Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

"Licha ya kuifunga Kagera, Yanga haikucheza vizuri" - Kocha Kaze

Kaze Pic 1 Data Kaze Awafanyia Sapraiz Simba kwa Mkapa

Fri, 1 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

LICHA ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze ameweka wazi timu yao haikuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Mjini Bukoba juzi.

Kocha msaidizi wa Yanga Kaze amesema sababu kubwa ya kutoonyesha kiwango kizuri ni kutokana na kutumia nguvu nyingi kwenye mchezo uliotangulia wa kuwania Ngao ya Jamii ambao walikutana na watani zao, Simba.

Kocha huyo alisema hali hiyo waliitarajia lakini wanawapongeza wachezaji wao kwa kutumia uzoefu na hatimaye kuondoka na pointi zao tatu muhimu.

"Hatukuridhishwa na kiwango cha leo (juzi), lakini tunajivunia kupata pointi tatu. Tulicheza mchezo mgumu wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, tulitumia nguvu nyingi kwa hiyo tulijua leo (juzi), hatuwezi kuwa na nguvu kama zile tena.

Wachezaji wetu bado hawajarudisha nguvu kwa sababu mechi hiyo haikuchezwa muda mrefu, lakini kitu kizuri tumeshinda," alisema Kaze.

Aliongeza kama wangekuwa makini katika kipindi cha kwanza wangepata mabao matatu au manne, lakini walishindwa kuzitumia nafasi walizozitengeneza.

"Kama unaongoza bao moja, halafu unashindwa kutumia nafasi, unampa nguvu mpinzani wako. Na ndivyo ilivyotokea. Ukiondoa kufunga mabao, lakini umeona sasa wachezaji wanacheza kwa kupishana, wanafika hadi mbele ya goli. Kama wanafanya hivyo, basi kuna mambo kidogo ya kurekebisha ili timu iweze kutumia nafasi inazozipata," Kaze alisema.

Naye Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Francis Baraza alisema ameridhishwa na vijana wake, lakini akikiri amefungwa na timu bora.

"Tumefungwa na timu bora, nilisema hivyo tangu awali, lakini nimeridhika na vijana wangu. Kuna makosa madogo tumeyafanya kama yaliozaa bao, tutarudi mazoezini kuyafanyia kazi. Kuna wachezaji wetu wa kigeni ambao bado hawajapata vibali naamini watatusaidia kuelekea mchezo wetu wa pili dhidi ya Namungo," alisema Baraza.

Yanga imerejea jijini Dar es Salaam na kesho itashuka kwenye Uwanja wa Taifa kucheza dhidi ya Geita Gold FC huku Kagera Sugar itasafiri kuelekea Lindi kuwafuata Namungo kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani humo.

Chanzo: ippmedia.com