Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makocha 10 wa kigeni watakaotoana jasho Ligi Kuu 2021/2022

TPL 20211 Vita vya makocha 10 wa kigeni Ligi Kuu 2021/22

Mon, 6 Sep 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

RATIBA ya Ligi Kuu inatarajiwa kutoka wiki Ijayo kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo. Na baada ya hapo kila timu itajua itaanza na nani. Hakika itakuwa ni vita ya timu 16 kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 2021/ 22.

Inatarajiwa kuwa Ligi Kuu ya aina yake kutokana na udhamini mkubwa, ikiwamo kupungua kwa idadi ya timu. Msimu uliopita zilikuwa timu 18, lakini msimu ujao zitakuwa 16. Tumeona klabu zikijizatiti kusajili wachezaji bora. Hata hivyo, kusajili wachezaji bora ni jambo moja na kutengeneza timu ni jambo lingine.

Kazi hiyo ni ya benchi la ufundi, hivi sasa makocha wako kwenye pilikapilika ya kuvisuka vikosi vyao kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano. Makocha ndiyo mhimili wa timu nadiyo wanaotengeneza mifumo mbalimbali na kuvifanya vikosi vyao kuwa imara. Hawa ni makocha watakaoonyeshana kazi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu 2021/22...

#1. Didier Gomes - Simba (Mfaransa)

Ni kocha wa mabingwa wa nchi. Raia huyo wa Ufaransa ameipa Simba ubingwa msimu huu, ingawa hakuanza nayo.

Aliichukua timu hiyo kutoka kwa kocha Mbelgiji Sven Vandenbroeck. Hakubadili gea, aliendelea nayo na moto ule ule, na si kwenye Ligi Kuu tu, hata Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa sasa ameanza nayo timu tangu mwanzo, amesajili mwenyewe, hata hivyo pamoja na kupoteza wachezaji Luis Miquissone na Clatous chama, bado anatarajia kuleta upinzani mkali kwa timu zingine.

#2. Nasreddine Nabi - Yanga (Mtunisia)

Aliianza kuifundisha Yanga, baada ya kutimuliwa kwa kocha raia wa Burundi, Cedrick Kaze. Kocha huyo raia wa Tunisia, kwa muda mfupi alioingia msimu uliopita, aliifanya Yanga kushinda mechi nyingi mfululizo.

Tatizo lilikuwa ilishatoka sare nyingi, hivyo kushindwa kabisa kuikuta Simba kileleni. Msimu huu amehusika kwenye usajili, anaiandaa timu tangu mwanzo mwenyewe akitarajia kwenda kuipa Simba wakati mgumu kutetea taji lake.

#3. George Lwandamina - Azam (Mzambia)

Angalau sasa Azam FC imetulia baada ya ujio wa kocha huyu wa zamani wa Yanga. Baada ya kuvurunda kwenye mechi kadhaa za msimu uliopita, viongozi wa Azam walimleta kocha huyo ambaye alianza kusajili wachezaji anaowahitaji kipindi cha dirisha dogo. Timu ikakaa vizuri.

Sasa amesajili na anaitengeneza timu yake kwa ajili ya msimu ujao. Ni moja kati ya timu inayotarajiwa kuleta upinzani na hata kutwaa ubingwa msimu ujao.

#4. Patrick Okumu - Biashara United (Mkenya)

Okumu ni mmoja wa makocha waliojipatia sifa kwa muda mfupi tu baada ya kujiunga na Biashara United. Alichukuliwa baada ya kocha Francis Baraza kwenda Kagera Sugar.

Alishikilia uzi ule ule wa Mkenya mwenzake, na kuipeleka Biashara United kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Msimu huu anatakiwa kuthibitisha kuwa hakutembelea nyota ya mwenzake.

#5. Melis Melo - Coastal Union (Marekani)

Coastal Union wamemchukua kocha kutoka Marekani, ambaye amezifundisha timu kadhaa nchini Kenya. Melis Melo, ndiye kocha mkuu wa sasa wa timu hiyo akishika nafasi ya Juma Mgunda, ambaye amekuwa Mkurugenzi wa Ufundi. Wengi wanataka kumuona kocha huyo mpya nini atakifanya kwenye timu hiyo.

#6. Etienne Ndayiragije - Geita Gold (Burundi)

Huyu ni kocha mzoefu na maarufu nchini, aliwahi kuwa kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars. Alizifundisha pia timu za Mbao na KMC. Itakumbukwa aliwahi kuifanya Mbao FC kutoka kuwa timu ndogo na kuwa tishio.

Sasa ataiongoza Geita Gold iliyopanda daraja msimu huu. Ila anatakiwa kukumbuka kuwa rekodi inaonyesha kuwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kila msimu. Timu moja iliyopanda daraja ni lazima ishuke.

#7. Francis Baraza - Kagera Sugar (Mkenya)

Mkenya huyu aliifanya Biashara United kuwa moja ya timu tishio tangu ipande Ligi Kuu. Aliondoka kwenye timu hiyo na kwenda Kagera Sugar kwa ajili ya kazi moja tu. Kuinusuru isishuke daraja. Na kweli alifanikiwa. Kwa sasa anaiandaa kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu. Anatarajia kuleta ushindani mkubwa kwa klabu zingine.

#8. Mathias Lule - Mbeya City (Mganda)

Kocha huyu Mganda msimu uliopita aliinusuru Mbeya City kushuka daraja. Ndiyo maana hadi leo yupo kwenye klabu hiyo. Anatarajia kuiongoza tena timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao. Ni kocha mwenye mbinu na mwenye uwezo wa kusoma mfumo wa timu pinzania, akaufanyia kazi.

#9. Haruna Hererimana - Mbeya Kwanza (Mrundi)

Ni kocha raia wa Burundi, lakini si mgeni sana kwenye soka la Tanzania. Aliwahi kuzifundisha timu za Lipuli na KMC. Amepewa mikoba ya kuifundisha Mbeya Kwanza ambayo itacheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara.

#10. Thierry Hitimana - Mtibwa Sugar (Mnyarwanda)

Aliwahi kuifundisha Biashara United, halafu akatimkia Namungo, akaenda Mtibwa Sugar, lakini hakukaa sana na sasa amerudishwa Mtibwa Sugar. Ni mmoja wa makocha wazoefu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo anategemewa kutoa upinzani mkubwa kwa makocha wenzake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live