Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magdalena avunja rekodi ya Taifa riadha

96685 Magdalena+pic Magdalena avunja rekodi ya Taifa riadha

Mon, 24 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwanariadha nyota wa Tanzania, Magdalena Shauri amevunja rekodi ya Tanzania ya nusu marathoni katika mashindano ya Ras Al Khaimah Half Marathon yaliyofanyika Dubai jana.

Magdalena ameshika nafasi ya saba kwa kutumia muda wa saa 1:06:16 na kuvunja rekodi iliyodumu miaka 20 ya mwanariadha nyota wa zamani, Resistuta Joseph aliyeiweka mjini Malmo, Sweden Aprili 12, 2000 alipotumia 1:07:59.

Katika mashindano hayo, mwanariadha wa Ethiopia, Abadel Brihane alishika nafasi ya kwanza kwa kutumia muda wa saa 1:04:31 wakati nafasi ya pili ilichukuliwa na mwanariadha wa Kenya, Brigid Kosgei kwa kutumia 1:04:49 na tatu Rosemary Monicah wa Kenya aliweka muda wa 1:05:34.

Mwanariadha mwingine wa Kenya, Eveline Chirchir alishika nafasi ya nne kwa kutumia muda wa saa 1:06:01 na Joan Chelimo vilevile wa Kenya aliyemaliza katika nafasi ya tano kwa kutumia muda wa 1:06:16. Nafasi ya sita ilichukuliwa na Yalemzerf Densa wa Ethiopia kwa muda wa 1:06:35.

Wanariadha wengine katika nafasi 10 bora mbali na Magdalena ni Vivian Jerono Kiplagat wa Kenya aliyetumia muda wa 1:06:38, Degitu Azimeraw (Ethiopia) 1:07:02 na Fancy Chemutai wa Kenya aliyetumia muda wa 1:08:02.

Kocha wa Madgalena, Thomas Tlanka alisema matokeo hayo ni mazuri kwa mwanariadha huyo ambaye pia anatafuta tiketi ya kufuzu mashindano ya Olimpiki.

Pia Soma

Advertisement
Tlanka alisema Magdalena alifanya mazoezi mazuri kujiandaa na mbio hizo na anaamini atafanya vizuri mwezi Aprili katika mashindano ya kufuzu ya Olimpiki USA.

“Kwa kweli nimefarijika kwa matokeo ya Magdalena, nampa hongera mashindano yalikuwa magumu na alishindana na wanariadha wenye rekodi nzuri duniani, matokeo yake yanaakisi kwenye kutafuta tiketi ya mashindano ya Olimpiki atafanya vyema,” alisema Tlanka.

Alisema kuna maendeleo makubwa kwa mwanariadha huyo na anaamini kama ataendelea na bidii aliyoionyesha atafika mbali na Tanzania itatwaa medali za dunia. “Ameweza kuvunja rekodi ya taifa iliyodumu miaka 20 si mchezo naamini anaweza kufanya maajabu katika kufuzu na hata mashindano ya Olimpiki tunatakiwa kujiandaa vyema muda wa mazoezi kabla ya kushindana Marekani bado upo,” alisema.

Kwa upande wa wanaume, Mwanariadha mwingine wa Tanzania, Gabriel Geay alimaliza katika nafasi saba. Geay alitumia saa 1:00:09 ambapo Mkenya Kibiwott Kandia alishinda kwa kutumia 58:58.

Nafasi ya pili ilikwenda kwa Mkenya mwingine, Alexander Mutiso aliyetumia 59:16 huku Mule Wasihun wa Ethiopia akishinda nafasi ya tatu kwa kutumia 59:47.

Wakenya waliendelea kutamba katika mbio hizo ambapo Alfred Barkach alishika nafasi ya nne kwa muda 59:49 huku Vincent Kibor akishika nafasi ya tano kwa muda 59:51, nafasi ya sita ilikwenda kwa Leonard Barsoton wa Kenya akitumia 1:00:02.

Wengine katika 10 bora ni Joseph Karanja (Kenya 1:00:13), Maxwell Kortek (Kenya 1:00:20) na Abdallah Kibet wa Uganda aliyetumia muda 1:00:35.

“Geay pia amefanya vizuri sana, nampongeza kwa matokeo pamoja na ukweli kuwa mashindano yalikuwa magumu,” alisema Tlanka.

Chanzo: mwananchi.co.tz