Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha Simba, Yanga watambiana

F9b6ea5478b79ec1916c23437eaf1682 Makocha Simba, Yanga watambiana

Thu, 22 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAKOCHA wa klabu za Simba na Yanga, wametambiana kila mmoja akijitapa kuibuka na ushindi katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA, utakaopigwa Jumapili ijayo Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Simba na Yanga zitakutana kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa fainali ya michuano hiyo, ambayo bingwa wake hupata nafasi ya kuliwakilisha taifa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Caf.

Akizungumza na gazeti hili kuelekea kwenye mchezo huo wa fainali Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes alisema yeye pamoja na wachezji wake wameupa uzito mkubwa mchezo huo sababu wanataka kutetea taji hilo na kulipa kisasi cha kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga kwenye ligi.

Alisema kikosi chake kipo katika hali nzuri ikiwepo afya njema kwa wachezaji wake na anachokifanya kwenye uwanja wa mazoezi hivi sasa ni kuwaelekeza vijana wake mbinu muhimu zitakazowapa urahisi wa kushinda mchezo huo.

“Najua utakuwa mchezo mgumu na wenye ushindani kwa pande zote mbili, lakini Simba tumedhamiria kushinda mchezo huu kwa kucheza soka safi na idadi kubwa ya mabao kutokana na mbinu, ambazo nawapa wachezaji wangu kitu cha msingi naomba waamuzi wawe makini ,” alisema Gomes.

Kocha huyo alisema katika mchezo huo amepanga kutumia mifumo tofauti na ile ambayo wamekuwa wakiitumia kwenye mechi za ligi, lengo ni kuwachanganya wapinzani wao na kupata urahisi wa kupata ushindi, ambao kwao ndio kitu muhimu na amefurahi kuona mshambuliaji wake Bernard Morrison kurejea kwa wakati akitokea Ghana alikokwenda kwa matatizo ya kifamilia.

Kwaupande wake kocha wa makipa wa Yanga, Razak Siwa alisema maandalizi kwa ajili ya mchezo huo wa fainali yanaendelea vizuri na wachezaji wao wameonesha shauku kubwa ya kuendeleza furaha waliyoipata Julai 3 kwa kuifunga Simba.

Siwa alisema yeye na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi wamekuwa wakiendelea na matumaini makubwa kutokana na kile wanachowafundisha wachezaji wao kuelekea mchezo huo kuona wamekishika mapema na kukifanyia kazi vizuri.

Alisema pamoja na Simba kuwa ni timu bora, lakini wao hilo haliwatishi sababu hata Yanga siyo timu ndogo na wameshalithibitisha hilo licha ya kukosa ubingwa lakini taji la Kombe la FA anaamini litakwenda Jangwani.

“Hatutaki kuwa na maneno mengi sababu hiki ni kipindi cha maandalizi ya mechi, tusubiri dakika 90 za uwanjani ndio zitathibitisha nani bora kuliko mwingine kitu cha msingi kwetu ni wachezaji wetu kufahamu umuhimu wa mchezo wenyewe na malengo tuliyojiwekea kwenye mechi hiyo,” alisema Siwa.

Kocha huyo alisema wapo tayari kwa mchezo huo na wamejipanga kutoa burudani safi kwa mashabiki wao wa Kigoma, ambao wamedhamiria kuwaachia furaha.

Chanzo: www.habarileo.co.tz