Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MTIBWA YAIPANIA SIMBA

47b5bbc38fb32871c09c6f7b83ac12bb.jpeg MTIBWA YAIPANIA SIMBA

Thu, 10 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TIMU ya Mtibwa Sugar imesema inajua namna ya kuwakabili mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Simba, katika mchezo ujao utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Wakatamiwa hao wa Manungu wamesema katika mchezo huo watashusha kikosi kamili walichosajili msimu huu baada ya baadhi yao kutochezeshwa katika mchezo uliopita dhidi ya Ruvu na kutoka suluhu.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha wa Mtibwa, Zuberi Katwila, alisema wanajua wapinzani wao ni mabingwa watetezi hivyo, wanajipanga kupambana wakijua wanakwenda kukutana na timu ya aina gani.

“Sisi tunaendelea vizuri na maandalizi huku Manungu, tunajua tunakwenda kukutana na mabingwa watetezi, ni lazima tupambane tukijua wapinzani wetu ni watu wa aina gani, tunajua tutakuja na mbinu gani,” alisema.

Msemaji wa kikosi hicho, Thobias Kifaru ‘Ligalabwike’, alitamba hawatakubali kufungwa kirahisi na Simba licha ya kufahamu ubora wa wapinzani wao. Alisema mchezo huo unaweza kuwa mgumu kwani Simba watakuwa wanataka kuwaonesha Watanzania ubora wao.

“Simba ni timu nzuri ndio mabingwa mara tatu, usajili wao msimu huu ni wa nguvu na wametengeneza muunganiko, lakini kwetu hatutakubali kwani huu mwaka tumepanga kufanya vizuri na kuchukua taji la ligi,” alisema.

Alisema wapo wachezaji wapya waliosajiliwa msimu huu wakiwemo wafungaji bora kutoka Zanzibar na kumrejesha beki Hassan Kessy aliyekuwa Zambia watawachezesha mchezo huo.

Kifaru alisema yaliyowakuta msimu uliopita hawataki yajirudie, hivyo ni lazima wapambane kwa juhudi na kufanya vizuri kuanzia mechi zao za awali ili kuwa katika nafasi nzuri.

Alisema malengo yao kama sio kuchukua taji, basi ni kuhakikisha wanamaliza ligi katika nafasi tatu za juu, huku akikiri ligi itakuwa ngumu kutokana na kila timu kujiandaa vizuri.

Aliiaomba Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwalipa waamuzi posho zao mapema ili wachezeshe kwa haki. “Waamuzi wanatakiwa wapewe stahiki zao mapema ili wawe makini, wafanye kazi nzuri,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz