Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabondia wanaoongoza kwa vituko ulingoni hawa hapa

23481 Ndondi+pic TanzaniaWeb

Mon, 22 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Conor Mac Gregory alipopigika kwa mpinzani wake Khabib Nurmagomedov, siku 15 zilizopita, ukumbi ulinywea, lilikuwa pambano la simanzi kwa ‘team’ Mac Gregory wakiongozwa na msanii nguli, Drake, hawakutarajia kilichotokea.

Mac Gregory mkali wa Kick Boxing (ngumi na mateke) alipata umaarufu kwenye ngumi alipozichapa na Floyd Mayweather mwaka jana, pambano lake la kwanza lililoingiza fedha nyingi japo alipigwa.

Pambano la hivi karibuni dhidi ya Nurmagomedov lilimuathiri Mac Gregory, lakini halikuishiwa vituko, mpinzani wake alimkejeli Mac Gregory, kitendo kilichowakera hadi mashabiki na kuzua tafrani, huku bingwa akishindwa kuvalishwa mkanda kwa kujitakia mwenyewe kutokana na mbwembwe zake.

Hiyo ni Ulaya, ngumi za kibongo nazo hazikosi vituko, mchezo huo haujawahi kumalizika pasipo kituko cha aina yoyote ile, iwe kwa mashabiki, mwamuzi, makocha, majaji na hata mabondia wenyewe na hivi ni vituko vilivyopitiliza vilivyofanywa na mabondia wa bongo ulingoni.

Bondia anyukwa, atimua mbio ulingoni

Sio ‘muvi’, hii imetokea bongo, bondia Hussein Gogosi alipoamua kutumia kipaji cha nguli wa mbio fupi duniani, Usain Bolt kusepa ulingoni.

Pambano hilo lilipigwa Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaa, ambapo Gogosi alikuwa akizichapa na Adam Ngange.

Raundi mbili za awali, Gogosi alimtembezea ngumi za maana mpinzani wake aliyepasuka na kuanza kuvuja damu huku Gogosi akiamini atashinda kwa TKO, lakini ikawa ndivyo sivyo.

Mpinzani wake alikomaa na ilipoanza raundi ya tatu, Ngange alicheza kama chui aliyejeruhiwa, alimchakaza makonde mfululizo mpinzani wake pasipo majibu, licha ya kwamba alikuwa amelowa damu.

Gogosi kuona anaelemewa akaona isiwe taabu, baada ya kupata mwanya alitoka mbio ukumbini akidai hawezi kuendelea na pambano kwa kuwa mpinzani wake anavuja damu sana na kumpa ushindi wa TKO raundi ya tatu Ngange.

“Lilikuwa tukio la kushangaza kwa kweli, kwani hakuna aliyetarajia kama bondia yule alikuwa akitafuta upenyo ili akimbie,” alisema promota wa pambano hilo, Said Mbelwa.

Adai glovu za mpinzani zina pilipili

Kituko kingine kilitokea kwenye pambano kati ya Shedrack Juma na Said Chino lililopigwa CCM Mwinjuma, Mwananyamala, baada ya bondia kuelemewa na kipigo alidai glovu za mpinzani wake zina pilipili.

Chino aligoma kuendelea akidai glovu za mpinzani wake zimepakwa pilipili ambayo kila akipigwa ngumi inamuingia machoni.

Baada ya madai hayo, mwamuzi ilibidi asimamishe pambano na hakukuwa na ushahidi mwingine zaidi ya Shedrack kuvuliwa glovu hizo ili mabondia wote wawili na makocha wao pamoja na ‘official’ mmoja kuanza kuzilamba ili kuthibitisha tuhuma hizo za Chino.

Hata hivyo, wote waliolamba glovu hizo isipokuwa Chino, hakuna aliyesikia ladha ya pilipili, ingawa pamoja na matokeo hayo Chino aligoma kuendelea na pambano na mwamuzi kulazimika kumaliza mchezo bila bingwa kupatikana.

“Zile glovu zilikuwa zangu, mimi ndiye nilitoka nazo nyumbani, kwa kuwa nilikuwa promota wa pambano hilo, kuna vitu ilikuwa lazima nihakikishe vinakuwepo ulingoni,” alisema Rajabu Mhamila ‘Super D’.

Alisema chama kilichokuwa kikisimamia pambano hilo, kiliondoka na glovu kwa uchunguzi zaidi na alirejeshewa baada ya siku tano huku ushahidi wa kuwa zilikuwa na pilipili ukikosekana kila zilipochunguzwa.

Mwamuzi amtaja mshindi aliyeamuliwa na mashabiki

Hii ilimtokea Japhet Kaseba ambaye alizichapa na Mada Maugo kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es Salaam, katika pambano hilo, mashabiki ndiyo waliamua bingwa.

Ilikuwa hivi, katikati ya pambano, Maugo alimchezea faulo za kutosha tu Kaseba ambaye alikasirika na yeye kuamua kucheza ngumi za mtaani akimkata mtama Maugo kabla ya mashabiki wa Kaseba kuingilia kati wakidai Maugo anabebwa, hivyo bora wao waondoke ulingoni.

Pambano likiwa limesimama, msaidizi wa Kaseba ulingoni (second) alimvua glovu bondia wake, kabla ya hatma ya pambano kujulikana huku Maugo akiwa bado amevaa glovu zake kuashiria bado yuko mchezoni.

Mwamuzi, John Chagu aliamua kuwauliza mashabiki waliokuwa wamefurika ukumbini hao kuwa nao waseme ni bondia yupi kati ya Maugo na Kaseba wao wanaona nani ana uwezo wa kuendelea na pambano hilo.

Mashabiki wa ‘team’ Maugo wakaitikia kwa nguvu wakimtaja bondia wao kuwa ndiye mwenye uwezo wa kuendelea na pambano, kisa tu alikuwa amevaa glovu na mpinzani wake (Kaseba) alikuwa ameshavua za kwake.

Palepale, mwamuzi alimtangaza Maugo kuwa bingwa wa pambano hilo, huku uhasama wa mabondia hao ukianzia hapo na hata pambano lao la mwisho walilozichapa kwenye uwanja wa Kinesi, bado Kaseba hakuweza kulipa kisasi kwa Maugo kwani alipigwa kwa TKO.

Mdogo wa Cheka afanya kituko

Ilitokea kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kwenye pambano la bondia Francis Cheka na Said Mbelwa.

Kwenye pambano hilo, Cheka alimpiga Mbelwa ngumi ya kisogo, lakini mwamuzi Emmanuel Mlundwa akaonyesha ishara ya kukataa kuwa siyo faulo, Mbelwa mwenyewe alizunguka ulingoni akakutana na konde hilo.

Kitendo kile kilimkasirisha Mbelwa ambaye alikurupuka kama kifaru kwenda kumshambulia Cheka kwa ngumi na mateke.

Mdogo wa Cheka, Cosmas alipoona vile kwa haraka alichomoka kwa mashabiki na kuwapita askari kadhaa waliokuwa jirani na ulingo na kupanda na kwenda kuanza kuzichapa kavu kavu na Mbelwa.

Hata hivyo, kabla madhara hayajatokea, askari walivamia ulingoni na kwenda kuamuali ugomvi wa Cosmas na Mbelwa, huku Cosmas akiondolewa haraka na pambano liliendelea ingawa Mbelwa alipigwa kwa TKO.

Shabiki amvamia bondia ulingoni

Ulishawahi kuona mieleka namna mpinzani anavyoingia ndani ya ulingo na kumtupa nje bondia wa timu pinzani? ndicho kilitokea kwenye pambano la Japhet Kaseba na Francis Cheka kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Kilitokea kituko cha mwaka kwa baunsa aliyejulikana kwa jina la Khalifa kupanda ulingoni na kumnyanyua Cheka juu juu na kumtupa nje ya ulingo.

Ilitokea baada ya Kaseba kushambuliwa na kupigwa konde kali lililomtoa hadi nje ya ulingo, wakati Cheka akisubiri kutangazwa bingwa, shabiki huyo alipanda kwa kasi ulingoni na kumnyanyua Cheka na kumrusha nje ya ulingo na kumfuata Kaseba.

Kitendo kile kiliibua tafrani na pambano liliishia hapo lakini baadaye Cheka alitangazwa bingwa wa pambano.

Bondia apiga mashabiki

Ilitokea kwenye pambano la Awadh Tamim na Ashrafu Suleiman kwenye ukumbi wa DDC Mwenge baada ya Tamim kutangazwa bingwa kwa Knock Out (KO). Raundi mbili za awali, Tamim alitembezewa kipigo cha maana kilichompeleka chini mara tatu, lakini ilipoanza raundi ya tatu, bondia huyo alimchapa konde la kidevu mpinzani wake lililompeleka chini moja kwa moja na pambano liliishia hapo.

Baada ya kutangazwa mshindi kwa KO, Tamim alianza kurusha viti vya ukumbini hapo na kupiga mashabiki akidai aletewe gari aina ya ‘Vogue’ aliloahidiwa kama atashinda pambano hilo.

Mabaunsa wanne walifanya kazi ya ziada kumkamata na kumpakiza kwenye gari kabla ya kumpeleka hospitali.

Bondia abinuka sarakasi ulingoni

Ilikuwa kali ya mwaka kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee katika pambano kati ya Rashid Ally kutoka Keko na Rogers Mtagwa aliyekuwa akitokea kwenye kambi ya Steven Ngonyani ‘Majimarefu’.

Raundi ya tatu ya pambano, Ally alimchapa ngumi ya taya Mtagwa na kwenda moja kwa moja chini, mwamuzi akiwa anasogea ili kumhesabia hata kabla hajaanza kuhesabu bondia huyo alinyanyuka kwa staili ya kama anaruka sarakasi na kufuta glovu kuashiria anaendelea na pambano.

Mwamuzi alipoanzisha pambano, Mtagwa alimpiga ngumi mfululizo Ally ambaye naye alikwenda chini na alinyanyuka akitumia staili ile ile iliyotumiwa awali na mpinzani wake, na kuwafanya mashabiki wake kulipuka kwa furaha ukumbini, ingawa pambano lilimalizika kwa matokeo ya sare.

Chanzo: mwananchi.co.tz