Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makambo aipeleka Lyon shimoni

51261 MAKAMBO+PIC

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Mabao mawili yaliyofungwa na mshambuliaji Heritier Makambo yameipaisha Yanga, lakini yameididimiza African Lyon katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Makambo amefikisha mabao 14 sawa na mshambuliaji nyota wa Simba, Meddie Kagere. Salum Aiyee wa Mwadui ya Shinyanga anaongoza kwa kufunga mabao 16.

Yanga jana ikiwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ilipoza machungu ya mashabiki wake baada ya kuilaza African Lyon mabao 2-0.

Kabla ya kumenyana na African Lyon, Yanga ililazimisha sare ya bao 1-1 na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara ambapo Amissi Tambwe alikosa penalti.

Matokeo hayo yamezidi kuiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kuwania ubingwa baada ya kufikisha pointi 71 katika mechi 30 ilizocheza.

Hata hivyo, matokeo hayo ni mabaya kwa African Lyon kwa kuwa yanazidi kuiweka katika nafasi finyu ya kubaki katika Ligi Kuu msimu ujao kwa kuwa bado inaburuza mkia ikiwa na pointi 22 katika mechi 33.

Wakati Yanga ikiwa imebakiwa na mechi nane kumaliza ligi, Simba ina mechi 11 za viporo. Timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, imecheza mechi 22 tu.

Mchezo wa jana

Dakika ya tano Makambo alifunga bao la kwanza kwa kiki baada ya kuvunja mtego wa kuotea na kumchambua kipa Douglas Kisembo.

Yanga ilipata bao la pili lililofungwa tena na Makambo dakika ya 30 kwa mpira wa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Haruna Moshi ‘Boban’.

Kipa wa African Lyon alifanya kazi ya ziada kwa kuokoa kiki ya Pius Buswita aliyoifumua dakika ya 43 baada ya kuwatoka mabeki wa African Lyon. Pia, Makambo alikosa bao dakika ya 80 kabla ya Papy Tshishimbi kurudia makosa kama hayo baada ya kupata pasi ya Mrisho Ngassa.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema licha ya kupata ushindi, lakini wachezaji wake walicheza katika mazingira magumu kutokana na uchovu. Zahera alisema Yanga inatembea umbali mrefu kucheza mechi zake kulinganisha na Simba aliyodai ina mechi nyingi za viporo.

Kocha wa Africa Lyon, Salvatory Edward ambaye ni nahodha wa zamani wa Yanga, alisema licha ya kufungwa lakini wana imani ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao kwa kuwa mechi bado zipo za kutosha ambazo wanaweza kushinda.

Yanga: Klausi Kindoki, Juma Abdul, Gadiel Michael, Kelvin Yondani/Said Makapu, Andrew Vincent, Feisal Salum, Mrisho Ngassa/Rafael Daud, Haruna Moshi/Thabani Kamusoko, Heritier Makambo, Papy Tshishimbi na Pius Buswita.

African Lyon: Douglas Kisembo, Khafan Mbarouk, Kassim Simbaulanga, Baraka Jafari, Daud Mbweni, Jabir Aziz, Said Mtikila, Awadh Juma, Benedictor Jacob/Adili Nassor, Kassim Mdoe na Hamisi Thabit.



Chanzo: mwananchi.co.tz