Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ligi Kuu yaanza kwa mabadiliko makubwa

74029 Ligi+pic

Tue, 3 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 umeanza rasmi Agosti 24 na utaendelea hadi ifikapo mwezi Mei mwakani wakati utakapohitimishwa rasmi.

Raundi ya kwanza ya ligi hiyo msimu huu ilihusisha mechi zilizokutanisha timu za Namungo iliyocheza dhidi ya Ndanda, Alliance iliyowakabili Mbao, Biashara iliyokutana na Kagera Sugar, Lipuli dhidi ya Mtibwa Sugar, Mbeya City na Prisons, Polisi Tanzania na Coastal Union, KMC na Azam FC, Yanga iliwavaRuvu Shooting wakati mabingwa Simba walikutana na JKT Tanzania.

Ufunguzi huo wa Ligi Kuu msimu huu uliambatana na mambo na matukio mbalimbali ambayo kwa namna moja au nyingine yanaacha kumbukumbu kwa klabu, mashabiki, wachezaji na hata mamlaka zinazosimamia mchezo wa mpira wa miguu nchini.

Spoti Mikiki linakuangazia baadhi ya mambo yaliyojiri katika ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Mechi za Watani

Kulikuwa na mechi nne za watani wa jadi zilizohusisha timu mbili zinazotoka katika mkoa mmoja au kwenye maeneo yanayokaribiana ambazo kwa kiasi kikubwa ziliwagawa mashabiki katika kuchagua upande wa kushangilia.

Pia Soma

Advertisement   ?
Mechi ya kwanza ni ile ya wapinzani kutoka Kanda ya Kaskazini iliyozihusisha Polisi Tanzania ya Kilimanjaro ambayo ilikutana na Coastal Union ya Tanga na Polisi kuibuka na ushindi wa bao 1-0. Nyingine ni ile ya jiji la Mwanza baina ya Mbao FC na Alliance FC zilizotoka sare ya bao 1-1.

Kulikuwa na vita ya Kusini ambayo Namungo waliibuka vinara kwa kuichapa Ndanda FC, mabao 2-1 na pia ile ya Mbeya iliyoisha kwa sare tasa kati ya Prisons na Mbeya City.

Mdhamini Mkuu

Baada ya kusota kwa msimu mmoja bila ya uwepo wa mdhamini mkuu, hatimaye msimu huu umeanza vizuri baada ya Kampuni ya Huduma za Mawasiliano ya Vodacom Tanzania kurudi tena na kuidhamini Ligi Kuu Bara kwa mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Sh 9 bilioni.

Kupitia mkataba huo, inakadiriwa kwamba kila klabu ya Ligi Kuu msimu huu itavuna kiasi kinachofikia Sh100 milioni.

Ukijumlisha na fedha ya udhamini wa haki za matangazo kutoka kampuni ya Azam Media, kila klabu inatarajia kuvuna kitita cha Sh 262 milioni kwa msimu huu pekee.

Miujiza ya Lipuli

Lipuli FC iliondokewa na kundi kubwa la wachezaji wake wanaounda kikosi cha kwanza mara baada ya msimu kumalizika na mbaya zaidi ikajikuta ikimpoteza kocha aliyesuka vyema kikosi chao msimu uliopita, Seleman Matola aliyetimkia Polisi Tanzania.

Ilitegemewa waanze ligi kwa kusuasua kwani hata maandalizi yao kwa ajili ya msimu huu yalichelewa lakini katika hali ya kushangaza, imeanza kwa kishindo kwa kuichapa Mtibwa Sugar kwa mabao 3-1.

Kwa kile ambacho wengi walikitegemea na matokeo ambayo yalipatikana ni wazi kwamba Lipuli imewashtua wengi.

Etienne vs KMC

Kitendo cha Azam FC kupangwa na KMC kwenye mechi ya kwanza kilimaanisha kuwa kocha Etienne Ndayiragije alikutana mapema na waajiri wake wa msimu uliopita ambao aliwaongoza kumaliza kwenye nafasi ya nne baada ya kupanda daraja huku pia wakifuzu kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, Etienne aliweka kando urafiki na uhusiano wake mzuri na KMC na kuiongoza vyema Azam FC kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi hiyo iliyochezwa katika Uwanja wa Uhuru jijini.

Bilali aweka rekodi

Athuman Bilali aliyekuwa anainoa Alliance anaweza kuwa ndio kocha aliyedumu kwa muda mfupi zaidi katika kibarua chake kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara tangu ilipoanzishwa.

Hiyo inatokana na uamuzi wa Alliance kufikia makubaliano ya kuachana na kocha huyo aliyewahi kuzinoa pia Toto Africans na Stand United muda mfupi baada ya kumaliza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Mbao FC uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kuvunjwa kwa mkataba huo kumetangazwa huku Bilali akiwa ameinoa timu hiyo kwa dakika 90 tu kwenye mechi moja ya ligi, jambo ambalo halikuwahi kutokea kabla.

Dar es Salaam yatamba

Mechi hizo za ufunguzi wa Ligi zilihusisha timu zote 20 za Ligi Kuu ambazo zinatokea katika mikoa tofauti nchini.

Hata hivyo, mashabiki wa soka na wakazi wa jiji la Dar es Salaam ndio ambao watakuwa wamefaidi zaidi kwani ndio kituo ambacho kimekuwa na idadi kubwa ya mechi kuliko vingine.

Jumla ya mechi tatu za Ligi Kuu zimechezwa jijini Dar es Salaam ambapo mechi ya kwanza ilikuwa ni baina ya KMC iliyochapwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC na mechi iliyofuata ilizikutanisha Yanga na Ruvu Shooting.

Alhamisi kukawa na mchezo mwingine ambao Simba ilishuka dimbani kuumana na JKT Tanzania wakati kwenye mikoa mingine kulikuwa na mechi mojamoja tu.

Makocha Stars watoana jasho

Mbali na kuwa mechi ya watani wa jadi wa Kanda ya Kaskazini, mchezo ambao Polisi Tanzania iliumana na Coastal Union, pia iliwakutanisha makocha wawili wasaidizi wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’

Polisi Tanzania wananolewa na Seleman Matola wakati Coastal Union wako chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na Juma Mgunda.

Hata hiyo, Matola alimzidi ujanja, Mgunda na kuiongoza timu yake kupata ushindi kwenye mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi ambao unatumiwa na Maafande wa Polisi Tanzania kwa mechi zake za nyumbani.

Ligi hiyo imesimama kupisha mechi za kimataifa.

Chanzo: mwananchi.co.tz