Dar es Salaam. Wajumbe wa kamati ya Utendaji wa Yanga, Thobias Kingalangala na Samwel Lukumay wametoa kali ya mwaka kila mmoja akijitambulisha kuwa ni kaimu makamu mwenyekiti wa Yanga.
Walioudhuria kikao hicho kwa upande wa Yanga ni Jaji John Mkwawa, Hussein Nyika, Siza Lyimo, Lingalangala na Lukumay, wakati TFF iliwakilishwa na rais Wallace Karia, Makamu wa rais wa TFF, Athuman Nyamlani, na mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa TFF, Ally Mchungahela.
Utambulisho wa vigogo hao ulimshtua waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na michezo, Dk Harrison Mwakyembe ambaye alidai hali ilivyo inaonekana Yanga kuna fukuto.
Waziri Mwakyembe amekumbana na kioja hicho alipokutana na viongozi wa Yanga, TFF na Serikali kwa ajili ya kuhitimisha sintofahamu ya mvutano uliopo kuhusu uchaguzi wa Yanga utakaofanyika Januari 13.
Kabla ya kikao kuanza, waziri aliwataka wajumbe kujitambulisha, ndipo Lukumay alipojitambulisha kama kaimu Mwenyekiti wa Yanga.
Ilipofika zamu ya Lingalangala yeye alijitambulisha kuwa Kaimu Mwenyekiti wa Yanga halali ambaye ameteuliwa kwa kufuata taratibu zote.
"Kitendo hiki tu kinaonyesha Yanga kuna fukuto, haiwezekani klabu yenye wajumbe wanne pekee wa kamati ya Utendaji, wawili wanajitaja kuwa wana kaimu nafasi ya Mwenyekiti," alisema Mwakyembe.
Kikao hicho kinaendelea ili kupata mwafaka, ingawa awali Mwakyembe amesisitiza kuwa jambo hilo litaisha na uchaguzi utafanyika.