Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo 5 yaliyotikisa Stars ikifuzu Afcon

48735 5+PC

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu kuzimia na wengine kujeruhiwa ni miongoni mwa matukio matano makubwa yaliyojiri kabla na baada ya mchezo baina ya timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ na Uganda ‘The Cranes’.

Timu hizo zilivaana juzi jioni katika mchezo wa mwisho kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Taifa Stars ilishinda mchezo huo na kufuzu fainali hizo baada ya kupita miaka 39. Mara ya mwisho Tanzania ilishiriki fainali hizo mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria.

Mabao ya Saimon Msuva, Erasto Nyoni na Aggrey Morris, yaliwapa raha maelfu ya Watanzania waliokwenda uwanjani kushuhudia mchezo huo wa Kundi L.

Hata hivyo, furaha ya baadhi ya mashabiki hao iligeuka shubiri baada ya kuzimia na wengine kujeruhiwa katika matukio tofauti.

Baadhi ya mashabiki waliumia walipojaribu kuruka geti kuingia ndani ya uwanja na wengine walizimia baada ya Taifa Stars kufunga bao la kwanza.

Msongamano

Pia tukio la msongamano wa mashabiki lilitia dosari baada ya polisi kutumia mbwa kuwatawanya ambapo baadhi yao walianguka walipokuwa wakijaribu kujiokoa.

Msongamano huo haukuiacha salama timu ya Uganda iliyolazimika kusubiri kwa dakika kadhaa kabla ya kuruhusiwa kuingia ndani baada ya polisi kutawanya mashabiki katika eneo la lango kuu la kuingia.

Ndani ya uwanja hali ilikuwa tete kwa mashabiki ambao kutokana na wingi huo walilazimika kukaa kwenye ngazi na kusababisha vurugu na msongamano mkubwa uliowaopa kazi ya ziada watu usalama.

Tiketi

Tukio jingine lililochomoza uwanjani hapo ni idadi kubwa ya mashabiki kurejea uwanjani na tiketi zao baada ya kukosa nafasi ya kuingia.

Mashabiki hao walionekana wakilalamikia kitendo cha wasimamizi wa mchezo huo kushindwa kuweka utaratibu mzuri wa kuingia uwanjani.

Baadhi wakionekana kuchukizwa na kadhia hiyo walisikika wakisema walikwenda uwanjani mapema, lakini walishindwa kuingia kushuhudia mchezo huo kutokana na msongamano.

Wakati mashabiki wakiendelea kupimana ubavu mlangoni, tangazo ndani ya uwanja lilisikika likiwataka mashabiki kutokwenda uwanjani na badala yake wafuatilie mchezo huo kupitia luninga.

Uganda, Stars raha tupu

Huenda katika baadhi ya nchi nyingine duniani linaweza kuwa tukio la kushangaza, lakini kwenye mechi ya Taifa Stars na Uganda, limetokea.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, raia wa Tanzania na Uganda walikaa pamoja na kushangilia timu zao kwa pamoja jukwaani kwa raha zao.

Mashabiki wa Tanzania na Uganda waliokuwa wamejipamba kwa rangi za bendera za nchi zao, walishangilia matukio yaliyojiri uwanjani hapo na wengine walionekana wakifurahi kwa pamoja.

Baadhi ya mashabiki wa Uganda waliokuwa wamekaa katika viti vya VIP B na Taifa Stars walipiga ngoma na kuimba nyimbo za utamaduni wa mataifa yao.

Mageti 11 yavunjwa

Si taarifa njema, lakini imetokea. Mchezo huo umeacha maumivu kwa wasimamizi wa uwanja huo baada ya mageti 11 kuvunjwa na mashabiki baada ya kutokea vurugu.

Mageti hayo yalivunjwa baada ya idadi kubwa ya mashabiki waliokuwa nje ya uwanja walipolazimisha kuingia ndani.

Polisi waliokuwa wakilinda usalama walizidiwa nguvu na idadi kubwa ya mashabiki ambao kwa umoja wao walivunja mageti na kuingia ndani kushuhudia mchezo huo.

Akizungumzia matukio yaliyojiri katika mchezo huo, Meneja wa Uwanja wa Taifa, Gordon Nsajigwa alisema uharibifu mkubwa wa vifaa umefanywa na mashabiki.

“Katika mechi kubwa kama ile ni kawaida vitu kama koki za maboma na vyooni kuharibika yakiwemo mageti,” alisema meneja huyo.

Nsajigwa alisema mageti mawili yalivunjika na mengine tisa yaliharibika baada ya mashabiki kuvamia.

Meneja huyo alisema wanatarajia kufanya tathimini kubaini chanzo cha uharibifu kama wahusika ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuweka kiingilio kidogo, polisi hawakusimamia vyema suala la ulinzi au mageti ya uwanja hayakuwa imara hata kabla ya mchezo.



Chanzo: mwananchi.co.tz