Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maagizo ya serikali kwa waamuzi wa mpira nchini

Large 1621688334 IMG 20210521 WA0024 Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul

Wed, 11 Aug 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amewataka waamuzi wa michezo kufanya maamuzi ya haki na kuepuka upendeleo pindi wanapotekeleza majukumu yao ili kuepusha migogoro na migongano ambayo imekuwa ikijitokeza kutokana na waamuzi kukiuka misingi ya majukumu yao.

Naibu Waziri Gekul ameyasema hayo leo Agosti 10, 2021 alipotembelea kambi ya mafunzo ya makocha na waamuzi yanayoendelea Babati Mkoani Manyara ambapo mafunzo hayo yamehusisha makocha na waamuzi kutoka mikoa mbalimbali nchini.

“Taaluma na mafunzo mnayopata mkayatumie vizuri kwa kufanya maamuzi ya haki michezoni, tumeshuhudia migogoro mingi sana na malalamiko yakihusisha waamuzi kusimamia maslahi binafsi, hiyo inasababisha wanamichezo kuvunjika moyo na hata kupelekea michezo kutosonga mbele, nendeni mkasimamie haki na kuepuka maslahi binafsi”, alisema Naibu Gekul.

Aidha Naibu Waziri Gekul ametoa rai kwa viongozi wa Taasisi mbalimbali Nchini kutoa ruhusa pamoja na kuwawezesha Maafisa michezo ili waweze kushiriki mafunzo mbalimbali kwa kuwa fedha zinatengwa na hilo litachangia kukuza Sekta ya michezo kwenye ngazi mbalimbali .

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Judith Ilunda amesema moja ya changamoto kubwa wanazokabiliwa nazo ni baadhi ya Maafisa ambao hawana sifa kuchukuliwa na kutumiwa kama Walimu wa Michezo kwa Shule za Msingi na Sekondari.

“Hawa Maafisa wanaohudhuria mafunzo haya wanakuwa na vyeti vya Kitaifa na wanakuwa na ujuzi wa kutosha, Maafisa elimu wawatumie hawa kwenye mafunzo ya michezo Mashuleni”, alisema Judith Ilunda.

Kwa upande wake Mkufunzi Mkuu wa mafunzo hayo, Kim Christophe amemshukuru Naibu Waziri kwa kuwatembelea na kuwatia hamasa kwa niaba ya Serikali huku akiomba Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutafuta wadhamini wa Netiboli.

Mafunzo hayo yamehusisha maafisa michezo wa mikoa na halmashauri mbalimbali nchini pamoja na walimu wa mchezo wa netiboli yameanza Agosti 01, 2021 na yanafanyika kwa siku 14 ambapo Mhe. Gekul ametoa mchango wa shilingi milioni moja kwa ajili ya kufanikisha mafunzo hayo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live