Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Macho yote kwa Kagere, Bocco pale Algeria leo

45807 Pic+kagere Macho yote kwa Kagere, Bocco pale Algeria leo

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Macho na masikio ya mashabiki wa Simba yatakuwa yakishuhudia ubora wa safu ya ushambuliaji inayoongozwa na nahodha wa timu hiyo, John Bocco na Meddie Kagere kuibeba timu hiyo leo kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura.

Simba wataingia kwenye mchezo wa leo utakaochezwa Stade du 20 Août 1955 (Bechar) kuanzia saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki wakiwa na kumbukumbu ya kuwafunga wenyeji wao, JS Saoura kwa mabao 3-0 jijini Dar es Salaam.

Katika michezo sita iliyopita ya hivi karibuni ya Simba, ukiwemo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao waliifunga Al Ahly, Kagere na Bocco wamechangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa matokeo ya ushindi kwenye michezo sita mfululizo.

Pacha ya washambuliaji hao, ina jumla ya mabao 10 huku kila mmoja akifunga matano kwenye michezo hiyo sita ambayo ni dhidi ya Al Ahly, Yanga, African Lyon, Azam, Lipuli na Stand United.

Februari 12, Simba walikuwa nyumbani uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam kucheza dhidi ya mabingwa wa kihistoria kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly na waliitandika kwa bao 1-0 lililofungwa na Kagere.

Katika mchezo uliofuata Februari 16, Kagere alipeleka tena majonzi Jangwani kwa kufunga bao pekee la Simba lililoifanya kukusanya pointi tatu muhimu kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania.

Bocco akajibu mapigo kwa Kagere, Februari 19 kwenye mchezo wa Ligi ambapo alifunga mara mbili mbele ya African Lyon ambao walikubali kipigo nyumbani kutoka kwa Simba cha mabao 3-0.

Washambuliaji hao kwa pamoja waliifanya Simba kutoka kifuambele Februari 22 mbele ya Azam kwa kuitandika mabao 3-0 yaliyosababishwa kutimuliwa kwa kocha aliyekuwa akiinoa timu hiyo, Mholanzi Hans van der Pluijm.Kagere alifunga mabao mawili huku Bocco akitupia moja.

Februari 26, njaa ya safu ya ushambuliaji ya Simba iliendelea kwenye mchezo dhidi ya Lipuli, Iringa na safari hiyo alifunga Bocco pekee bao moja huku mengine mawili yakifunga na kiungo Mzambia Cletous Chama.

Katika mchezo wa mwisho wa Ligi dhidi ya Stand United uliochezwa uwanja wa Kambarage aliyeibeba Simba alikuwa ni Bocco aliyefunga mara mbili mkoani Shinyanga.

Pamoja na makali ya safu ya ushambuliaji ya Simba ambayo itamkosa Mganda Emmanuel Okwi ambaye ni mgonjwa, wanafaida kwenye kikosi chao ya kuimarika safu yao ya ulinzi ambayo ilitandikwa mabao 10 ndani ya michezo miwili mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya AS Vital, Januari 19 na Al Ahly, Februari 2 yote ikiwa ugenini.

Kingine kinachoweza kuibeba Simba kwenye mchezo wa leo ni udhaifu wa JS Saoura kwenye safu yao ya ulinzi.

JS Saoura inajumla ya mabao manane kwenye michezo yake 10 iliyopita huku ukuta wao ukionekana kuwa na dhaifu na kuruhusu mabao karibu kwenye kila mchezo.

Ndani ya michezo hiyo wamefungwa mabao 11 na idadi hiyo ya mabao mengi wamefungwa kipindi cha kwanza.

Mbali na kuwa na madhaifu hayo, JS Saoura ambayo inanyota wa Kitanzania, Thomas Ulimwengu, katika rekodi zao zinaonyesha kuwa ni timu hatari kipindi cha pili kutokana na kufunga kwao mabao mengi zaidi kwenye kipindi hicho.

Katika mabao manane waliyofunga kwenye michezo yao 10 ya hivi karibuni ni bao moja pekee ambalo walilifunga kipindi cha kwanza tena ilikuwa Januari 22 kwenye mchezo wa Ligi dhidi ya Oran na bao hilo lilifungwa na miongoni mwa wachezaji hatari kwenye kikosi chao, Yahia Cherif.

Pluijm ampa tano Aussems

Kocha wa zamani wa Azam, Hans van der Pluijm alisema jana kuwa kwake Simba ndio wenye nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo kama wataenda na mbinu za kushambulia huku wakizua kwa pamoja.

“Kama awamu hii watakuwa vizuri kisaikolojia na wakicheza soka lao la kawaida wanaweza kushinda, Aussems anaweza kuifikisha Simba mbali.”



Chanzo: mwananchi.co.tz