Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makenji, Gulam wang'ara maandalizi ya Olimpiki Paris 2024

Imani Pic Makenji, Gulam wang'ara maandalizi ya Olimpiki Paris 2024

Mon, 19 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Nyota wa Zanzibar Winfrida Makenji na Ally Gulam wameibuka mabingwa wa mbio za mita 100 na 200 kwenye mashindano maalumu ya maandalizi ya Olimpiki 2024.

Mashindano hayo yanashirikisha timu za judo, ngumi na riadha yanafanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa na ule wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam yakiratibiwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Kwenye riadha, Makenji na Gulam wameibuka mabingwa wa mbio za mita 100 na 200 kwa wanaume na wanawake.

Kwenye mita 100, Makenji alitumia sekunde 11:80 wakati Gulam akitumia sekunde 10:40.

Katika mbio ya mita 200, Makenji alitumia sekunde 23:80 na Gulam sekunde 21:07.

"Umekuwa ni mwanzo mzuri kwangu na hatua nzuri ya maandalizi kuelekea kwenye Olimpiki, kama kungekuwa na utaratibu huu muda mrefu, bila shaka tungekuwa na rekodi bora kwenye Olimpiki," amesema Gulam nyota wa timu ya taifa wa mbio fupi.

Kwenye kurusha kisahani, Mohammed Ibrahim aliibuka kinara akirusha mita 39 na sentimita 49.

Katika mbio ya mita 1500, Salma Charles Samwel aliibuka kinara akitumia dakika 04:32:09 wakati kwa wanaume, Epimack Boniface aliyetumia dakika 3:46:38 akiibuka kinara.

Salma tena aliibuka shujaa wa mita 800 akitumia dakika 2:13:69 wakati kwa wanaume Seleman Khamis aliibuka kinara akitumia dakika 1:54:20.

Twahir Haji Makame alikuwa kinara wa mbio ya mita 400 akitumia dakika 48:50 wakati Jane Maige akitwaa ubingwa kwa wanawake akitumia dakika 56:62.

Joseph Panga aliibuka shujaa wa mita 5000 akitumia dakika 13:59:60 akiwaacha kwa mbali washindani wenzake, Faraja Lazaro, Marco Monko na Dickson Francis.

Kwenye kurusha mkuki, Dau Dahala aliibuka kinara akirusha mita 58:12.

Kwenye ngumi, Rashid Mrema aliibuka kinara kwenye uzani wa feather baada ya kumchapa Yusuph Abdallah.

Ibrahim Maulid aliibuka kinara kwenye uzani wa light baada ya kumchapa Mohammed Hamadi wakati Joseph Philipo akimchapa David Charles na kuibuka kinara kwenye uzani wa light middle.

Kwenye uzani wa juu mwepesi, Yusuph Changalawe alimchapa Hoza Abdallah katika fainali.

Makamu wa rais wa TOC, Henry Tandau amesema baada ya mashindano hayo, wale wote watakaofikia viwango wataanza programu maalumu ya mazoezi kujiandaa kutafuta viwango vya Olimpiki.

"Tutakuwa na programu mbalimbali za mazoezi na mashindano ya kufuzu, hivyo mapema mwakani watakaokuwa wamechaguliwa," amesema.

Awali TOC iliweka viwango vyake vya kufuzu ambavyo viko juu ya vile vilivyotolewa na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kwa ajili ya kufuzu kushiriki michezo hiyo ambayo Tanzania ina historia ya kutwaa medali mbili za fedha tangu Uhuru.

 "Lengo la maandalizi haya ni kujiweka tayari kwa ajili ya michezo ijayo ya Olimpiki, tunahitaji medali, hivyo lazima tujiandae mapema," amesema Tandau.

Chanzo: Mwanaspoti