wake kutoonekana kujituma ndani ya uwanja, jambo ambalo linawapa nafasi wapinzani wao kuwaadhibu.

Jambo la pili ni kitendo cha benchi la ufundi kutumia mbinu ya aina moja katika kila mchezo pasipo kubadilika kulingana na aina ya mpinzani wanayekutana naye.

Katika mechi zote ilizocheza, Simba imekuwa ikitumia mfumo wa 4-4-2 usiokuwa na mawinga halisi jambo linalofanya wapinzani kupata uhuru wa kuwashambulia wakitokea pembeni mwa uwanja.

Kingine ni nidhamu duni ya wachezaji wa Simba ambao wanadaiwa kutoheshimu kambi kipindi wanachokaribia kucheza mechi, hatua ambayo pengine inachangia wakose utulivu wa akili na mwili wa kujiandaa na mechi husika.

Jambo la nne ni makosa binafsi ya wachezaji ndani ya uwanja hasa katika kuzuia pindi wanaposhambuliwa, mfano kusababisha faulo zisizokuwa na sababu, lakini pia kuivunja yenyewe mitego ya kuotea ambayo timu inaiweka inapokabiliwa na mashambulizi ya timu pinzani.

Mbali na hilo, kingine kinachoonekana kuigharimu Simba ni wachezaji wake wengi kuonekana kutokuwa fiti na hii ni wazi kuwa inasababishwa na kutocheza mechi za kutosha zinazoweza kuwafanya kuwa vizuri.

Katika kipindi cha hivi karibuni, Simba imekuwa haichezi mechi za Ligi Kuu lakini hata zile za mashindano mengine ya kawaida, benchi la ufundi limekuwa likipumzisha kundi kubwa la wachezaji jambo linalowafanya wakose maandalizi mazuri ya kimwili kucheza mechi za kimataifa.

Hadi sasa Simba ina tofauti ya mechi 10 za viporo wakati tayari kuna baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara zimefikisha michezo 24.

Pia wachezaji wa kigeni wengi wameonekana kutokuwa na msaada kwenye timu hiyo na kuthibitisha hilo katika mechi dhidi ya Al Ahly kocha Patrick Aussems aliwapanga wachezaji wanane na wazawa watatu tu.

Msikie Aussems

Aussems alisema baada ya kufungwa na Al Ahly, mkakati wake ni kushinda mechi zilizobaki ingawa haitakuwa kazi nyepesi kwa kuwa timu hiyo na AS Vita ni klabu kubwa Afrika.

“Tumefuatilia timu zote tatu ambazo tumecheza nazo tunafahamu ugumu, ubora na udhaifu wa timu hizo ambazo tutashindana nazo kadri tunavyoweza ili kufikia malengo ya timu,” alisema Aussems muda mfupi baada ya kuwasili Dar es Salaam jana akitokea Misri.

Kauli ya Msola, Kibadeni

Kocha wa zamani wa Taifa Stars Dk Mshindo Msola alisema ameshitushwa na kauli ya Aussems kukiri AS Vita na Al Ahly siyo saizi ya Simba wakati awali alitamba anakwenda kushinda.

“Tatizo walipofungwa mabao 5-0 na AS Vita hawakuifanyia tathimini ile mechi kabla ya kuikabili Al Ahly, ndiyo maana makosa yaleyale yalijirudia katika mechi na Al Ahly.

“Benchi la ufundi na wachezaji wote wana makosa na wasipoangalia wanaweza kufungwa hata hapa nyumbani kwa sababu kama wangeifanyia tathimini mechi ya AS Vita wasingekwenda na aina ya soka la kushambulia, lazima wangebadilisha plani nyingine ikiwemo kukaa nyuma ya mpira na kujilinda huku wakifanya mashambulizi ya kushitukiza kwa kupiga pasi ndefu.

“Simba wanacheza soka la pasi nyingi zisizokuwa na faida, hivyo wanatakiwa kubadilika la sivyo mbele ya safari wanaweza kupata aibu kubwa zaidi,”alisema Msola.

Kocha wa Prisons Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema Simba ina tatizo kubwa la umakini hasa katika safu ya ulinzi na alionya bila kufanyiwa kazi haraka timu hiyo inaweza kukumbana na mvua nyingine ya mabao katika mechi zijazo.

“Fikiria kama wachezaji wa klabu kubwa kama Simba wanaweza kutoroka kambini huku wakijua wana mashindano makubwa, umakini utatoka wapi uwanjani.

“Wenzetu Waarabu wako makini katika idara zote kuanzia wachezaji, viongozi ndio maana wanafanikiwa lakini sisi tunafanya mambo kisiasa yaani tukimfunga Ndanda kwenye ligi tunaona tumemaliza,” alisema Kibadeni aliyewahi kuwa mshambuliaji nyota wa Simba. Stars enzi zake.



Chanzo: mwananchi.co.tz