Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAANDALIZI 2019 Utaipenda tu Serengeti Boys

Mon, 20 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukiwaangalia Serengeti Boys wanavyocheza, wanavyoshinda na wanavyoonana, utatamani mpira usimalizike lakini Fifa wameweka dakika 90 labda iwe mashindano hadi dakika 120.

Hiyo ndiyo Serengeti Boys, timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya Tanzania ambayo kesho inacheza na Rwanda mechi yake ya kusaka wa kwanza na wa pili katika Kundi A.

Tanzania na Rwanda zimeshafuzu kutoka kundi lao wakisubiri timu nyingine kutoka Kundi B.

Gumzo kila kona

Timu hii imegeuka gumzo kwenye mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo kupitia Ukanda wa nchi zinazounda Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) yanayoendelea jijini kutokana na kiwango na matokeo bora ambayo wamekuwa wakiyapata.

Serengeti Boys inaongoza Kundi A la mashindano hayo ambayo mshindi wake atafuzu Fainali za Afrika mwakani ikiwa na pointi sita sawa na Rwanda inayoshika nafasi ya pili ingawa inabebwa na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa iliyo nayo tofauti na wapinzani wao.

Mchezo wa kwanza iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa jijini kabla ya kupata ushindi mnono wa mabao 5-0 mbele ya Sudan katika mechi ya raundi ya pili ya kundi lake iliyochezwa Alhamisi ya wiki iliyopita.

Hata hivyo Serengeti Boys inashiriki mashindano hayo kama sehemu ya mazoezi tu kwani tayari imeshajihakikishia kufuzu Fainali za Afrika zitakazofanyika nchini mwakani kwa sababu zitaandaliwa hapa nchini hivyo na kikanuni, timu mwenyeji huwa inafuzu moja kwa moja.

Kiwango bora cha Serengeti Boys katika mashindano hayo kimetokana na muunganiko mzuri ambao timu hiyo imekuwa nao kuanzia kwenye safu ya ulinzi hadi ile ya ushambuliaji, jambo ambalo limeifanya iwe moto wa kuotea mbali katika kutengeneza nafasi na kufunga mabao lakini pia limepelekea kikosi hicho cha timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 cha Tanzania kuwa miongoni mwa timu zenye safu imara zaidi za ulinzi, ikiwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu.

Mbinu ambayo imekuwa chachu ya mafanikio kwa Serengeti Boys katika mashindano hayo ni ile ya kucheza soka la pasi nyingi zinazoanzia kwenye safu yake ya ulinzi kuelekea langoni mwa timu pinzani ambazo hupigwa huku wachezaji wa timu hiyo wakiwa wanapishana kwa haraka kwenye nafasi kwa lengo la kuchanyanya mabeki na kufungua ukuta wa wapinzani wao.

Kasi na uamuzi wa haraka ambao wachezaji wa Serengeti Boys wamekuwa nao, umesaidia kuifanyia kazi kwa ustadi mbinu hiyo ambayo imekuwa ikizaa matunda kwani mara kwa mara imekuwa ikiifanya mara wapinzani wao wasiwe wanashambulia na badala yake hulazimika kutumia muda mrefu wakiwa kwenye lango lao ili kudhibiti vijana hao wa Tanzania wasilete madhara.

Pindi Serengeti Boys inapokuwa na mpira, mawinga wake wamekuwa wakiingia ndani na kuacha nafasi kwa mabeki wa pembeni kupanda kwa kasi kupiga krosi au kutengeneza mashambulizi kutokana na pasi ambazo wamekuwa wakipigiwa na wachezaji wanaocheza safu ya kiungo.

Lakini pale wanapopoteza au mpira unapokuwa miguuni mwa timu pinzani, nyota hao wa Serengeti Boys wamekuwa ni wepesi kurudi kwa haraka nyuma kuwahi kuziba mianya ambayo inaweza kuwavutia wapinzani wao kutengeneza nafasi na kufunga mabao, mbinu ambayo imekuwa ikichangia lango lao kuwa salama katika sehemu kubwa ya mchezo.

Nyuma ya mafanikio haya ya Serengeti Boys liko benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu, Oscar Milambo anayesaidiwa na nyota wawili wa zamani wa Yanga, Maalim Salehe (Kocha Msaidizi) na Kocha wa Makipa, Manyika Peter.

Nyota muhimu

Sifa kubwa ya Serengeti Boys hii ya sasa ni kucheza kitimu lakini bado kuna nyota ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa ndio wakiiendesha timu kutokana na uwezo wao wa kusoma mchezo na kuwaongoza wenzao ndani ya uwanja katika kutengeneza mashambulizi na kumiliki mpira ambao ni viungo Morice Abraham, Mustafa Nankuku pamoja na mshambuliaji Kelvin John.

Mustafa Nankuku anayecheza namba sita, amekuwa na uwezo wa hali ya juu wa kung’amua mashambulizi pamoja na kutibua mipango ya timu pinzani lakini pia amekuwa na sifa ya kuchezesha timu kwa pasi zake ambazo zimekuwa zikifikia walengwa kwa usahihi.

Mbele ya kiungo huyo, yupo nahodha Morice Abraham ambaye ndiye mchezeshaji mkuu wa timu hiyo kutokana na ufundi wake wa kuwasoma na kuwapenya viungo na mabeki wa timu pinzani na kupiga pasi za mwisho kwenda kwa washambuliaji wa timu hiyo lakini pia amekuwa na uwezo wa kumiliki mpira kwa muda mrefu bila kupokonywa jambo ambalo husaidia kuipumzisha na kuituliza timu pale wenzake wanapoonekana kuchoka.

Lakini mwisho wa siku kuna juhudi za kitimu zimekuwa zikitendewa haki na mshambuliaji Kelvin John ambaye amekuwa na kipaji cha hali ya juu cha kufumania nyavu na kuwasumbua mabeki jambo ambalo limekuwa likisaidia kuwafanya wapinzani wasiwe wanapanda mara kwa mara ili kumchunga nyota huyo.

Udhaifu

Penye mafanikio huwa hapakosi changamoto na kasoro. Pamoja na ubora wa kikosi cha Serengeti Boys, wamekuwa na changamoto kubwa ya kujisahau na kupiga chenga zisizo na sababu hasa pale wanapokuwa wanaongoza jambo ambalo limekuwa likisababisha wapoteze mipira kwenda kwa timu pinzani ambayo ikiwa zingekuwa zinatumia vizuri nafasi, zingezaa mabao.

Changamoto nyingine ambayo benchi la ufundi la Serengeti Boys linapaswa kuifanyia kazi ni udhaifu wa safu ya ushambuliaji katika kujipanga pindi timu inaposhambulia, jambo linalopelekea ipoteze idadi kubwa ya nafasi za mabao ambayo inatengeneza ama kujikuta wanaotea mara kwa mara hakuna mmaliziaji.

Pamoja na kucheza ndani ya uwanja, inatakiwa mambo ya kiufundi, kama kupiga mipira iliyokufa. Fainali za Kombe la Dunia za Russia, mipira iliyokufa ilitumiwa kikamilifu kupata mabao. Wachezaji wa Serengeti Boys hawana utaalamu wa kutafuta engo ya nyuzi 90 au 80 ya goli kwa juu ambazo hakuna makipa wanaoweza kuzifikia.

Udhaifu mwingine unaotakiwa kurekebishwa haraka ni ufundi wa kupiga penalti. Penalti ya Salum Lupepo ilionyesha wazi kwamba vijana hawajaiva kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo penalti.

Haitakiwi mtu mmoja awe fundi na katika kufanikisha hili, inatakwa kila baada ya mazoezi, dakika 10 za mwisho ni mikwaju ya penalti kwa kila upande.

Ukiacha hayo, vijana hao wanaonekana wanahitaji mechi nyingi za kirafiki dhidi ya timu kutoka nchi ambazo zimepiga hatua kubwa kisoka kama Nigeria, Tunisia, Morocco, Misri, Mali, Cameroon, Senegal, Ghana na Guinea ili wapate uzoefu utakaowafanya waingie kwenye fainali za Afrika wakiwa fiti na wamepevuka.

Utofauti na Serengeti Boys ya Gabon

Mwaka jana, Serengeti Boys ilishiriki fainali za Afrika kwa vijana wenye umri huo ambazo zilifanyika Gabon na kushika nafasi ya tatu kwenye kundi B lililokuwa na timu za Mali, Guinea na Angola.

Baadhi ya wadau wa soka nchini wamekuwa wakijiuliza ni kikosi kipi bora cha Serengeti Boys baina ya hiki cha sasa na kile cha mwaka jana kilichoshiriki Fainali za Afrika ambazo hata hivyo mwakani tutashiriki tena tukiwa kama wenyeji.

Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za Gabon, yenyewe haikuwa inacheza soka la pasi nyingi lakini pia ilikuwa haimiliki sana mpira huku ikitumia nguvu kubwa katika kujilinda lakini hii ya sasa imekuwa ikicheza soka la kushambulia na kupiga pasi nyingi huku ikiufungua uwanja jambo linalofanya yenyewe iwe na mpira kwa muda mrefu kuliko timu pinzani.

Maoni ya wadau

Kocha wa Sudan, Zdravko Logalusic anaamini Serengeti Boys ni timu tishio zaidi kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ingawa ameshauri kuwe na mfumo mzuri utakaowafanya wawe tegemeo kwa timu ya taifa siku za usoni. “Ni vijana wadogo lakini wananyesha utofauti na wengine kwani wamepevuka na wanatambua wafanye nini na kwa wakati gani ingawa kuna muda wanajisahau na kucheza kama wanafunzi. Nadhani ndio timu iliyoandaliwa kwa muda mrefu na nawapongeza Tanzania kwa hilo lakini changamoto kubwa kwa bara la Afrika ni namna gani wachezaji hawa wataendelezwa hadi wawe nyota muhimu kwenye timu ya taifa,” anasema Logalusic.

Kocha wa timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya Rwanda, Rwasamanzi Yves alitoa ushauri kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuitafutia Serengeti Boys mechi nyingi za kirafiki ili iweze kuimarika.

“Tanzania (Serengeti Boys) ni timu nzuri na ninaamini italeta ushindani kwenye mashindano ya Afrika lakini nadhani wanatakiwa kutafuta mechi za kutosha za kirafiki ili wazidi kupata uzoefu utakaowasaidia waweze kuhimili ushindani na kumaliza kwenye nafasi za juu,” alisema Yves.

Kabla ya kushiriki fainali zilizofanyika Gabon mwaka jana, Serengeti Boys iliweka kambi kwenye nchi za Madagascar, Shelisheli, Morocco na Cameroon ambako ilicheza idadi kubwa ya mechi za kirafiki ingawa hii ya sasa bado haijafanikiwa kutoka nje ya nchi kuweka kambi japo imekuwa ikicheza mechi za kirafiki na klabu mbalimbali hapahapa nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz