Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malinzi, wenzake kizimbani tena kesho, askari wa JWTZ naye yumo

39873 Pic+kesi Malinzi, wenzake kizimbani tena kesho, askari wa JWTZ naye yumo

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kesho Jumatatu Februari 3, 2019 itaendelea kusikiliza ushahidi katika kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha inayomkabili aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake wanne.

Tayari mashahidi 11 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao. Miongoni mwa mashahi hao ni aliyekuwa Mhasibu wa TFF, Sereck Mesack (68).

Katika ushahidi wake alioutoa Desemba 5, 2018, Mesack alieleza kuwa Malinzi aliwahi kuikopesha TFF,  Dola 41,000 katika kipindi cha mwaka 2016. Mesack ambaye ni shahidi wa tisa, alidai katika kipindi hicho, Malinzi pia aliikopesha TFF, Sh22 milioni.

Alisema fedha hizo, zilitumika kulipia posho na gharama za kuipeleka Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, katika nchi ya Rwanda na Congo.

Mbali na Malinzi, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa katibu mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine (46) na mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga (27).

Wengine ni meneja wa ofisi TFF, Miriam Zayumba na karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha, Dola 173,335.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wanaendelea kusota rumande kwa sababu wanakabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, kesi ya mauaji inayomkabili askari wa Jeshi la  Wananchi Tanzania (JWTZ) Ramadhan Mlaku (28) pia itatajwa mahakamani hapo. Mlaku anakabiliwa na shtaka moja la mauaji, akidaiwa kumuua mwanajeshi mwenzake.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Mlaku anadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 30, 2017, eneo la  Upanga, makao makuu ya Jeshi hilo.

Mlaku anadaiwa kumuua mwanajeshi mwenzake mwenye namba MT 79512, Sajenti Saimon Munyama.

Kwa mara ya kwanza, Mlaku alifikishwa mahakamani hapo, Machi 14, 2018, akiwa katika gari la kubebea wagonjwa (Ambulance).

Wakati huo huo, kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili watu watano, itatajwa Mahakamani hapo.

Washtakiwa hao ni Salehe Majaliwa (31) mfanyabiashara na mkazi wa Kigamboni na Mwanaisha Ndwangila (36), mkazi wa Tunduru.

Wengine ni Sauda Athuman (36) maarufu kama Kipeleka na mkazi wa Mbagala, Hamisi Ulega (27) mkazi wa Lindi na dereva Abdallah Mohamed (38) maarufu kama Bambo, mkazi wa Kilwa Masoko  mkoani Lindi.

Kwa pamoja washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kukutwa na vipande 18 vya meno ya tembo, vyenye thamani ya Sh 171, 796, 500, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mara  ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Desemba 12, 2018 wakikabiliwa na mashtaka hayo.

Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili ni kuongoza mtandao wa uhalifu, kosa ambalo linamkabili mshtakiwa wa kwanza hadi wa nne.

Inadaiwa kuwa katika tarehe tofauti, kati ya Novemba Mosi na Novemba 21, 2018,  Dar es Salaam na Lindi, kwa pamoja walishiriki kuuza nyara za Serikali, ambazo ni vipande 18 vya meno ya tembo, vyenye thamani ya dola  75,000 sawa na Sh171, 796, 500, bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori.



Chanzo: mwananchi.co.tz