Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama Samia atoa neno kwa wanariadha

28d1b98970571d0ccca23f0d8249e66f.jpeg Mama Samia atoa neno kwa wanariadha

Mon, 23 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wanariadha wanaojiandaa kwenda kushiriki mashindano ya Olimpiki kwenda kushinda ili kuwafuta Watanzania machozi ya muda mrefu.

Akizungumza baada ya kushiriki NBC Dodoma Marathon jijini hapa juzi, Mama Samia alisema muda umefika sasa kama nchi kuzalisha akina Philbert Bayi wengi zaidi.

"Leo nimeshuhudia wanariadha wazuri sana ila huwa najiuliza tukifika kwenye medali za kimataifa tunakwama wapi?"

"Niwaombe wana riadha wanaojiandaa kwenda kwenye mashindano ya kimataifa kwenda kushinda ili kutufuta machozi Watanzania machozi ambayo tumekuwa nayo kwa muda mrefu na warudi nyumbani na medali za kutosha," alisema.

Samia aliwatakia kila la kheri wanaridha wanaokwenda katika mashindano hayo na akawataka kujiandaa vizuri.

Katika mbio hizo za Dodoma Marathon ambazo zilikuwa za kuunga mkono harakati dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi kwa ushirikiano na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na benki ya NBC, wakiambiaji kutoka Tanzania, Kenya na Uganda walichuana vikali.

Mbio hizo zimezofanyika kwa mara ya kwanza jijini humo na kuvutia washiriki zaidi 3,000 kutoka ndani na nje ya nchi ambao walishinda zawadi mbalimbali ikiwamo fedha taslimu na medali kutoka kwa waandaji.

Katika mbio hizo ilishuhudiwa Mganda, Philip Kiplimo akiibuka mshindi wa kwanza kwa mbio za kilomita 42.2 kwa kutumia muda 2:17:26 hivyo kujishindia zawadi ya Sh milioni 3.5, wakati Hamis Misai wa Tanzania na Stanley Kipchirchir wa Kenya wakiibuka washindi wa pili na watatu kwa kutumia muda wa saa 02:17:35 na 02 19:13.

Kwa upande wa wanawake, mbio za kilomita 42 Mkenya, Nyawira Muriuki aliibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia muda wa saa 02:40:14, wakati mwenzake, Cheruto Isgah na Mtanzania Natalia Elisante waliibuka washindi wa pili na wa tatu kwa kutumia muda saa 02:41:02 na 02:49:26 kwa mfuatano.

Katika mbio za kilomita 21.1 kwa upande wa wanaume ilishuhudiwa Watanzania wakitamba zaidi kwa kushinda nafasi zote tatu za juu, ambapo Gabriel Geay alishinda nafasi ya kwanza kwa kutumia muda wa saa 01:04:28, Fabiano Sule akishika nafasi ya pili kwa kutumia muda wa saa 01:04:49 na Mathayo Sombi akitumia saa 01:04:59 na hivyo kuwa mshindi wa tatu.

Mwanariadha Doreen Chemutai wa Uganda alishinda mbio hizo kwa wanawake ambapo alitumia muda wa saa 01:13:45.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa mbio hizo, Samia, aliipongeza Benki ya NBC kwa kushirikiana na Shirikisho la Riadha Taifa kwa kuandaa mbio hizo ikiwa ni mkakati wa wadau hao kukuza vipaji vya mchezo huo sambamba kupambana na saratani ya mlango wa kizazi kwa akinamama.

"Shirikisho la Riadha, Benki ya NBC kwa kushirikiana na wadau wengine mmefanya kazi nzuri na huu ni mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine. Saratani ya kizazi imekuwa ikiathiri sana wanawake wengi hapa nchini hivyo jitihada hizi ni za kuigwa,’’ alisema.

Alisema iwapo mchezo wa riadha ukitumika vizuri unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii na kutumika katika kuongeza uelewa pamoja na kutangaza ajenda muhimu za kitaifa ikiwamo utalii.

Alipendekeza mbio hizo zifahamike kwa jina la NBC Dodoma Marathon huku akiitaka benki hiyo kuiendeleza kwa viwango vya kimataifa zaidi, kuvutia washiriki wengi wa kimataifa ili ziweze kutumika pia katika kutangaza utalii wa ndani.

Chanzo: habarileo.co.tz