HAKUJAWA na mazungumzo kuhusu wachezaji bora zaidi duniani ambayo hayajamuhusisha Cristiano Ronaldo, angalau kwa muongo mmoja uliopita. Ukuaji wake katika klabu ya Manchester United ulimpandisha nyota huyo wa Ureno hadi kileleni.
Uwapo wake Real Madrid ulifanya LaLiga kuwa mpya kila wakati. Hata sasa kazi yake inaendelea kuchanua pale Old Trafford.
Pengine mfungaji mahiri zaidi katika soka la kisasa, Ronaldo amevunja rekodi nyingi, hata nyingine alizokuwa tayari ameziweka mwenyewe. Nyota huyo wa 'Mashetani Wekundu', alishinda tuzo yake ya kwanza ya Ballon d'Or akiwa na umri wa miaka 23. Sasa akiwa na umri wa miaka 36, bado yuko kwenye kinyang'anyiro cha kuwania tuzo hiyo maarufu zaidi katika soka la dunia.
Ni wachezaji wachache tu mbali na Ronaldo wamecheza zaidi ya mechi 1,100 wakiwa na takriban mabao 800. Ikumbukwe kwamba nyota huyo pia ana mabao na asisti nyingi zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika kipindi chote cha uchezaji wake, ameshinda rekodi ya mataji 32 makubwa. Hii ni pamoja na taji la Serie A, mataji ya LaLiga, taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, na mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu England. Ni wazi kuwa ni mchezaji mahiri wa kiwango cha kimataifa kwa kila namna.
Nyota huyo wa Ureno ndiye mwanamichezo mwenye ushawishi mkubwa zaidi duniani. Ufuasi wake mkubwa wa mitandao ya kijamii ni mkubwa zaidi.
Haishangazi kwamba wachezaji wenzake, wapinzani, makocha, na hata magwiji wa soka wamezungumza kwa mshangao juu ya chapa yake ya CR7 anayoigiza. Makala haya tunaangalia nukuu 10 zinazozungumzwa kuhusu Ronaldo, ikiwa ni pamoja na moja kutoka kwa mpinzani wake pekee, Lionel Messi, haya sasa...
#10. Eusebio | Gwiji Benfica
Kabla ya Ronaldo, kulikuwa na gwiji mwingine wa Ureno ambaye aliichukua Ulaya kwenye miguu yake, akifunga mabao 733 katika mechi 745, ambaye ni Eusebio. Mshambuliaji huyu aliwahi kumzungumzia Ronaldo akisema: "Ana uchawi kwenye vitu vyake. Jambo la kwanza unalogundua juu yake ni kwamba ana haraka sana na ana nguvu sana. Ana udhibiti mkubwa na mbinu zake ni bora. Anaamini kuwa anaweza kufanya lolote akiwa na mpira, na kujiamini huko kunamfanya awe wa pekee sana.”
#9. Johan Cruyff | Gwiji Barcelona
Johan Cruyff tayari alikuwa mshindi wa Ballon d'Or mara tatu kabla hata hajajiunga na Barcelona mwaka 1988.
Anachukuliwa na wengi kama mmoja wa wachezaji bora zaidi katika historia ya mchezo huo mzuri. Wachezaji wengine waliofanikiwa sana ni pamoja na George Best na Denis Law, ambao Cruyff aliwalinganisha na Cristiano Ronaldo na kusema: "Cristiano Ronaldo ni bora kuliko George Best na Denis Law, ambao walikuwa wachezaji wawili mahiri na wazuri katika historia ya Manchester United."
#8. Sir Bobby Charlton | Gwiji Manchester United
Sir Bobby Charlton anafahamika kwa kushinda Kombe la Dunia akiwa na England na kutwaa Ballon d'Or pia. Yeye ni mmoja wa viungo wakubwa katika historia ya soka duniani. Charlton alinusurika kwenye ajali ya ndege ya Munich mwaka 1958. Alibaki Old Trafford kuiongoza Man United kurudi kwenye utawala wa soka la Uingereza na Ulaya.
Wayne Rooney, Sir Bobby Charlton, George Best na Cristiano Ronaldo ndio pekee wamefunga mabao mengi zaidi kwa Man United kuliko, Marcus Rashford kabla ya kufikisha miaka 23.
Gwiji huyo aliona mengi wakati wa maisha yake ya soka, lakini anamchukulia Ronaldo kama keki na alisema: "Cristiano Ronaldo anabadilisha mchezo nchini Hispania. Kwa kasi hiyo na nguvu, anairudisha Real Madrid kwenye utawala huko na Ulaya. Nina furaha sana amepata tuzo yake ya Mwanasoka Bora wa Dunia wa Mwaka. Lionel Messi ni mchezaji mzuri pia, lakini Cristiano anastahili heshima hiyo."
#7. Jose Mourinho | Kocha AS Roma
Uhusiano kati ya Jose Mourinho na Cristiano Ronaldo haujawa mzuri kila wakati. Mourinho alikuwa akiinoa Real Madrid kuanzia mwaka 2010 hadi 2013, alipomsimamia Ronaldo.
Katika kipindi hiki, Mourinho alimkosoa Ronaldo kwa kushindwa kukubali kukosolewa, akieleza: "Labda (Cristiano Ronaldo) anafikiri kwamba anajua kila kitu na kwamba kocha hawezi kumboresha tena..."
“Hata hivyo, hiyo haikupunguza maneno mazuri ya Mourinho juu ya Ronaldo akisema: "Nilimwona (Diego) Maradona mara kadhaa. Sikuwahi kumwona Pele. Lakini Cristiano ni wa kushangaza. Mtu huyu ndiye bora zaidi… Cristiano ni mashine ya mabao. Ni mchezaji wa ajabu. Ni kama (Zinedine) Zidane, hakutakuwa na Ronaldo mwingine.”
#6. Ronaldo Nazario | Rais wa Real Valladoid na Gwiji wa Real Madrid
Ronaldo Nazario de Lima alikuwa mmoja wa wachezaji wachache waliong'ara Barcelona na Real Madrid. Mbrazil huyo alikuwa mmoja wa washambuliaji wakatili zaidi wa miaka ya 1990 na 2000.
Alishinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia wa FIFA akiwa na umri wa miaka 20, pia alishinda Ballon d'Or akiwa na umri wa miaka 21. Kwa uhodari wake wote, Ronaldo de Lima bado anaona Cristiano Ronaldo ni mchezaji wa aina yake na alinukuliwa akisema: "Nilifanya mazoezi kwa sababu nililazimika. Anafanya mazoezi kwa sababu anapenda. Ni wachezaji wachache sana wanaoitunza miili yao, wana nia kali ya kutaka kuimarika. Yeye ni wa aina yake.”
#5. Robbie Ryan | Gwiji Millwall
Robbie Ryan na Millwall walikutana na Cristiano Ronaldo na Manchester United katika fainali ya Kombe la FA mwaka 2004. Ingawa Millwall haikuweza kufurukuta kabisa dhidi ya kikosi kikatili cha United. Na baada ya mchezo huo Ryan alinukuliwa akimzungumzia Ronaldo akisema: "Sijawahi kucheza dhidi ya mtu yeyote kama huyo maishani mwangu na nilifurahi sana."
#4. Sir Alex Ferguson | Gwiji Manchester United
Cristiano Ronaldo aliwahi kumtaja Alex Ferguson kama baba, na magwiji wengi wa Manchester United wanaweza kukubaliana na mtazamo huo. Alikuwa ni Ferguson aliyemleta nyota huyo kutoka Sporting ya Ureno.
Ilikuwa Ferguson ambaye alimpa Ronaldo wakati wa kucheza aliohitaji ili kuboresha kiwango chake kwa kiasi kikubwa.
Ronaldo amerejea Man United na ujuzi wake wa kufunga mabao bado uko juu. Kwa Ferguson, Ronaldo ni mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea na alisema: "Tumekuwa na wachezaji wazuri katika klabu hii katika miaka yangu 20, lakini yeye ni bora zaidi."
#3. Zinedine Zidane | Gwiji Real Madrid
Wakati Zizou alikuwa mchezaji wa Real Madrid, alishinda mataji sita makubwa, ikiwa ni pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Aliporudi kama kocha, aliipa 'Los Blancos' mataji 11.
Alimtaja Ronaldo kama mchezaji wake muhimu zaidi kupitia mafanikio yake ya ukocha akisema: "Unapocheza na Ronaldo kwenye timu yako, tayari uko mbele kwa bao 1-0."
#2. Carlos Quieroz | Kocha timu ya Taifa ya Misri
Muda wake kama kocha pale katika dimba la Santiago Bernabeu unaweza kuwa hakuwa na mafanikio makubwa, lakini kazi yake kama kocha msaidizi wa Manchester United ilikuwa nzuri. Quieroz alitumia miaka mitano kuwafundisha Ronaldo na 'Mashetani Wekundu'. Hii ilimpa ufahamu wa kipaji cha Ronaldo, akimlinganisha nyota huyo na Michael Jordan kwa kusema: “(Yeye ni) nyota wa dunia katika soka kama Michael Jordan alivyokuwa kwenye mpira wa kikapu … Wote wawili wamebarikiwa kuwa na kipaji ambacho hakijawahi kuonekana hapo awali.”
#1. Lionel Messi | Gwiji Barcelona, mpinzani wa cr7
Wachezaji wote wawili wameshiriki jukwaa la Ballon d'Or mara nyingi sana katika muongo mmoja uliopita na ni wazi hakuna mchezaji bora kuliko wawili hao. Wakati Messi akiwa Barcelona, mechi za upinzani dhidi ya Cristiano Ronaldo na Real Madrid zilikuwa na watazamaji duniani kote. Kila mtu alitaka kuwaona nyota wote wawili.
Mwezi mmoja kabla, Messi na Ronaldo walikuwa hawaendi popote. Mwezi mmoja baadaye, wote wawili wakahama klabu zao katika dirisha moja la uhamisho.
Ushindani wao, haujamzuia Messi kushangaa jinsi Ronaldo alivyo na kipaji. Alitoa maoni yake akisema: "(Ronaldo) huwa anafunga mabao katika michezo yote anayoshiriki katika klabu yake na timu ya taifa. Amekuwa akifanya hivyo kwa miaka mingi akiwa kwenye kilele chake au chini kidogo haileti tofauti.”