Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabao ya vichwa Abeid Mziba hakuiacha Simba salama

44787 Simba+pic Mabao ya vichwa Abeid Mziba hakuiacha Simba salama

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Miaka ya nyuma, Yanga kulikuwa na mtu mmoja matata pale mbele, huyu alikuwa anaitwa Issa Athumani Mgaya. Mgaya alikuwa fundi wa mpira ya kichwa. Mungu ampe Amani ya milele.

Mgaya alikuwa akikaa mwisho wa goli hivi akiisubiri krosi au mpira wa kona, na mpira ukimkuta wa kichwa, hakuachi. Lazima mrudi kati. Issa sasa yuko mbele za haki, lakini nafasi yake kwenye soka ya Tanzania ipo kwani alikuwa mmoja wa wachezaji mahiri Taifa Stars.

Lakini pia kulikuwa na mtu anaitwa Abeid Mziba. Huyu jamaa hana mfano kwenye mipira ya vichwa. Mziba alikuwa fundi, si tunasema Issa alikuwa hakuachi, sasa Mziba omba Mungu asikutane na mpira unaotua mbele ya paji la uso au kile kichwa cha uchinjo juu kidogo ya sikio, aaah hakuachi salama.

Mziba alikuwa mwisho kwa mipira hiyo. Alifunga katika mazingira yoyote yale. John Bocco wa Simba ni kama anataka kumuiga hivi kufunga mpira ya kichwa japo anajaribu, lakini hakuna, Mziba alikuwa namba nyingine.

Waliomfahamu nyota huyo, wanamtaja alikuwa mkali kwa kufunga mabao mengi ya kichwa kuliko aliyotumia mguu, kumbe siri ya ufungaji huo ilikuwa hivi....

“Unajua kufunga kwa kichwa ni ujasiri, lakini pia kufunga kwa stahili hiyo kuna raha yake,” anaanza kusimulia Mziba katika mahojiano maalumu na Mwananchi.

Anasema japo mabao aliyowahi kufunga kwa mguu yapo, lakini mengi amefunga kwa kichwa.

“Magoli ya vichwa niliyofunga ni mengi sana, lakini sikuwahi kufanya mazoezi ya kufunga kwa kichwa. ilitokea tu nikiliangalia goli, nikipiga nalenga palepale na linakuwa goli,” anasema.

Mziba anasema alikuwa akifunga mabao ya kichwa ya uamuzi, kwani kufunga kwa kichwa ni kitendo cha ujasiri kwani mpira unapopigwa krosi haupigwi kwa spidi ndogo.

“Wachezaji wengi wanapouona mpira ule umepigwa kwa nguvu wengi uwa wanafumba macho, bahati nzuri mimi wakati nacheza sikuwa na kawaida ya kufumba macho, hivyo mpira nilikuwa nauona,” anasimulia.

Anasema kilichokuwa kikimbeba ni urefu wake, lakini pia alikuwa na uwezo mkubwa wa kuruka katika kuwania mipira ya krosi au kona, ndiyo sababu aliweza kufunga mabao mengi ya kichwa.

“Unajua shingo na kifua vinazunguka, hivyo nilikuwa naweza kuruka juu zaidi na kuzunguka mwili mzima ndiyo sababu nilikuwa nafunga kirahisi,” anasimulia.

Mziba anasema yapo mabao ambayo amefunga kwa mguu, lakini aliyofunga kwa kichwa ni mengi zaidi na yalipendwa na watu.

“Mabao ya vichwa yana raha yake, japo sasa hivi siyaoni sana kwenye soka letu, ingawa kina Tambwe (Amiss) na Makambo wanajaribu ila sio mabao ya raha kama enzi zetu,” anasema.

Mabao yake ya vichwa

Mziba anasema kutokana na umahiri wake wa kufunga mabao ya vichwa, hivyo akaamua kujipozisheni kwenye ufungaji wa mabao ya vichwa.

“Ilifikia hatua hata kwenye klabu yangu, wakiona tumekamatika, tunakubaliana tutafute kona moja ambayo wachezaji wenzangu walijua ikipigwa tu, lazima tupate bao na kweli ilikuwa ikitokea nafunga.

Anasema ilikuwa inatokea timu yao ikikamatika kwenye mechi, wanaona hawana namna hivyo bora watafute kona ili yeye Mziba afunge, kwani walimuamini kuwa ikipigwa kona tu lazima afunge.

Ataja beki iliyokuwa ikimsumbua

Mziba licha ya utaalamu wake wa kupachika mabao ya kichwa anasema enzi anacheza pia kulikuwa na beki matata ambayo ikitokea wanacheza na timu yao, basi halali.

“Wakati ule kulikuwa na mabeki hatari, mfano Simba walikuwepo kina Daud Salum, Kajole, Lilla Shomari, hata klabu zingine kama CDA ya Dodoma walikuwepo kina Charles Mngodo, Majimaji kulikuwa na Peter Mhina, Spazo Athuman ambaye ni marehemu kwa sasa.

“Walikuwa mabeki kweli, tofauti na sasa ukiwaangalia mabeki wetu unamuona kama beki kilo moja, lakini zamani fowadi ukiruka unaruka na uzito, lakini beki naye unakuta sio mtu wa masihara.

Kimo kinahusiana vipi na mpira?

Mziba anasema kwenye soka la sasa nchini, maumbile ya mpira yamepotea, tofauti na walivyokuwa enzi zake akicheza soka.

“Simaanishi kama kama enzi zetu wachezaji wafupi hawakuwepo, walikuwepo! lakini walikuwa na kitu cha ziada Mungu kawapa.

“Hata Yanga tulikuwa na mchezaji mfupi, lakini alikuwa mipira yote ya juu anagusa pamoja na ufupi wake, tofauti na sasa.

Kimo kwenye soka kina faida gani?

Mziba ambaye ni mrefu, lakini pia ana mwili wa mazoezi anasema kimo kwenye soka ni kitu cha kwanza kwa mchezaji.

“Tusiangalie tu Tanzania, hata Ulaya kuna wachezaji wanacheza kwa kimo chake tu, mwili na urefu wake tu ni fimbo ya kuwasumbua mabeki.

“Hata kocha, atamuangalia mchezaji kimo kisha kipaji chake, kwenye mpira kwanza ni kimo, popote pale duniani, cha pili ni kipaji, japo kuwa huna kimo lakini una kipaji hilo ni suala jingine, lakini makocha wengi duniani wanaanza kuangalia kimo,” alisema. Mziba alitolea mfano namba tisa wa Al Ahly iliyocheza na Simba Dar es Salaam hivi karibuni katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Yule namba tisa wa Al Ahly wala hakuwa fiti kisoka, lakini kimo chake tu kilimbeba kwani alikuwa akipata mpira anasumbua mabeki, wachezaji kama hao wanakuwa hatarishi.

Eti Mziba hakuitaka Yanga

Mziba anasema hakuwahi kufikiri kama kuna siku angechezea klabu kubwa kama Yanga, ingawa alikuwa akiifuatilia tangu akiwa kwao Kigoma.

“Yanga ilikuwa ikicheza naifuatilia kwenye redio, hakuna siku ambayo Yanga ilicheza nisifuatilie, lakini watu walikuwa wakiniambia kuwa naweza kuichezea timu hiyo, niliwakatalia kuwa haiwezekani.

“Lakini nikajikuta tu natoka Kigoma, naenda Dodoma ambako nilijiunga na Reli Dodoma, baadaye nikaenda RTC Kagera, Yanga walinionea Zanzibar, tulikuwa kwenye Ligi.

“Zamani kulikuwa na Ligi ya makundi, sisi tulicheza na Simba Dar es Salaam baada ya hiyo mechi tulikwenda Zanzibar,kwenye mashindano,kule ndiko walinionea, japo kuwa Yanga wakati ule ilikuwa na fowadi nzuri, lakini wakanifuata kufanya mazungumzo, wala sikutaka kujivunga, maana ile ndiyo timu ya Wananchi.

Anasema wakati ule Yanga ikikutaka kwanza unaogopa, kwani ilikuwa ni kama Barcelona au Mancester ya Tanzania, ingawa mwanzo aliona kama haiwezekani kujiunga na timu hiyo, lakini alijiamini hasa baada ya watu wengi kuonekana kukubali kiwango chake na yeye akaamua kujiamini kuwa ataweza na kweli akaweza.

Alivyotua Yanga

“Niliikuta Yanga ikiwa na mastaa kibao, nilimkuta Omary Hussein, marehemu Juma Mkambi, Boniface mwenyewe (Charles Mkwasa), Shaaban Katwila, Ally Shomari, Charles Kilinda na wengine wengi, Yanga ilikuwa ina wachezaji ukiwataja majina yao, unaogopa.

“Lakini nikasema hapana, sikutaka kuendekeza hofu juu yao, nilijua nitapambana na nilijiwekea malengo ya kupambana ili kupata namba.

Anasema baada ya muda timu hiyo iliongeza wachezaji wengine ambao waliungana na Hussein Iddi, Makumbi Juma na Juma Kampala, wakawa na timu bora yenye vipaji. “Timu yetu ya wakati ule, Simba kila ikicheza na sisi tulikuwa tunampiga, tulikuwa na timu nzuri wakati ule, halafu tulizoeana na wachezaji wengi walikuwa na vipaji kwenye timu yetu, Simba halikuwa hatuwezi.

Anasema msimu wa 1983/1984, Yanga ilicheza msimu mzima bila kufungwa kutokana na ubora wa kikosi chao, kwani walikuwa na kikosi kipana cha timu mbili zenye uwezo wa kucheza mechi mbili kwa wakati mmoja.

“Tulikuja kufungwa kwenye Ligi ya Muungano na Small Simba bao 1-0 na tulipokuja kurudiana tukawafunga 4-0, wakati ule tulikuwa na kikosi kipana.

Ushirikina mechi za mahasimu

Mziba anakumbuka enzi zao namna walivyokuwa wakijiandaa kila walipokutana na watani zao Simba, sio kwa mazoezi ya uwanjani tu, hadi mambo ya ushirikina yalikuwepo.

“Unajua mechi za Simba na Yanga uwa zinabaki kwenye kumbukumbu za watu, mechi ya Simba na Yanga kila upande unahangaika kujiandaa, haijawahi kutokea timu hizi zinacheza halafu ukute moja wapo inauchukulia mchezo huo kama kawaida, ni kitu ambacho hakiwezekani,” anasema.

Anasema kila moja uwa inahangaika kujiandaa na hata ushirikina uwa unafanyika, lakini ameufananisha ushirikina huo na kama kachumbari kwenye pilau.

“Ushirikina unafanyika kwenye mechi hizi, lakini hauutegemei sana, huo unakuwepo lakini pia na timu ifanye juhudi, ile ni kama kachumbari tu kwenye pilau, hata isipokuwepo utakula pilau, hivyo ushirikina nao bila juhudi haukusaidii kupata magoli.” Anasema ukijiandaa vizuri, kachumbari haikusaidii kupata magoli kwenye mpira.

“Yanga zamani tulikuwa na mtu mmoja alikuwa akituambia kabisa leo matokeo yatakuwa hivi na kweli inatokea, lakini mfanye juhudi, hivyo mambo hayo yalifanyika lakini ilikuwa ni kama kachumbari tu kwenye pilau. Kisa Simba, aingia na majeraha

Mziba anakumbuka moja ya mechi za Simba na Yanga ambapo hadi dakika ya 80, timu hizo zilikuwa zimemaliza kwa sare ya 1-1. Anasema katika mechi hiyo iliyochezwa 1989, alimuomba kocha aingie kucheza dakika 10 tu, ingawa kocha alimuweka nje kwa kuwa alichanika nyama za mguu.

Mziba anasimulia hali ilivyokuwa wakati huo Yanga inapofungwa na Simba. Kulitokea nini, wachezaji na viongozi walifanya nini? Fuatana na Spoti Mikiki wiki ijayo kukupa simulizi tamu



Chanzo: mwananchi.co.tz