Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha wa kigeni wampa mchongo Amunike

18428 Pic+makocha TanzaniaWeb

Fri, 21 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Makocha wa kigeni wanaofundisha timu za Ligi Kuu Tanzania Bara, wametoa ushauri na mbinu zitakazoiwezesha timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ kupata matokeo mazuri katika mechi mbili za nyumbani na ugenini dhidi ya Cape Verde mwezi ujao.

Mechi hizo mbili zilizopo Kundi L zina nafasi kubwa ya kuamua hatima ya Taifa Stars kufuzu Fainali za Afrika (Afcon), zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.

Hata hivyo, kubanwa kwa ratiba ya mechi hizo mbili ambazo zitachezwa ndani ya muda usiozidi saa 120 kunaweza kuwa kikwazo kwa Taifa Stars kuvuna pointi sita muhimu dhidi ya Cape Verde ambazo zitaiweka karibu na lango la Fainali za Afrika.

Taifa Stars itaanzia ugenini jijini Praia, Cape Verde ambako Oktoba 12 itakabiliana na wenyeji wao kabla ya kulazimika kusafiri kwa mechi ya marudiano itakayochezwa Oktoba 16 Dar es Salaam ikiwa ni kipindi cha siku nne ambacho mechi hizo zitachezwa.

Muda wa siku nne ambao Taifa Stas itacheza mechi hizo na umbali mrefu ambao msafara wake utasafiri kwenda Cape Verde na kurudi nchini, unaweza kuiathiri kama ilivyotokea miaka mitatu iliyopita ilipojikuta ikiathirika na ratiba ya namna hiyo katika mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Algeria.

Novemba 14 ilitoka sare ya mabao 2-2 na Algeria katika mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam kabla ya kulala 7-0 ziliporudiana ugenini.

Katika kuhakikisha mzimu wa mwaka 2015 haujirudii na timu hiyo icheze fainali hizo, makocha wa kigeni wanaofundisha timu za Ligi Kuu Bara wametoa maoni nini kifanyike kukabiliana na ratiba iliyoko mbele yake.

“Jambo la msingi Shirikisho la Soka Tanzania, linapaswa kuhakikisha linatenga muda wa kutosha kwa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani waliopo kwenye kikosi cha Taifa Stars wanapata muda wa kutosha kupumzika.

“Nimewaona na kuifuatilia kwa ukaribu Cape Verde ilipocheza na timu yetu ya Taifa na DRC. Sio timu nyepesi ina wachezaji wazuri ambao wengi wanacheza nje. Stars inapaswa kuingia kwenye mchezo huo wachezaji wakiwa fiti zaidi.

“Bahati nzuri naamini timu ya Taifa ya Tanzania imeimarika sana kwa sasa ina ubora. Kutokana na hilo, ni lazima kuhakikisha inaingia na kikosi kilichokamilika cha wachezaji wasiokuwa na uchovu, hivyo hakuna haja ya kuweka mechi nyingi mfululizo za ligi katika kipindi ambacho Taifa Stars inajiandaa kucheza na Cape Verde,” alisema Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera raia wa DRC.

Kocha wa Mwadui, Mnyarwanda Ally Bizimungu alisema kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike anatakiwa kuwaeleza wachezaji wake namna ya kucheza kwa ushirikiano katika mechi zote mbili.

“Kucheza mechi mbili ndani ya siku nne si kazi rahisi muhimu ni wachezaji kuwa na nidhamu ya mchezo kwa sababu hakutakuwa na muda wa mazoezi, yaani mechi ya kwanza ndio itakuwa mazoezi ya mechi ya pili.

“Katika mechi na Uganda wachezaji walicheza zaidi nyuma, upande wa washambuliaji walibaki wachache hatua iliyochangia kutopata ushindi, lakini naamini Taifa Stars ina nafasi nzuri ya kushinda kama wachezaji watajituma,”alisema Bizimungu.

Kocha wa Stand United Amas Niyongabo alisema kutokana na ufinyu wa muda baina ya mechi hizo wachezaji wanatakiwa kuweka mbele moyo wa uzalendo zaidi ili kushinda mechi hizo.

“Ligi Kuu inawaandaa kuzoea mazingira ya mechi hizo mbili dhidi ya Cape Verde, hata hapa mechi zimefuatana sana. Muhimu ni kujituma, kufuata maelekezo ya kocha na kuweka moyo wa kizalendo naamini watashinda,” alisema Niyongabo.

Kocha wa Biashara United, Mrundi Hitimana Thierry alisema ingawa muda ni mfupi baina ya mechi hizo, lakini endapo wachezaji watajituma watashinda mechi zote mbili.

“Mechi na Uganda wachezaji walijitahidi sana, lakini wanatakiwa kuhakikisha wanatumia vizuri nafasi wanazopata. Wasizembee kwa sababu nafasi ya goli haijirudii

“Faida aliyonayo kocha wa Taifa Stars ana wachezaji watakaokuwa fiti kwa sababu wanacheza mechi za ligi mfululizo wakiongezewa nguvu na wanaocheza nje ya nchi sidhani kama kutakuwa na tatizo. Muhimu ahakikishe mechi zote za nyumbani anaondoka na pointi tatu,”alisema Thierry.

Hivi karibuni TFF ilitangaza mkakati wa kuhakikisha unapatikana usafiri wa ndege ya kukodi ambao utaiwahisha na kuirudisha timu mapema itakapocheza dhidi ya Cape Verde ugenini.

Chanzo: mwananchi.co.tz