Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makambo atikisa Rwanda

14462 Pic+makambo TanzaniaWeb

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigali. Wakati Yanga leo inateremka uwanjani katika mchezo wa kukamilisha ratiba dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, gumzo kubwa ni mshambuliaji wa kigeni Herieter Makambo.

Mshambuliaji huyo raia wa DR Congo, ameifungia Yanga mabao mawili katika mechi mbili alizocheza ukiwemo mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria na mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar.

Makambo anaonekana mkombozi wa Yanga katika safu ya ushambuliaji baada ya kucheza kwa kiwango bora katika nafasi aliyokuwa akicheza Donald Ngoma aliyejiunga na Azam.

Akizungumza mjini hapa jana, kocha mpya wa Rayon, Mbrazili Roberto Goncalves alisema ametoa maelekezo kwa mabeki wake kutompa nafasi Makambo.

Alisema safu ya ulinzi inatakiwa kumpa ulinzi mkali Makambo aliyedai kuona makali yake kupitia mkanda wa mechi ya Yanga na USM Alger.

“Mabeki wetu wanatakiwa kutulia vizuri nimeangalia mechi zao mbili hii ya mwisho nimeona kuna mshambuliaji ameongezeka na ana akili na nguvu tutahitaji kuwa naye makini,” alisema kocha huyo.

Wakati Goncalves akionekana kuigwaya Yanga, kocha wa Yanga Mwinyi Zahera ametamka kuwa watajilipua kupata ushindi ugenini.

Zahera alisema Yanga itaendeleza moto iliyouanzisha katika mchezo walioshinda mabao 2-1 dhidi ya USM Alger na ule waliopata ushindi kama huo dhidi ya Mtibwa Sugar.

Yanga iliyotua jijini hapa jana alfajiri itaingia uwanjani leo na akili moja tu ya kulinda heshima kwa kusaka ushindi au sare na endapo itashinda itakuwa imejiondoa katika nafasi ya kushika mkia kwenye kundi lao.

“Tumejiandaa vizuri hatuna tutakachopoteza tutakwenda kucheza soka letu tukitumia ubora wetu ambao tunao kwa sasa.

“Presha itakuwa kwa wapinzani wetu, wanahitaji nafasi sisi tutacheza kwa kutulia, nafikiri hilo ndiyo muhimu kwetu,” alisema Zahera ambaye hatakaa kwenye benchi la ufundi kwa kuwa hana kibali cha kufanya kazi Tanzania.

Yanga haina uwezo wa kushika nafasi mbili za juu ambazo zitaipa tiketi ya kutinga robo fainali na ikishinda itakuwa imewatibulia wapinzani wao ambao wanahitaji ushindi.

Yanga itacheza mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi mbili muhimu dhidi ya USM Alger na Mtibwa ambapo timu hiyo iliwapa raha mashabiki wake kwa kucheza soka maridadi.

Yanga ilifanya mazoezi ya mwisho jana jioni Uwanja wa Nyamirambo uliopo nje kidogo ya Jiji la Kigali tayari kwa mchezo huo.

Rayon inautumia Nyamirambo kama uwanja wa nyumbani huku ikipenda zaidi kutumia nyasi bandia ambazo zitaifanya Yanga kubadilika kutokana na kutumia viwanja vingi vyenye nyasi asilia kwenye Ligi Kuu.

Yanga inatarajiwa kukosa huduma ya wachezaji mahiri nyota wa kiungo Thabani Kamusoko na Papy Tshishimbi waliobaki Dar es Salaam kwa matatizo binafsi.

Pia Said Juma ‘Makapu’ atakosa mchezo huo baada ya kufiwa na mama yake mzazi, Juma Abdul akiwa majeruhi na Mwinyi Haji amekwenda Zanzibar kwa matatizo ya kifamilia.

Zahera raia wa DR Kongo, amewatoa hofu mashabiki wa Yanga kuhusu kukosekana kwa wachezaji hao muhimu.

Kwa upande wake Goncalves, alisema atakuwa na kazi ngumu kupata ushindi kwa kuwa atakosa huduma ya wachezaji tisa akiwemo kipa wake nguli Ndayimishiye Jean aliyefukuzwa kwa utovu wa nidhamu.

Pia atawakosa nyota watatu Kassim Ndayinga, Yannick Mukunzi na Mcameroon Christ Mbondi wakati Pierre Kwizera na Nahimana Shasir mikataba yao imemalizika.

Goncalves atamkosa mshambuliaji Shabani Hussein ‘Tshabalala’ aliyetimka Rayon na kujiunga na Baroka ya Afrika Kusini.

Pia beki raia wa Rwanda Faustin Usengimana amekwenda kucheza soka ya kulipwa nchini Qatar na Ismaila Diarra ametimkia Algeria.

Kocha huyo anatarajia kuwatumia wachezaji wanane waliokuwa wakisugua benchi kucheza mchezo wa leo kujaza nafasi za nyota hao.

“Yanga sio timu nyepesi, hakuna aliyetarajia kusikia wangeifunga USM Alger. Huu ni mchezo wa soka, siku zote umekuwa na matokeo ya kushtukiza hilo ni fundisho kwetu tunatakiwa kuwa makini,” alisema kocha huyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz