Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabosi Man United wamvuruga Mourinho

9260 PIC+MABOS TanzaniaWeb

Wed, 1 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jose Mourinho amegeuka mbogo muda mfupi baada ya Manchester United kutunguliwa mabao 4-1.

Mourinho alisema hafurahishwi na mwenendo wa vigogo wa klabu hiyo ya Old Trafford kuhusu mchakato wa usajili wa majira ya kiangazi.

Kocha huyo alitoa kauli hiyo muda mfupi, baada ya Man United kucharazwa idadi kubwa ya mabao na watani wao wa jadi Liverpool katika mchezo wa kirafiki juzi usiku.

“Nilitaka wachezaji zaidi ya wawili hodari katika usajili wa majira ya kiangazi, tayari nina orodha ya majina ya nyota watano,” alisema Mourinho.

Mourinho alisema mkakati wake ni kujenga timu imara itakayoleta ushindani mkali katika mashindano ya Ligi Kuu England msimu ujao.

Kocha huyo alisema amechanganyikiwa kwasababu hajui hatima ya wachezaji anaotaka wakati dirisha la usajili likikaribia kufungwa Agosti 9, mwaka huu.

Alisema hana uhakika wa kupata wachezaji imara anaotaka katika usajili hata kama atapata fedha kutoka kwa vigogo hao kutokana na muda kupata mfupi.

Miongoni mwa wachezaji anaowataka ni shujaa wa Kombe la Dunia anayetamba katika kikosi cha Leicester City na England, Harry Maguire.

Mourinho anataka beki wa kati ili kuimarisha safu ya ulinzi baada ya ukuta wa Man United kuyumba msimu uliopita.

“Ningependa kusajili zaidi ya wachezaji wawili. Sina uhakika kama malengo yangu yatatimia, labda naweza kupata mmoja,” alisema Mourinho.

Kocha huyo raia wa Ureno, alisema alikabidhi majina ya wachezaji watano kwa mabosi wa klabu hiyo lakini hakuna kinachoendelea.

Chanzo: mwananchi.co.tz