Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo 3 yampa ulaji Kahata Simba

65546 Kahata+pic

Fri, 5 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mambo matatu yanaweza kuwa sababu zilizoishawishi Simba kumsajili kiungo mshambuliaji wa Kenya, Francis Kahata ambaye huenda leo akakamilisha mpango wa kujiunga na timu hiyo.

Ubora wa nyota huyo ambaye ametoka kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu huko Misri akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, uzoefu alionao wa soka la Afrika pamoja na gharama ndogo za usajili wake, vinaweza kuchangia kuivutia Simba kumnasa nyota huyo.

Kahata anayemudu vyema kucheza kama mshambuliaji wa pili, winga wa pembeni pamoja na kiungo mshambuliaji namba nane, ana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao, kupiga pasi za mwisho kwa washambuliaji na pia kuchezesha timu jambo ambalo litakuwa faida kwa Simba kutokana na ugumu wa mashindano na aina ya wapinzani ambao inaelekea kukutana nao kwenye Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27 ambaye amekuwa akitumia zaidi mguu wake wa kushoto, anabebwa na sifa nyingine ambayo ni kuvunja ukuta wa timu pinzani pamoja na kufunga mabao na kutokana na kimo chake cha mita 1.78, Kahata ni mchezaji anayetumia zaidi akili pasipo kutegemea sana matumizi ya nguvu.

Pamoja na ubora wake akitegemewa kuziba nafasi ya Haruna Niyonzima ambaye hajaongezewa mkataba, Kahata anasajiliwa na Simba akiwa na uzoefu wa kutosha wa soka la Afrika ambapo amefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2018 akiwa na Gor Mahia ya Kenya na msimu wa 2018/2019 alikuwemo kwenye kikosi cha timu hiyo kilichofuzu hatua ya robo fainali ya mashindano hayo, huku pia akiwa ametwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mara tatu mfululizo.

Ameshakutana mara kadhaa na timu za Tanzania katika mashindano mbalimbali ambapo mwaka 2018, alikumbana na Yanga mara mbili kwenye Kombe la Shirikisho na mwaka huu alikutana na Mbao FC kwenye Kombe la SportPesa.

Pia Soma

Pamoja na mambo hayo mawili, sababu nyingine ambayo huenda ikawa imeishawishi Simba kumsajili Kahata, ni gharama nafuu za dau lake kwani kwa sasa mkataba wa kiungo huyo na Gor Mahia umemalizika hivyo anajiunga kama mchezaji huru ikimaanisha kuwa Simba haitaingia gharama mara mbili ambazo ni ile ya kuvunja mkataba na fungu la mchezaji kwa ajili ya kutia saini.Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, awali Simba haikuwa kwenye mipango ya kumsajili Kahata lakini ghafla imeamua kumuweka kwenye hesabu zake baada ya kupendekezwa na Kocha Patrick Aussems ambaye yuko kwenye mpango kabambe wa kusuka kikosi chake.

Nyota huyo ambaye katika mashindano ya AFCON yanayoendelea huku Misri, ameanza kwenye kikosi cha kwanza mara mbili dhidi ya Algeria na Tanzania, inadaiwa kuwa leo atawasili nchini tayari kukamilisha uhamisho huo.

Kauli ya Matola

Nyota wa zamani wa Simba, Selemani Matola alisema uwezo wa Kahata na Niyonzima unaelekea kufafana isipokuwa Mkenya huyo ana vitu vya ziada.

“Kahata ana faida zaidi, kwani anapiga pasi za mbele, anafunga hata kukaba vilevile ana nguvu kuliko Niyonzima,” alisema kiungo huyo wa zamani wa Simba na Taifa Stars.

Kocha huyo alisema kama wachezaji hao wakisajiliwa timu moja kama ambavyo Simba wanapishana kuhusu kumrejesha tena Niyonzima, kuwatumia wote kwa wakati mmoja itategemea na falsafa ya kocha kulingana na aina ya mechi.

Chanzo: mwananchi.co.tz